1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saif al-Islam Gaddafi ahukumiwa kifo

Admin.WagnerD28 Julai 2015

Mahakama ya Libya leo (28.07.2015) imemhukumu Saif al-Islam Gaddafi na watu wengine wanane hukumu ya kifo kwa uhalifu wa kivita yakiwamo mauaji ya waandamanaji wakati wa mapinduzi ya mwaka 2011.

https://p.dw.com/p/1G6Z1
Saif al-Islam Gaddafi
Mwana wa kiume wa Gaddafi, Saif al-IslamPicha: Reuters/Stringer

Afisa mkuu wa uchunguzi katika ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu mjini Tripioli, Sadiq al-Sur, ameuambia mkutano na waandishi wa habari mjini Tripoli kwamba maafisa wa zamani wa utawala wa Gaddafi wamehukumiwa kufa kwa kupigwa risasi na kikosi maalumu. "Mahakama imewahukumu watetezi Said al Islam, mkuu wa zamani wa ujasusi, Abdullah al-Senussi, waziri mkuu wa zamani Baghdadi al-Mahmoudi, Mansour Dou, Abu Zeid al Dawradah, Milad Daman, Munther al-Ghunaimi, Abdel Hamid Uhaida na Uweidat Abu Soufa, kifo kwa kupigwa risasi."

Maafisa wanane wa zamani wa utawala wa Gaddafi walihukumiwa kifungo cha maisha jela na hukumu saba jela za miaka kumi na miwili kila mmoja. Wanne kati ya watuhumiwa 37 hawakupatikana na hatia na wengine wamepata vifungo vifupi gerezani.

Sadiq hakutaja mashitaka yaliyotumika kupitisha uamuzi huo. Washukiwa walikuwa wameshitakiwa kwa makosa mbalimbali yakiwamo matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanaji ambao hawakuwa na silaha, pamoja na rushwa.

Hukumu dhidi ya Saif al-Islam imepitishwa bila yeye kuwa mahakamani mjini Tripoli kwa kuwa amekuwa akizuiliwa na kundi la zamani la waasi tangu mwaka 2011 katika eneo la Zintan, ambalo haliko chini ya udhibiti wa serikali ya mjini Tripoli.

Hukumu yakosolewa

Washukiwa wana haki ya kukata rufaa dhidi ya hukumu hizo na zote sharti zithibitishwe na mahakama ya juu kabisa ya Libya. Hata hivyo wataalamu wa sheria na wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu wanasema mchakato mzima wa kusikilizwa kesi hizo ulivurugwa na kuingizwa siasa tangia mwanzo.

Abdullah Al-Senussi Libyen Geheimdienst 2011?
Abdullah al-Senussi na hayati Muammar GaddafiPicha: picture alliance/dpa

Wakati haya yakiarifiwa, Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya haki za binaadamu mjini Geneva, Uswisi, imesema imesikitishwa sana na hukumu ya kifo dhidi ya Saif al-Islam na maafisa wanane wa serikali ya kiongozi wa zamani wa Libya hayati Muammar Gaddafi.

Ofisi hiyo imesema katika taarifa yake na hapa tunanukuu, "Tulifuatilia kwa karibu kuzuiliwa kwake na kesi yake na kugundua kuwa viwango vya kimataifa vya kuhakikisha kesi ya haki havikuzingatiwa." mwisho wa kunukuu.

Ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa imesema mahakama ilishindwa kuweka jukumu binafsi la makosa ya jinai, hakukuwa na uwezekano wa washukiwa kuwa na mawakili, kulikuwa na madai ya washitakiwa kutendewa mambo mabaya na kesi ziliendeshwa bila washukiwa kuwepo mahakamani.

Mwandishi:Josephat Charo/rtre/dpa

Mhariri:Daniel Gakuba