1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sanaa yazizima baada ya mauaji makubwa

19 Septemba 2011

Hali ya wasiwasi imeongezeka katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa, hii leo (19.09.2011), siku moja baada ya waandamanaji 26 kuuawa kwa risasi na wengine 700 kujeruhiwa na vikosi vitiifu kwa Rais Ali Abdullah Saleh.

https://p.dw.com/p/12bqF
Mwandamanaji akikamata silaha kupambana na wanajeshi watiifu kwa Rais Saleh mjini Sanaa.
Mwandamanaji akikamata silaha kupambana na wanajeshi watiifu kwa Rais Saleh mjini Sanaa.Picha: picture alliance/dpa

Wapinzani wameyaita mashambulizi haya kuwa ni mauaji ya 26 ya kuangamiza kufanywa na utawala wa Rais Saleh tangu vuguvugu la upinzani dhidi ya kiongozi huyo kuanza mwishoni mwa mwezi wa Januari mwaka huu.

Kwa mujibu wa televisheni ya Al-Arabiya, hadi asubuhi ya leo mitaa ya mji mkuu wa Sanaa ilikuwa haina watu. Mashambulizi ya jana dhidi ya waandamanaji yameupoozesha mji huo, ambao umekuwa kitovu cha upinzani dhidi ya Rais Saleh.

Hata hivyo, naibu waziri wa habari wa Yemen, Abdul al-Janadi, amekanusha taarifa kuwa ni vikosi tiifu kwa Rais Saleh ndivyo vilivyofanya mashambulizi hayo, na badala yake amedai kuwa yalifanywa na "wahalifu wasiojuilikana".

"Mashambulizi haya yalitayarishwa ili kuuwa watu wengi kadiri ilivyowezekana. Ni njama dhidi ya Wayemeni wote." Amesema Abdul al-Janadi.

Rais Ali Abdullah Saleh alivyo sasa baada ya kushambuliwa hapo Juni 2011
Rais Ali Abdullah Saleh alivyo sasa baada ya kushambuliwa hapo Juni 2011Picha: dapd

Waandamanaji hawa waliuawa wakati wakiwa kwenye maandamano ya kumtaka Rais Saleh, anayetibiwa nchini Saudi Arabia, ajiuzulu na pia kutaka haki itendeke kwa waandamanaji wenzao waliouawa kwenye maandamano ya hapo kabla.

Usiku wa kuamkia leo, ulishuhudia kukatika ghafla kwa umeme kwenye mji mkuu Sanaa, huku waandamanaji wakidhibiti daraja muhimu mjini humo, kusimamisha safari za magari na kuanza kujenga mahema.

Maelfu ya waandamaji wengine wanaripotiwa kuyavamia majengo ya serikali, na kuyatia moto yale ambayo wanasema yanakaliwa na watunguaji na makundi yanayoiunga mkono serikali.

Daktari mmoja katika hospitali ya mjini Sanaa, Tarek Nooman, alikiambia kituo cha televisheni cha Al-Jazeera, kwamba ni wazi kuwa vikosi vilivyowashambulia waandamanaji vilitumia silaha za moto na vilikusudia hasa kuua. Hali katika hospitali za mjini Sanaa inatajwa kuwa ya kutisha.

"Washambuliaji walitumia silaha nzito, na hili linaweza kuonekana katika aina ya majeraha na matundu ambayo risasi zimetokea katika miili ya majeruhi na maiti. Tuna tatizo kubwa hivi sasa katika hospitali kuu na hospitali nyengine la upungufu wa vifaa na madawa." Amesema Dkt. Nooman.

Maandamano dhidi ya Rais Saleh mjini Sanaa
Maandamano dhidi ya Rais Saleh mjini SanaaPicha: DW

Licha ya mashambulizi haya, upinzani nchini Yemen umeapa kuendelea na maandamano hadi Rais Saleh na kile walichokiita "timu yake ya kisiasa" waondoke madarakani. Mwandamanaji mmoja mwanafunzi ameiambia Al-Jazeera kuwa "hakutakuwa na skuli wala masomo mpaka Rais Saleh aondoke.

Msemaji wa kile kinachojuilikana kama Jeshi la Mapinduzi la Yemen, Askar Zuail, kinachowajumuisha wanajeshi waliomuacha mkono Rais Saleh, amewataka Wayemeni kutokurudi nyuma.

"Ninawaomba Wayemeni wote, watu walio huru, kuja na kusimama nyuma ya vijana wetu kwa njia za amani hadi tufikie malengo yetu." Amesema Zuail katika taarifa yake aliyoisoma kwenye televisheni ya upinzani nchini humo.

Mashambulizi ya Jumapili ya jana ni miongoni mwa matukio mabaya sana dhidi ya waandamanaji na yamekuja katika wakati ambao kuna mkwamo wa kisiasa ndani ya nchi baina ya wapinzani na serikali.

Rais Saleh aliyeko nchini Saudi Arabia tangu mwanzoni mwa mwezi Juni, kutibiwa baada ya ikulu yake kushambuliwa, amekataa kuondoka madarakani, na badala yake amemuidhinisha makamu wake, Abd-Rabb Mansour Hadi, kutafuta muafaka wa kukabidhi madaraka.

Jambo hili, hata hivyo, linachukuliwa na wengi kwamba ni mbinu ya kurefusha muda tu.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Josephat Charo