1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rousseff amshutumu makamu wake Temer

Yusra Buwayhid13 Aprili 2016

Rais wa Brazil Dilma Rousseff amshutumu makamu wake wa rais kwa kupanga njama za kutaka kumpindua. Huku akiwa anakabiliana na kura ya kufunguliwa mashitaka ya kutumia vibaya uongozi, itakayoweza kumuondoa madarakani.

https://p.dw.com/p/1IURr
Brasilien Dilma Rouseff
Picha: Getty Images/AFP/E. Sa

Katika hotuba yake kali ya hivi karibuni Rousseff mwenye umri wa miaka 68 alisema makamu wake wa rais Michel Temer, pamoja na spika wa bunge la nchi hiyo Eduardo Cunya kwa pamoja wanapanga njama za kutaka kumuondoa madarakani.

"Kama kulikuwa na shaka yoyote kuhusu mapinduzi ya kijeshi, pamoja na usaliti ambao unaendelea, basi sasa hakuna shaka tena. Kama kulikuwa na shaka yoyote juu shutuma zangu za kuwa kuna mapinduzi ya kijeshi yanayopangwa, basi sasa shaka hiyo haipo tena. Kuna viongozi wawili wanaounga mkono mapinduzi hayo dhidi yangu, ” amesema Rousseff.

Katika hotuba hiyo, Rousseff alikuwa akizungumzia sauti iliyovuja aliyojirekodi Makamu wa Rais Michel Temer, akifanya mazoezi ya hotuba yake atakayoisoma pale Rousseff atakapotangazwa kufunguliwa mashitaka. Halikadhalika mwengine aliyemtaja kuhusika na mapinduzi hayo, ni spika wa bunge Eduardo Cunha.

Rousseff anashutumiwa kwa madai ya kutumia vibaya madaraka, kwa kupanga hesabu za uwongo zilizoficha athari za kweli za mgogoro wa kiuchumi wa mwaka 2014. Wakati alipotaka kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili madarakani.

Brasilien Präsident Dilma Rousseff und Michel Temer Vizepräsident
Rais wa Brazil Dilma Rousseff akiwa na makamu wake Michel TemerPicha: picture alliance/dpa/F. Bizerra Jr

Temer asema yupo tayari kuliongoza taifa

Makamu huyo wa rais Temer mwenye umri wa miaka 75, aliliambia wazi shirika la habari la Globo kwamba yupo tayari kumpokea madaraka rais Rousseff iwapo atafunguliwa mashitaka.

"Bila ya kujisifu na kwa unyenyekevu, naweza kusema nina uzowefu wa kutosha katika kazi za uongozi wa umma," amesema Temer.

Wabunge wanategemewa kuanza majadiliano siku ya Ijumaa, na kupiga kura ya maamuzi siku ya Jumapili, hayo ni kwa mujibu wa maafisa.

Msemaji mkuu wa ofisi ya spika wa Brazil ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa upigaji kura huwo utaanza Jumapili mchana na matokeo yanatarajiwa kutolewa jioni.

Iwapo theluthi mbili ya kura zitapigwa ndani ya bunge ambazo ni sawa na wabunge 342, basi kesi ya Roussefff itahamishiwa kwenye baraza la Seneti.

Baraza la Seneti litatakiwa kuthibitisha kuipokea kesi hiyo, na hatua itakayofuata ni kujiuzulu kwa Rousseff kwa siku 180 wakati ambapo atafunguliwa mashitaka rasmi. Temer ambaye hivi karibuni amejitoa katika serikali ya shirikisho ya Rousseff na kuunga mkono upande wa upinzani, anatarajiwa kuchukuwa nafasi ya kiongozi huyo.

Lakini iwapo kura zitakazopigwa zitakuwa shini ya idadi hiyo, Rousseff ataendelea na kazi yake ya urais bila ya shutuma zaidi.

Rousseff kwa hakika amepoteza umaarufu wake nchini Brazil, huku uchumi wa nchi hiyo ukiwa unaendelea kudorora. Halikadhalika mfumo mzima wa kisiasa umedhoofika, kutokana na kashfa kubwa ya rushwa iliyohusisha kampuni ya mafuta ya serikali ya Petrobras.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afpe/ape

Mhariri: