1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Schalke yamaliza msimu katika nafasi ya pili

Bruce Amani
7 Mei 2018

Wolfsburg na Hamburg kusubiri hadi siku ya mwisho ili kuona nani atashushwa daraja, Schalke yamaliza msimu katika nafasi ya pili kwa mara ya kwanza baada ya misimu minane

https://p.dw.com/p/2xK2P
Fußball Bundesliga Jubel Schlke 04
Picha: Imago/Eibner

Schalke watarejea msimu ujao katika kundi la wanaume, ligi ya mabingwa Ulaya, kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2014-15. Hii ni baada ya kuwachapa Augsburg kwa urahisi mabao mawili kwa moja na kuikamata kabisa nafasi ya pili. Msimu huo pia ndio ulikuwa wa mwisho kumaliza mbele ya watani wao wakali Borussia Dortmund, ijapokuwa msimu huo, Schalke walimaliza katika nafasi ya sita na Dortmund ya saba. Kocha wa Schalke Domenico Tedesco alikuwa mwenye furaha baada ya mechi "Nna furaha kubwa sana kuhusu namna timu ilivyouangalia mchezo wote wa leo. Ilicheza kwa kujituma na moyo wote, shauku na hivyo nna fuiraha kubwa".

Deutschland Eintracht Frankfurt - Hamburger SV | enttäuschte Spieler
Hatima ya Hamburg ipo mikononi mwaoPicha: picture-alliance/dpa/A. Dedert

Lakini nyuma ya Schalke kuna vita vikali vya kuwania nafasi mbili zilizobaki za Champions League. Timu zilizokuwa katika nafasi za tatu, nne na tano yaani Borussia Dortmund, Hoffenheim na Bayer Leverkusen zilishindwa kupata ushindi ambapo ni Leverksuen pekee ilipata pointi moja

Hii ina maana timu zozote mbili kati ya hizo tatu pamoja na Eintracht Frankfurt na RB Leipzig huenda zikapata tikiti. Leipzig iliichabanga Wolfsburg mabao manne kwa moja. Maximilian Arnold ni mchezaji wa Wolfsburg "Bado tu suala ni kubaki katika ligi kuu. Haijalishi ni vipi, haijalishi ni mbinu zipi zitakazotumika. Hatuwezi kuviweka vichwa vywetu mchangani. Bado tu tuko pale pale.  Lazima tu tuwe kama kitu kimoja na kushirikiana katika hali hii na kisha tutafaulu".

Mchuano wa ugenini kati ya Borussia Dortmund na Hoffenheim Jumamosi ijayo utakuwa wa kukata na shoka. Hoffenheim walizabwa mabao mawili kwa sifuri na Stuttgart. Msikilize mshambuliaji wa Stuttgart, Mario Goetze "Katika Mzunguko huu wa pili mzuri kabisa, watu wametuonyesha katika uwanja wa nyumbani, katika mechi za ugenini, idadi kubwa ya watu wamenipa mapokezi mazuri dhidi ya Hertha, hicho ni kitu ambacho sitawahi kusahau. Umri wangu umesonga na sipendi kuzisikia habari hizi tena. Inafurahisha kuwa tulicheza vizuri sana katika mzunguko wa pili. Na ndio maana nna furaha kuwa nimeweka kuonyesha kitu kizuri katika uwanja huu".

Fußball Bundesliga VfL Wolfsburg RB Leipzig
Leipzig wanatafuta nafasi ya kucheza UlayaPicha: picture alliance/AP Photo/J. Meyer

Katika upande wa mkia, waliohitaji sana kupata pointi walishindwa kuzipata isipokuwa tu ushindi wa kushangaza wa Mainz dhidi ya Dortmund. Ni ushindi uliohakikisha kuwa watacheza katika Bundesliga msimu ujao.

Katika siku ya mwisho ya msimu, timu moja kati ya Hamburg, Wolfsburg na Freiburg itajiunga na Cologne katika ligi ya daraja la pili, nyingine itakuwa katika nafasi ya mechi ya mchujo na moja itaponea shoka la kushushwa ngazi.

Wolfsburg itaialika Cologne, Freiburg itaikaribisha Augsburg wakati Hamburg itakuwa nyumbani kupambana na Borussia Moenchengladbach. Kocha wa Hamburg Christian Titz hajakata tamaa baada ya kuzabwa tatu bila na Eintracgt Frankfurt "Bado tuna nafasi ukipiga hesabu. Na katika kandanda lolote lawezekana. Tukishinda nyumbani na kisha tunashindwa dhidi ya Wolfsburg, hali inageuka kwa ghafla. Hatutaweka vichwa vyetu kwenye mchanga. Tumesikitika na tutasuluhisha hilo na kujiandaa vilivyo kwa mchuano dhidi ya Gladbach na kwanza kabisa tutaona kama tutaweza kujikusanyia pointi tatu"

1. Bundesliga 30. Spieltag | FC Schalke 04 - Borussia Dortmund | Peter Stöger
Stöger atabaki Dortmund au ataondoka?Picha: picture-alliance/dpa/I. Fassbender

Wakati Hamburg wakijizatiti kutoshuka daraja, Nürnberg, timu iliyoshushwa daraja mara nyingi Zaidi na kupandishwa daraja Zaidi katika historia ya Bundesliga, itakaribishwa tena msimu ujao baada ya kupandishwa ngazi. Ushindi wao wa mbili sifuri dhidi ya Sandhausen uliipandisha timu hiyo ya Bavaria huku kukiwa na mechi moja iliyosalia msimu huu.

Katika habari nyingine za kandanda la Ujerumani ni kuwa Borussia Dortmund wanaendelea kutafakari kama watabaki na kocha wao Peter Stoeger au watamwajiri kocha mpya. Klabu hiyo mpaka sasa haisemi lolote kuhusu hilo. Lakini kiungo Sebastian Rode amesema wachezaji wa timu hiyo wanatarajia kikamilifu kuwa na kocha mpya msimu ujao. Rode amesema jinsi ambavyo Stoeger anavyojionyesha mbele yao ina maana kuwa wanatarajia kuwa na kocha mpya msimu ujao. Stoeger alichukua usukani katika klabu ya Dortmund kwa mkataba mfupi wakati klabu hiyo ilimtimua Mholanzi Peter Bosz mwezi Desemba.

Mwenyekiti wa BVB Hans-Joachim Watzke amekasirishwa na kauli za Rode, akisema kuwa kiungo huyo ataadhibiwa vikali kwa kuifanya hali ya Stoeger kuwa ngumu zaidi.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman