1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sarkozy na Ulaya

Maja Dreyer8 Mei 2007

Baada ya kuchaguliwa mhafidhina Nicolas Sarkozy kuwa ni rais mpya wa Ufaransa, wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamejihusisha na suali: uchaguzi huo utakuwa na matokeo gani ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/CHT1

Tukianza moja kwa moja na gazeti la “Mittelbayerische Zeitung”, mhariri anauliza:

“Kuchaguliwa Sarkozy kuna maana gani kwa Ujerumani na Ulaya kwa ujumla? Mhafidhina huyu alionyesha wazi kuwa yuko tayari kupigania maslahi ya kitaifa kwa nguvu kama simba. Lakini katika kampeni ya uchaguzi alishughulikia hasa sera za ndani. Hii ni kama ishara kwamba Sarkozy bado hana uhakika jukumu lake kwenye jukwaa la kimataifa ni lipi. Kuna matumaini kwamba atajipa moyo katika kazi hii yake. Tayari kwenye usiku wa uchaguzi aliarifu kuwa Ufaransa imerudi barani Ulaya.”

Zaidi juu ya uhusiano kati ya Ufaransa na Umoja wa Ulaya anachambua mhariri wa “Financial Times Deutschland”. Tunasoma:

“Kwa Umoja wa Ulaya sasa ni muhimu Ufaransa iwe tayari kuchukua hatua tena. Tangu Wafaransa kuikataa katiba ya Umoja huu katika kura ya maoni mwaka 2005 rais Jacques Chirac alipoteza nguvu zake kwenye uwanja wa Ulaya. Sasa kuna rais mpya nchini Ufaransa ambaye anaweza kujihisi kuwa na haki kamili ya kuwawakilisha Wafaransa kwa sababu hakujawahi kuwepo rais ambaye alipata idadi kubwa ya kura kama yeye. Wafaransa takriban Millioni 19 walimchagua Sarkozy kwenye uchaguzi wa Jumapili. Juu ya hayo, Sarkozy anasemekana kuwa na ushawishi mkubwa maoni yake yatekelezwe. Kwa hivyo, Ulaya inaweza kunufaika pale Sarkozy alipo na maslahi kuhusiana na Umoja wa Ulaya.”

Ni gazeti la “Financial Times Deutschland”. Kwa hivyo, matarajio juu ya sera za Sarkozy kuelekea nje ni mazuri. Kuhusiana na hali ya ndani ya Ufaransa, gazeti la “Tageszeitung” la mjini Berlin linataja wasiwasi:

“Vipi jamii ya Kifaransa ilivyogawika ilionekana wazi katika ghasia zilizotokea baada uchaguzi. Wakati wafuasi wa Sarkozy walisherehekea ushindi wa mtetezi wao, wapinzani wa Sarkozy walipigana na Polisi mabarabarani. Kisiasa ni vigumu kuchambua juu ya mapigano haya. Haiwezekani kusema ikiwa siku za usoni jamii itagawika zaidi kutokana na kuchaguliwa kwa Sarkozy. Lakini kwenye mitaa ya Paris, watu hawatafahamu vile Sarkozy alivyowaita vijana wahamiaji wahuni.”

Na sasa tuelekee kwenye suala lingine ambalo limegonga vichwa vya habari humu nchini Ujerumani tangu jana usiku, yaani tangu rais Horst Köhler alipoarifu kwamba hatampa msamaha gaidi wa zamani Christian Klar. Bw. Klar alikuwa mwanachama katika kundi la kigaidi la Ujerumani la RAF, ambalo katika miaka ya sabini lilirajibu kupambana na serikali ya Ujerumani. Klar alihukumiwa kwa kuhusishwa na mauaji. Huo hapa ni uchambuzi wa “Frankfurter Allgemeine Zeitung” juu ya kutopewa msamaha:

“Uamuzi wa rais Köhler hauathiri usalama wa sheria nchini humu, bali ni kinyume chake, unasaidia usalama wa kisheria. Pia unaenda sambamba na uzito wa uhalifu wa Bw. Klar. Hata baada ya kuzungumza naye binafsi, Klar hakumpa sababu rais asamehewe. Kisheria, tayari kuna njia kwa wafungwa wengi kusamehewa. Gaidi Klar, kwa mfano, ambaye alihukumiwa kufungwa gerezani maisha ataachiliwa kwa dhamana ikiwa mahakama husika itaamua kwamba Klar si hatari tena kwa jamii. Hivyo ndivyo taifa hili linavyowatendea wahalifu, hata wale waliojaribu kuiangamiza serikali yake.”

Na kwa maneno ya mhariri wa gazeti la “Frankfurter Allgemeine Zeitung” tunakamilisha udondozi wa magazeti ya Ujerumani ya hii leo.