1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Seleka: Bozize apelekwe ICC

10 Januari 2013

Mzungumzo baina ya Waasi wa Seleka na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati yameanza vibaya hapo jana baada ya waasi kukataa kwenda kwenye meza ya majadiliano.

https://p.dw.com/p/17Gw3
The Central African Republic's President Francois Bozize looks on as he gives a press conference, on January 8, 2013 at the presidential palace in Bangui. Bozize refused on January 8 to discuss resigning at upcoming peace talks with rebels who have stormed across the country and seized several key towns. AFP PHOTO/ SIA KAMBOU (Photo credit should read SIA KAMBOU/AFP/Getty Images)
Francois BozizePicha: AFP/Getty Images

Waasi hawakutokea mezani baada ya kauli ya Rais Francois Bozize kwamba wao ni wavamizi kutoka mataifa ya kigeni.

Kitendo cha waasi kutokuonekana kwenye meza ya mazungumzo kiliwalazimu wapatanishi kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika ya Kati, ECCAS, kufanya mazungumzo kwa makundi makundi yaani serikali peke yake, waasi, vyama vya upinzani na mashirika ya kiraia.

Waasi walichukizwa na kauli ya Rais Francois Bozize iliyowatuhumu kuwa wao ni wavamizi wa kigeni wanaofadhiliwa na watu kutoka nje ya nchi na hivyo hawezi kuachia madarakani kwa sababu ya matakwa yao.

Waasi wa Seleka katika Jamhuri ya Afrika ya Kati
Waasi wa Seleka katika Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: SIA KAMBOU/AFP/Getty Images

Kauli ya Bozize

Bozize alisema "suala la mimi kuachia ngazi halipo kabisa. Nilichaguliwa mara mbili na kuwa kiongozi wa taifa kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura. Niko hapa na huo ndio mwisho, hakuna kingine kitafanyika" .

Kiongozi huyo alisema kuwa wana taarifa kwamba baadhi ya waasi hao ni wapiganaji wa Janjaweed kutoka Sudan.

Bozize alitoa kauli hiyo baada ya Seleka kusambaza nyaraka katika eneo la mkutano zinazotaka apelekwe kwenye Mahakama ya Kimataifa Uhalifu, ICC, kutokana na makosa ya kivita na uhalifu dhidi ya binaadamu ikiwa ni pamoja na kuwafunga watu kimakosa, kuwateka nyara, mauwaji na adhabu za kifo alizitoa kwa watu wasio na hatia.

Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati
Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya KatiPicha: AP

Wito wa wapatanishi

Kufuatia vijembe hivyo wapatanishi wamezitaka pande zinazopingana kulegeza misimamo na kusaini makubaliano ya amani katika siku za mwanzo za mazungumzo. Hata hivyo hakukuwa na dalili yoyote ya kuitikiwa kwa wito huo kutokana na kiwango cha utayarifu wa kufanya hivyo baina ya wahusika kuwa kidogo.

Hii leo kunafanyika mkutano wa wakuu wa nchi za eneo la Afrika ya Kati ambapo Rais Bozize anatarajiwa kushiriki.

Mwenyekiti wa mazungumzo hayo Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kongo bwana Basile Ikouebe aliwataka wafuasi wa Bozize kufuata sheria za Umoja wa Afrika za mabadiliko ya utawala wakati kikao kinaanza.

The commander of the regional African force FOMAC Jean-Felix Akaga reviews troops, on January 2, 2013 in Bangui after a press conference during which he warned rebels from the SELEKA coalition in the Central African Vikosi cha kulinda amani vya Afrika ya Kati FOMAC mjini Bangui
Vikosi cha kulinda amani vya Afrika ya Kati FOMAC mjini BanguiPicha: SIA KAMBOU/AFP/Getty Images

Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa eneo la Afrika ya Kati walisema hapo kabla kwamba wanasikitika kuona pande zote kwenye mazungumzo hayo zinaendelea kutupiana maneno na kuonya kuwa zoezi la upatanishi litakuwa gumu kadri muda unavyokwenda.

Jana Jumatano, Mkuu wa kikosi cha kijeshi cha Chad kinacholinda amani Jamhuri ya Afrika ya Kati alisema kuwa amekutana na waasi umbali wa kilometa 10 kaskazini mwa mji wa Damara ambao ni wa mwisho kabla ya kuingia mji mkuu wa Bangui na akawaamuru watawanyike.

Mazungumzo ya sasa yanaangalia upya makubaliano ya amani yaliyofikiwa mwaka 2007 ambayo waasi wa Seleka wamekuwa wakimutuhumu Bozize kuyakiuka.

Mwandishi: Stumai George/ Dpa/Afp/Reuters

Mhariri: Daniel Gakuba