1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Hakuna ushahidi wa ushirikiano wa Trump na Urusi

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
25 Machi 2019

Ripoti iliyowasilishwa na mwanasheria maalum wa Marekani Robert Mueller haioneshi iwapo kuna ushahidi kwamba waendesha kampeni wa Rais Trump walishirikiana na Urusi katika kampeni ya uchaguzi wa Rais mnamo mwaka 2016.

https://p.dw.com/p/3FbVA

Robert Mueller zum Sonderanwalt für Russland-Sonde ernannt
Picha: picture-alliance

Kwa mujibu wa muhtasari wa ripoti ya Robert Mueller uliondaliwa na mwanasheria mkuu wa nchini Marekani William Barr, kwenye barua yenye kurasa nne iliyowasilishwa kwa kamati ya wabunge wa Baraza la wawakilishi katika bunge la Marekani, Barr, ameeleza kuwa uchunguzi uliofanywa na Robert Mueller haukuthibitisha iwapo Trump alifanya kosa la jinai.

Mwanasheria mkuu huyo amesema Mueller hakuwa na uhakika kwamba waendesha kampeni ya Trump walipanga au kuhusika na mpango wa serikali ya Urusi wa kuingilia kati ya uchaguzi wa Rais wa Marekani wa mwaka 2016. Akizungumzia juu ya ripoti hiyo Rais Trump amesema hana hatia.  Hatua hiyo inampa ushindi mkubwa wa kisiasa Rais Trump.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Makamu wa Rais wa Marekani Mike Pence amesema hitimisho la uchunguzi wa mwanasheria maalum Robert Mueller ni uthibitisho wa jumla kuwa Rais Donald Trump na waendesha kampeni yake wamevuliwa tuhuma mbaya mno na ni muhimu matokeo hayo kupokewa kwa furaha na Wamarekani wanaopenda ukweli na uadilifu uliokuwepo wakati wa uchaguzi. Pence ameiita siku iliyotolewa ripoti hiyo kuwa ni siku muhimu kwa taifa la Marekani, kwa rais Trump na Utawala wake. 

Mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje ya Urusi Konstantin Kosachev amesema hatua hiyo inatoa fursa ya kuufufua uhusiano kati ya Marekani na urusi.

Mwanasheria maalum Robert Mueller alitumia karibu miaka miwili kuchunguza madai kwamba Urusi iliingilia kati uchaguzi wa urais wa Marekani na kumsaidia Trump kumshinda mpinzani wake, Hillary Clinton. Lakini pia mwanasheria huyo mkuu amesema uchunguzi huo haujamwondolea Trump madai ya kuzuia sheria kutendeka.

Spika wa bunge Nancy Pelosi na kiongozi wa wa shughuli za bunge Chuck Schumer wote wanachama wa ngazi za juu wa chama cha Democratic wamesema  ripoti  hiyo inaibua maswali mengi kuliko majibu yaliyopo. Wademocrat wanataka ripoti yote ya mwanasheria maalumu wa Marekani Robert Mueller ichapishwe hadharani.

Vyanzo:p.dw.com/p/3Fb52RTRE/AP