1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rowhani kuendelea kumsaidia Assad

4 Agosti 2013

Uongozi mpya wa Iran umeiahidi Syria kwamba hakutakuwa na mabadiliko yoyote kwenye muelekeo wa Iran kuelekea Syria na kwamba ushirikiano wa nchi hizo mbili utaendelea kama kawaida.

https://p.dw.com/p/19JXx
epa03748799 Iranian President-elect Hassan Rowhani greets media during a press conference in Tehran, Iran, 17 June 2013. President-elect Rowhani said on 17 June that Iran would be ready to reduce tensions with arch-enemy United States based on goodwill and mutual respect. 'With the US we have an old wound but we are still ready to look into the future and reduce tensions, but on the basis of goodwill and mutual respect,' Rowhani said. On the topic of Syria he said that Iran would continue supporting the government of Syrian President Bashar al-Assad until an election in 2014. EPA/ABEDIN TAHERKENAREH +++(c) dpa - Bildfunk+++
Iran Präsident Hassan Rowhani PKPicha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Iran, Rais Hassan Rowhani, ambaye ameapishwa leo (Jumapili, 4 Agosti) amemuahidi Waziri Mkuu wa Syria, Wael al-Halqi, kwamba hakuna kitakachobadili mahusiano hayo.

"Hakuna nguvu hata moja duniani inayoweza kuyatikisa mahusiano haya madhubuti, ya kimkakati na ya kihistoria yanayofungamanisha urafiki wa nchi hizi mbili," Rowhani alimwambia Halqi, ambaye alikuwa Tehran kuhudhuria kuapishwa kwa rais huyo mpya.

Shirika la Habari la Syria, Arab News Agency, lilimnukuu Rowhani akisema kwamba "uhusiano wa Syria na Iran umejengeka juu ya maelewano na hatima ya pamoja" na kwamba rais huyo mpya aliahidi "kuendeleza uungaji mkono wa Iran kwa watu wa Syria na serikali yao, ili kurudisha amani, kukabiliana na changamoto, kusaidia juhudi za mageuzi na kutafuta suluhisho la amani kwa mgogoro ulioko."

Washirika wa kimkakati

Nchi hizo mbili zimekuwa washirika wa karibu tangu kuvamiwa Iran na Iraq mwaka 1980, ambapo serikali ya Syria ilikaa upande wa Iran kwenye vita vilivyodumu miaka minane.

Rais Bashar Assad wa Syria.
Rais Bashar Assad wa Syria.Picha: picture alliance / AP Photo

Tangu kuibuka kwa wimbi la upinzani dhidi ya utawala wa Rais Bashar al-Assad hapo Machi 2011, Iran imeendelea kuwa mshirika wa karibu wa kiongozi huyo, ikimsaidia kuwashinda waasi. Umoja wa Mataifa unasema mgogoro wa Syria umeshapoteza maisha ya watu 100,000 kufikia sasa.

Halqi alimkabidhi Rowhani barua kutoka kwa Assad ambamo amesisitiza kuimarisha mahusiano ya kimkakati kati ya nchi hizo mbili, lilisema shirika la habari la Syria, SANA. Assad amesema serikali hizo mbili zina "dhamira ya kukabiliana na hujuma za Magharibi, Marekani na vibaraka wao kwenye eneo hilo, ambao wanapigania kuudhofisha mstatili wa mapambano."

Dhana ya "mstatili wa mapambano" inawakilisha umoja kati ya Syria, Iran na kundi la Hizbullah la Lebanon, ambalo wapiganaji wake wamejiingiza waziwazi kwenye mgogoro wa Syria tangu mwezi Aprili.

Upinzani wataka Umoja wa Mataifa kuchunguza mauaji ya maangamizi

Wakati huo huo, kundi kuu la upinzani nchini Syria, National Coalition, limeutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza "matukio mbalimbali ya mauaji ya maangamizi" wanayosema yamefanywa na vikosi vya Assad wakati wa mwezi wa Ramadhani.

Mpiganaji wa waasi akionesha moshi unaotoka kwenye jengo lililoshambuliwa Aleppo.
Mpiganaji wa waasi akionesha moshi unaotoka kwenye jengo lililoshambuliwa Aleppo.Picha: Edouard Elias/AFP/Getty Images

Kundi hilo, ambalo ni muungano wa makundi mbalimbali yanayopigana dhidi ya jeshi la Assad, limesema liko tayari kutoa mashirikiano kwa uchunguzi wowote huru juu ya uhalifu unaoshukiwa kufanywa na wapiganaji wa upinzani.

Wito huu unakuja siku mbili baada ya Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa, Navy Pillay, kusema kiwango kikubwa cha mauaji ya wanajeshi wa serikali waliochukuliwa mateka na waasi katika mji wa kaskazini wa Khan al-Assal kinachunguzwa.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Bruce Amani