1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Risasi za fyatuliwa upya Bangladesh

26 Februari 2009

Hali bado si tulivu kuafuatia uasi wa wanajeshi walinzi wa mpakani.

https://p.dw.com/p/H1ZR

Taarifa kutoka Dhaka,mji mkuu wa Bangladesh, zinasema kwamba risasi zimefyatuliwa upya leo katika kambi ya wanajeshi mjini Dhaka huku vikosi vitiifu kwa serikali vikishika zamu majiani katika miji mbali mbali kote nchini siku moja baada ya watu 50 kuuwawa jana pale jeshi la walinzi wa mipaka lilipoasi likidai nyongeza ya mishahara.

"Risasi zilifyatuliwa tena leo katika kambi ya Jeshi la mpakani BDR ingawa tunatazamia uasi ...........kumalizika haraka."-alisema afisa wa POLISI ya Bangladesh. Visa vya ufyatuaji risasi juu ya jeshi la ulinzi wa mipaka BDR vimetokea katika zaidi ya miji darzeni moja.Hii ni kwa muujibu wa polisi.

Jukumu kubwa la kikosi hiki cha BDR , ni kulinda mipaka ya Bangladesh na mara kwa mara, hushirikiana na Jeshi rasmi na hata polisi ya Bangladesh katika kutekeleza shughuli zao.

Waziri mkuu wa Bangladesh bibi Sheikh Hasina, ametoa mwito wa kuwapo utulivu nchini,lakini uasi wa baadhi ya askari wa kikosi cha " Bangladesh Rifles "(BDR) kuhusu malipo bora , ulienea nje ya mji mkuu Dhaka hata baada ya kutangazwa kabla kuwa, hali ya mambo inadhibitiwa kutokana na msamaha uliotolewa na serikali.

Huduma za simu za mkononi zimekatwa kwa amri ya serikali ili kuzuwia kuenezwa kwa uvumi na taarifa zisizo sahihi.

Hapo kabla ,maafisa waliripoti kuwa watu 50 wameuwawa jana yalipozuka mapigano katika Makao Makuu ya kambi ya jeshi hilo la mpakani mjini Dhaka.Tukeo hili linaangaliwa kuwa pigo kali kwa matumaini kuwa, serikali ya bibi Hasina ilioshika madaraka mwezi uliopita tu,ingeweza kuleta hali ya utulivu ambayo ingewavutia watiaji raslimali nchini na kuhimiza maendeleo.

Bangladesh, nchi ya wakaazi milioni 140,ilikumbwa na mapinduzi kadhaa ya kijeshi tangu uhuru 1971,lakini uasi huu wa sasa, hauoneshi kufungamana na nia za kisiasa.Machafuko haya yanabainisha dhahiri-shahiri changamoto inayomkabili waziri mkuu Sheikh Hasina alieshinda uchaguzi mkuu wa Bunge Desemba iliopita -uchaguzi ambao uliirejesha Bangladesh katika demokrasia kufuatia kiasi cha miaka 2 cha utawala wa kijeshi.

Wachambuzi wanadai kuwa uasi huu wa wanajeshi, unampa mtihani mkubwa bibi Hasina kuliunganisha jeshi lake lenye nguvu ambalo limekuwa na uchu wa kujiingiza mara kwa mara katika siasa.