1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sasa ni awamu ya mtoano kombe la dunia

Sekione Kitojo
30 Juni 2018

Kocha wa Ufaransa Didier Deschamps huenda akajaribu kutekeleza mkakati wa "no Messi, no Argentina" yaani bila Messi hakuna Argentina, wakati akijitayaisha na pambano la duru ya mtoano ya timu 16 katika awamu ya makundi.

https://p.dw.com/p/30ZyT
Russland WM 2018 Frankreich gegen Peru
Picha: imago/Lavandeira

Lakini  kocha  huyo  wa Ufaransa anapaswa  pia  kutafakari kupata kila  kitu  kutoka  kwa  wachezaji  wa  kikosi  chake.

Kuingia  kwa  Ufaransa  katika  awamu  hiyo  kutoka  katika awamu  ya makundi  bila  matatizo kwa  ushindi  mara  mbili  na  sare  moja kumekifanya  kikosi  hicho  kupigiwa  upatu  kuishinda  Argentina, ambayo  ilitandikwa na  Croatia na  ilihitaji  ushindi  wa  dakika  za mwisho dhidi  ya  Nigeria  kuweza  kukata  tikiti  yake kuingia  katika awamu  hii  ya  mtoano.

Russland WM 2018 Frankreich gegen Peru
Mshambuliaji wa Ufaransa Kylian MbappePicha: imago/Lavandeira

Pia  imejitutumua  tu katika  kundi  hilo  ambapo haikuonesha umahiri wake  katika awamu  hiyo  ya  makundi, ambapo kikosi  chake chenye  nyota wengi  vijana bado  hawajaonesha makucha  yao katika  medani  hii  kubwa  ya  dunia.

Messi, nafasi  yake  katika  kombe  la  dunia  na  Argentina kumtegemea  sana mshambuliaji  huyo  wa  Barcelona , hata  hivyo, kumetamalaki  katika  maelezo  kuelekea  pambano  hili  la Jumamosi , saa 10 jioni  saa  za  Ulaya  ya  kati, ikiwa  ni  saa 11 saa  za  Afrika  mashariki katika  Kazan Arena.

Katika  mkutano  wake  na  waandishi  habari , Deschamps aliulizwa mara  kadhaa vipi Ufaransa  itamzuwia  Messi, na  alijibu  taratibu  tu , hadi  pale  swali  la  nne  kama  hilo  lilisababisha kutoa  hisia  za kuchoshwa na  swali  hilo.

"Mchezaji  huyu ni  wa  hali  ya  juu  kabisa kwa  hiyo  tunapaswa kuchukua  tahadhari," nahodha  huyo  wa  zamani wa  timu  ya  taifa ya  Ufaransa  na  mshindi  wa  kombe  la  dunia  alisema.

Fußball WM 2018 Dänemark v Frankreich
Kocha wa Ufaransa Didier DeschampsPicha: Getty Images/AFP/F. Fife

Kumnyima  mipira  Messi  kwa  kudhibiti  sehemu  ya  kiungo kutaonekana  bila  shaka  ni  mwanzo kwa  Deschamps  kuchukua tahadhari.

Kumfunika  Messi

Croatia  ilifanikiwa  kumfunika Messi kwa  kuwa  na Ivan Strinic  na Marcelo Brozovica kukaa  nyuma  ya  wachezaji  wa  kati  kina  Luka Modric  na  Ivan Rakitic,  na  kusaidiana kwa kubadilishana  katika kukimbia  pamoja  na  mshambuliaji  huyo  hatari wa  Arngentina.

N'Golo Kante  na  Blaise Matuidi huenda  wakalazimika  kufanya  kazi hiyo, na  Deschamps anaweza  kuamua  kurejea  katika  mfumo  wa msingi  wa  4-2-3-1 ambapo Matuidi atakuwa  anashika  nafasi  ya mshambuliaji  wa  pembeni  upande  wa  kushoto badala  ya nafasi ya  kushambulia  zaidi kama  vile  anavyocheza  mchezaji  mwenzake Messi  Osmane  Dembele  katika Barcelona.

Fußball WM 2018 Dänemark v Frankreich
Mshambuliaji wa Ufaransa Osmane DembelePicha: Getty Images/D. Mullan

Kuweka msisitizo  zaidi  kwa  Messi , hata  hivyo, kunaweza kusababisha  hali  ngumu  kwa  ushambuliaji  wa  Ufaransa ambao umeonekana  kuwa  mkusanyiko  wa vifaa  ghali ambavyo  bado havijaweza  kuwa kitu  kimoja.

Deschamps alipoteza  fursa  kwa  vijana  wake  hao  kung'aa kwa kubadilisha  kikosi  chake  kilichotoka  sare  bila  kufungana  na Denmark, ambayo  ilikata tikiti  yake  ya awamu  ya  mtoano  lakini haijafanya  pakubwa  kuleta mchezo  wa  uelewano  katika  timu.

Mabadiliko  mengine  yanaonekana  kuja katika  mchezo  dhidi  ya Argentina, ambapo Deschamps huenda  akamwacha  nje  mchezaji chipukizi  Kylian Mbappe  katika  benchi tena  ama  kumpumzisha Pogba.

Katika  mchezo  mwengine  jioni Cristiano Ronaldo, Luis Suarez  na Edinson Cavani , Ureno  na Uruguay zinajivunia  baadhi  ya wafungaji  bora  kabisa  katika  soka  la  dunia  kwa  sasa, lakini Sochi  kunaweza  kuwa  eneo  ambalo  mpambano  wa  kombe  la dunia  unaweza  kuleta  mvuto  mkubwa  leo  Jumamosi.

Russland WM 2018 l Iran vs Portugal  1:1 - Ronaldos Reaktion zum Spielende
Mshambuliaji wa Ureno Cristiano RonaldoPicha: Reuters/L. Nicholson

Timu  hizo zinapambana  katika  pambano  la  pili  saa  mbili  usiku kwa  saa  za  Ulaya  ya  kati  na  saa  3  usiku  kwa  saa  za  Afrika mashariki.

Nchi  hizi  mbili  ndogo  zikiwa  na  utamaduni  wa  kusifika  wa kandanda  zinapambana  katika  pwani  ya  bahari  nyeusi  nchini Urusi  zikiwania  nafasi  katika  robo  fainali  ya  kombe  la  dunia mwaka  huu 2018.

Kwa Ronaldo  ni  kwamba  anarejea  katika  uwanja  ule  ule  ambako alipachika  mabao  matatu  dhidi  ya  Uhispania  mapema  katika mashindano  haya, lakini mara  hii atapambana na ngome  ya Uruguay  ambayo  ni  pekee  miongoni  mwa  timu  32 zilizofika  Urusi na kuingia  katika  duru  ya  mtoano  bila  kufungwa  bao.

Hilo na rekodi  ya  hivi  karibuni  ya  Ureno  iliyohusika  katika michezo  migumu  katika awamu za  mtoano  na kufikia hadi  dakika za  mwisho, kumeleta  uwezekano  wa  mpambano wa  kukata  na shoka  wakati  kombe  la  dunia  linaelekea  katika  awamu za mwisho.

Mwandishi: Sekione  Kitojo / afpe/ rtre

Mhariri: Sylvia  Mwehozi