1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Saudia yawatimua wanadiplomasia wa Iran

4 Januari 2016

Saudi Arabia imevunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran, baada ya waandamanaji kuuvamia ubalozi wake mjini Tehran na kuuchoma moto, na kutoa saa 48 kwa wanadiplomasia wa Iran kuondoa nchini humo.

https://p.dw.com/p/1HXXB
Mfalme wa Saudi Salma bin Abdul-Aziz al-Saud.
Mfalme wa Saudi Salma bin Abdul-Aziz al-Saud.Picha: picture-alliance/dpa/Saudi Press Agency

Hatua ya Saudi Arabia ilikuja saa chache baada ya waandamanaji kuuvamia na kuuchoma moto ubalozi wake mjini Tehran, katika kupinga mauaji ya kiongozi wa Kishia Sheikh Nimr al-Nimr.

Mauaji ya Nimr pamoja na wengine 46 - ambayo ndiyo makubwa zaidi kufanywa kwa wakati mmoja katika kipindi cha miongo mitatu na nusu - yamebainisha wazi migawanyiko mikubwa inayoikabili kanda ya Mashariki ya Kati, ambako waandamanaji waliingia mitaani kuanzia Bahrain hadi Pakistan kuyapinga.

Al-Nimr alikuwa mtu muhimu katika maandamano ya Washia wachache wa Saudi Arabia, yaliyohamasishwa na uasi wa umma katika mataifa kadhaa ya Kiarabu, hadi alipokamatwa mwaka 2012.

Alitiwa hatiani kwa makosa ya ugaidi, lakini alikanusha kuchochea vurugu. Kiongozi wa juu kabisa nchini Iran, Ayatollah Ali Khomenei, alisema Saudi Arabia italipa gharama kubwa kwa mauaji ya Nimr.

Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir.
Waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir.Picha: picture-alliance/dpa/C. Dharapak

Aituhumu Tehran kwa kuendeleza sera za kibabe

Waziri al-Jubeir alisema mashambulizi dhidi ya balozi zake nchini Iran ni mwendelezo wa sera za kibabe za utawala wa Tehran katika kanda hiyo, zinazolenga kuvuruga usalama na kueneza ugomvi na vita, ambavyo amesema vinathibitishwa na hatua ya Iran kuwapa hifadhi viongozi wa Al-Qaeda tangu mwaka 2011, na pia kuwapatia ulinzi baadhi ya walioshiriki katika uripuaji wa majengo ya al-Khobar mwaka 1996.

"Kwa kuzingatia ukweli huu, Saudi Arabia inatangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran, na inaomba kwamba wanadiplomasia wote walioko ubalozini, ubalozi mdogo na ofisi tanzu zote kuondoka katika muda wa saa 48," alisema Al-Jubeir.

Iran ilisema iliwakamata watu 44 kuhusiana na mashambulizi ya ubalozi, na rais Hassan Rouhani akawaelezea waandamanaji hao kuwa wenye itikadi kali, na kwamba mashambulizi dhidi ya balozi za Saudi hayakuwa na uhalali wowote.

Visasi vyaanza

Nchini Iraq, misikiti miwili ya Kisunni imeripotiwa kushambuliwa kwa mabomu katika mkoa wa katikati mwa nchi hiyo wa Hilla, huku muadhini akiuawa kwa kupigwa risasi karibu na nyumbani kwake mjini Iskandariya, kulingana na maafisa wa polisi na wahudumu wa afya.

Katika mkoa huo wa Hilla, uliyoko umbali wa kilomita 80 kusini mwa mji mkuu Baghdad, Afisa wa polisi alisema msikiti wa Ammar bin Yasser uliyoko katika kijiji cha Bakerli uliripuriwa kwa mabomu usiku wa manane.

Ubalozi wa Saudi mjini Tehran ukiwaka moto baada ya kushambuliwa na magenge ya waandamanaji.
Ubalozi wa Saudi mjini Tehran ukiwaka moto baada ya kushambuliwa na magenge ya waandamanaji.Picha: Isna

"Baada ya kusikia mripuko, tulienda mahala ulipotokea na kukuta vifa vya miripuko vya kutengeneza kienyeji vikiwa vimewekwa katika msikiti, alisema kapteni huyo wa polisi. "Wakazi walisema watu waliovalia sare za jeshi walifanya operesheni hiyo," alisema na kuongeza kuwa nyumba 10 ziliharibiwa katika mripuko huo.

'Saudi yafunika makosa yake'

Naibu waziri wa mambo ya nje Hossein Amir Abdollahian alinukuliwa akisema uamuzi wa Saudi kuvunja uhusiano na Iran hauwezi kuifanya dunia isahau kosa lake kubwa la kumuua Nimr.

"Kwa kuamua kuvunja uhusiano wa kidiplomasia, Saudi Arabia haiwezi kuifanya dunia isahau kosa lake kubwa la kumuuwa," alisema naibu waziri huyo akinukuliwa na shirika la habari la Iran IRNA.

Aliongeza kuwa Saudi Arabia ilifanya kosa la kimkakati kwa kuchukuwa maamuzi ya haraka, ambayo yameeneza ukosefu wa utulivu na kusababisha kukuwa kwa ugaidi katika kanda.

Naye msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Hossein Jaberi Ansari, alisema katika matamshi yaliyotangazwa kwenye televisheni, kuwa Iran inayo dhamira ya kuzilinda balozi zote za kigeni chini ya mikataba ya kimataifa. Lakini ailiongeza kuwa Saudi Arabia imetumia tukio hilo kama kisingizio cha kuchochea mgogoro.

Washia wa Saudi wakiandamana kupinga mauaji ya kiongozi wao Sheikh Nimr al-Nimr.
Washia wa Saudi wakiandamana kupinga mauaji ya kiongozi wao Sheikh Nimr al-Nimr.Picha: Getty Images/AFP/Str

Uhusiano wa mivutuno

Uhusiano kati ya Saudi Arabia na Iran umekuwa wa mivutano kwa miongozo kadhaa, huku Riadh ikiishtumu Tehran mara kwa mara kwa kuingilia masuala ya mataifa ya Kiarabu.

Mataifa hayo mawili pia yamegawanyika juu ya vita vya karibu miaka mitano nchini Syria, ambako Iran inaunga mkono utawala wa Bashar Al-Assad, na katika mgogoro wa Yemen ambako muungano unaongozwa na Saudi Arabia unapambana dhidi ya waasi wa Kishia.

Abdollahian ameituhumu pia Saudi Arabia kwa kile alichokiita "kupuuza maslahi ya watu wake na Wasilamu wa kanda hiyo kwa njama yake ya kushusha bei za mafuta," akimaanisha bei za mafuta ghafi ambazo ziko karibu kufikia kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudia katika kipindi cha miaka kadhaa.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre
Mhariri: Daniel Gakuba