1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudia kutoa ushahidi wa mashambulizi ya vituo vya mafuta

Admin.WagnerD18 Septemba 2019

Saudi Arabia imesema itatoa ushahidi leo Jumatano (18.09.2019) unaoihushisha Iran na mashambulizi katika vituo vyake viwili muhimu vya uzalishaji mafuta, tukio ambalo Marekani inaamini lilipangwa nchini Iran.

https://p.dw.com/p/3PmBu
Saudi-Arabien Drohnenangriffe
Picha: Reuters

Wizara ya ulinzi ya Saudi Arabia imesema itakuwa na mkutano na waandishi habari baadaye leo mchana kuwasilisha inachokiita ''ushahidi wa wazi'' pamoja na silaha za Iran ili kuthibitisha kuhusika kwa  utawala wa Iran kwenye mashambulizi hayo.

Serikali mjini Riyadh imekwishasema tangu mwanzo kuwa matokeo ya uchunguzi wa awali yanaonesha mashambulizi hayo hayakutokea nchini Yemen, kama ilivyodaiwa na waasi wa Kihouthi.

Afisa mmoja wa Marekani ameliambia shirika la Habari la Reuters kuwa mashambulizi kwenye miundombinu hiyo ya mafuta yalitokea kusini magharibi ya Iran.

Maafisa wengine watatu wamesema mashambulzii hayo yalihusisha makombora na ndege zisizo na rubani, taarifa zinazoashiria kuwa yalipangwa kwa ustadi wa hali ya juu tofauti na ilivyodhaniwa hapo kabla. 

Hata hivyo maafisa hao hawakutoa ushahidi wowote au kueleza ni taarifa zipi walizotumia kufikia hitimisho hilo.

Iran yasisitiza haihusiki 

Iran kwa upande wake imekana kuhusika na mashambulizi hayo ya Septemba 14 yaliyokilenga pamoja na eneo jingine, kiwanda kikubwa kabisa duniani cha kusafishia mafuta hali iliyotikisa kwa muda mfupi karibu nusu ya uzalishaji mafuta nchini Saudia Arabia.

Kundi la waasi wa Houthi nchini Yemen ambalo ni mshirika na Iran limedai kuhusika na mashambulzii hayo likisema lilitumia ndege zisizo na rubani kuihujumu miundombinu ya kampuni ya mafuta ya taifa nchini Saudi Arabia, Aramco.

Saudi-Arabien -  Prinz Abdulaziz bin Salman
Waziri wa Nishati wa Saudi Arabia, Abdulaziz bin SalmanPicha: Getty Images/AFP

Katika hatua nyingine Saudi Arabia imesema uzalishaji wa mafuta utarejea kikamilifu mwishoni mwa mwezi Septemba na Oktoba na kufikia kiwango sawa na kile cha kabla ya mashambulizi ya Jumamosi iliyopita.

Akitoa tangazo hilo jana Jumanne waziri wa nishati wa Saudi Arabia Mwanamfalme  Abdulaziz bin Salman amesema "usambazaji mafuta utarejea katika hali ya kawaida katika masoko yetu  kama ilivyokuwa kabla ya saa 3:43 asubuhi siku ya Jumamosi"

Pompeo aelekea Saudi Arabia

Mike Pompeo auf dem Weg nach Thailand
Picha: Getty Images/AFP/J. Ernst

Wakati huo huo, waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Mike Pompeo na maafisa wengine wa Marekani wanakwenda Saudi Arabia leo ili kujadiliana na wenzao mjini Riyadh kuhusiana na mashambulizi hayo.

Kadhalika wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanaofutuatilia vikwazo dhidi ya Iran na Yemen pia wanaelekea Saudia kwa mikutano na viongozi wa falme hiyo.

Iwapo ushahidi usio na shaka utatolewa na kuihusisha Iran na mashambulizi hayo utaweka uwezekano mkubwa wa Marekani na Saudi Arabia kuchukua hatua dhidi ya Iran ingawa rais Donald Trump amesema mara kadhaa kuwa hataka hana mipango ya kuanzisha vita kwenye kanda hiyo.