1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Samaki hatarini kupotea

Lilian Mtono
10 Julai 2018

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeonya kuhusu hatari iiliyopo katika wakati ambapo theluthi ya bahari duniani ikikakabiliwa na athari za uvuvi uliopitiliza, huku mahitaji ya samaki yakisalia kuwa juu wakati wote.

https://p.dw.com/p/319mm
Weißer Hai
Picha: picture-alliance/WILDLIFE/M. Carwardine

MMT J3.10.07.2018-UN report on fishing - MP3-Stereo

Hatua hiyo inaibua wasiwasi kuhusu kuendelea kuwepo kwa samaki, ambao ni chanzo kikubwa cha protini kwa mamilioni ya binadamu duniani kote. 

Ripoti hiyo iliyochapishwa hapo jana na shirika na Umoja wa Mataifa linalishughulikia chakula, FAO imesema uvuvi huo uliopitiliza ni mbaya na hususan kwenye mataifa yanayoendelea, ambako idadi kubwa ya watu tayari wanapambana kuhakikisha wanapata chakula cha kutosha chenye virutubisho.

Mkurugenzi wa kitengo kinachojihusisha na uvuvi na ufugaji wa samaki kwenye shirika hilo, Manuel Barange alisema kuna shinikizo kubwa linalokabili rasilimali za bahari, na hivyo kuna haja kubwa pia kwa serikali kujitoa katika kuboresha mazingira ya uvuvi kwenye nchi zao.  

Ameuambia wakfu wa Reuters kwamba kuna wasiwasi katika siku za usoni, Afrika itaanza kuingiza samaki kutoka nje, na kuongeza kwamba upungufu wa samaki huenda ukapelekea bidhaa hiyo kupanda bei, na hivyo kuathiri zaidi watu masikini.

Senegal Dakar - Siumbediom Fischmarkt
Kuna wasiwasi kwamba afrika huenda ikaanza kuagiza samaki kutoka nje kutokana na kupungua kwa rasilimali hiyo.Picha: picture-alliance/AA/X. Olleros

Barange amesema, Afrika ilikuwa na uwezo mkubwa katika eneo la ufugaji wa samaki, lakini ilihitaji kusaidiwa kwa upande wa kifedha, malisho na usambazaji wa samaki hao.

Ripoti hiyo imesema sekta hiyo ya ufugaji wa samaki ambayo umeendelea kukua kwa haraka zaidi katika kipindi cha miaka 40, kwa kiasi kikubwa umewezesha upatikanaji zaidi wa samaki.

Katika wakati ambapo uvuvi baharini ukiendelea kupungua, mataifa mengi zaidi hivi sasa yanageukia sekta ya ufugaji wa samaki. Nchini Algeria, serikali imeendelea kuwahimiza wakulima kuzalisha samaki ili kuogeza kipato na kuimarisha uzalishaji jumla wa rasilimali hiyo.

Nordsee Fischfang
Samaki wanaweza kuongezeka ifikapo mwaka 2030 na kufikia tani milioni 201Picha: Reuters/D. Martinez

Hata hivyo wakosoaji wanasema, hatua hiyo inaweza kuchangia uharibifu wa mazingira, ingawa Barange anasema suluhisho la wasiwasi huo ni kuwa na kanuni muafaka, sheria na ufuatiliaji, lakini pia udhibiti kwenye shughuli za uvuvi.

Ripoti hiyo inaonyesha asilimia 33.1 ya samaki walivuliwa bila kuzingatia taratibu mnamo mwaka 2015, ikiwa imeongezeka kutoka asilimia 31.4 ya mwaka 2013, na asilimia 10 mwaka 1974. Ulaji wa samaki nao umeendelea kuwa juu kwa kilo 20.2 kwa mtu mmoja kutoka kilo 9 za mwaka 1961, lakini kukitarajiwa ongezeko zaidi, katika wakati ambapo wengi wanachagua kula samaki kutokana na matatizo ya kiafya.

Kiongozi wa programu za utafiti Shakuntala Thilsted, kutoka shirika la kimataifa lisilo la kibiashara la WorldFish, amesema kuna haja ya kutafutwa suluhu itakayowezesha kuitengeneza mifupa ya samaki pamoja na vichwa kuwa vyakula vyenye virutubisho, kwa kuwa sehemu hizo zina virutubisho vingi, badala ya kutegemea minofu ya samaki pekee.

Lakini, upande mwingine wa ripoti hiyo umesema, kunatarajiwa ongezeko la uzalishaji wa samaki kwa asilimia 18 ifikapo mwaka 2030 na kufikia tani milioni 201. Hata hivyo shirika hilo la FAO limetoa mwito kwa mamlaka husika kusimamia vyema  sekta ya uvuvi, ikiwa ni pamoja na kupunguza takataka na kukabiliana na uchafuzi wa bahari na mabadiliko ya hali ya hewa, ambavyo kwa pamoja huathiri bahari na uzalishaji wa samaki.

Mwandishi: Lilian Mtono/APE/RTRE.

Mhariri:Yusuf Saumu