1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Santorum aaga kinyang'anyiro

Abdu Said Mtullya11 Aprili 2012

Mjumbe wa chama cha Republican Rick Santorum aliekuwa anawania nafasi ya kuteuliwa ili kugombea urais wa Marekani mnamo mwezi wa Novemba amejitoa kwenye kinyang'anyiro hicho.

https://p.dw.com/p/14bRr
Rick Santorum
Rick SantorumPicha: AP

Rick Santorum aliyekuwa mshindani mkuu wa Mitt Romney ameamua kuisimamisha kampeni yake ya kuwania kuteuliwa na chama chake cha Republican ili kugombea Urais wa Marekani mnamo wa Novemba dhidi ya Rais Barack Obama.

Santorum aliwaambia waandishi wa habari mjini Gettysburg katika jimbo lake la uzawa la Pennyslvania kwamba kampeni ya kuwania uteuzi wa chama chake ili kugombea urais imefikia tamati kwake.

''Tulipitisha uamuzi wa kuingia katika kinyang'anyiro hiki tukiwa kwenye meza ya jikoni-katika muktadha wa vipingamizi vyote, na tuliamua mwishoni mwa wiki, kwamba wakati wa kinyang'anyiro hiki kwangu umefikia mwisho na kusimamisha kampeni, mapambano bado yanaendelea" Alisema Santorum.

Ushindi katika majimbo 10

Hapo mwanzoni Satorum aliwashangaza watu baada ya kushinda katika hatua ya kwanza ya uteuzi wa chama chake katika jimbo la Iowa mnamo mwezi wa Januari. Santoruma pia alishinda katika majimbo mengine 10 lakini alishindwa kuishikilia pinduli ili kuweza kumpita mshindani wake mkuu Mitt Romney ambae sasa anaongoza katika kampeni ya kuwania kuteuliwa na chama chake ili asimame dhidi ya Rais Obama mnamo mwezi wa Novemba.

Miongoni mwa wagombea 4 wa chama cha Republican, Rick Santorum ndie alikuwa mpinzani mkuu wa Mitt Romney.
Miongoni mwa wagombea 4 wa chama cha Republican, Rick Santorum ndie alikuwa mpinzani mkuu wa Mitt Romney.Picha: AP

Santoram aliewahi kuwa Seneta wa jimbo la Pennyslavia amesema licha ya kujiweka kando ya kampeni , ameahidi kufanya kila atakaloliweza ili kukiunga mkono chama chake cha Republican ili kukishinda chama cha Rais Obama cha Demokratik. Amesema ataendelea kupambana kwa niaba ya Wamarekani waliosimama wima na kumuunga mkono katika kampeni yake na kumwezesha kufikia hatua ambayo hata wataalamu wa masuala ya siasa hawakuweza kutabiri.

Katika hotuba yake ya kuisimaisha kampeni yake Santorum hakumtaja mpinzani wake mkuu Mitt Romney. Hata hivyo msemaji wa Santorum aliarifu kuwa wanasiasa hao walikutana na kufanya mazungumzo mazuri na kwamba watakutana tena hivi punde tu.

Mlango wazi sasa kwa Romney

Mitt Romney sasa ana nafasi kubwa ya kupambana na Rais Barack Obama katika uchaguzi wa Novemba.
Mitt Romney sasa ana nafasi kubwa ya kupambana na Rais Barack Obama katika uchaguzi wa Novemba.Picha: AP

Kamati ya kitaifa ya chama cha Republican imeusifu uamuzi wa Santorum wa kujiengua.

Mwanasiasa huyo ambaye ni muumini wa moyo wa kanisa katoliki anatetea sera za mrengo mkali wa kulia juu ya dini. Msimamo wake thabiti wa kupinga kutoa ujauzito na kupinga ndoa za mashoga uliitikiwa vizuri na wahafidhina. Lakini msimamo huo ulikuwa unawetenga wamarekani wenye siasa za ukadirifu.

Njia sasa ipo wazi kwa mshindani wake mkuu Mitt Romney ya kupata tikeki ya chama cha Republican ili kupambana na Obama katika uchaguzi wa rais mwezi wa Novemba. Lakini anahitaji kura 1144 za wajumbe ili kuweza kuipata tiketi hiyo kwenye mkutano mkuu utakaofanyika Tampa mwezi wa Agosti.

Mwandishi:Mtullya Abdu /AFPE

Mhariri: Gakuba Daniel