1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sera ya kigeni kutobadilika nchini Ufaransa.

Mohamed Dahman4 Mei 2007

Wagombea wawili wa marudio ya uchaguzi wa rais wa Ufaransa unaofanyika hapo kesho wamepachikana majina ya kijibwa cha Marekani na mpumbavu wa kidiplomasia lakini wote wawili Nicolas Sarkozy na Segolene Royal watakuwa na sera za kigeni za aina moja wakati watakapokuwa madarakani.

https://p.dw.com/p/CHEr
Wagombea urais nchini Ufaransa Nicolas Sarkozy na Segolene Royal.
Wagombea urais nchini Ufaransa Nicolas Sarkozy na Segolene Royal.Picha: AP Graphics/DW

Royal ambaye ni mjamaa anataka mataifa makubwa duniani kuwa wakali zaidi na Iran juu ya mpango wake wa nuklea.Wakati muhafidhina Nicolas Sarkozy anataka kuimarisha zaidi uhusiano na serikali ya Marekani.Wote wawili wanasema watakuwa wakali kwa nchi zenye kukiuka haki za binaadamu.

Lakini ukiachana na majigambo hayo wachambuzi wa mambo wanasema mshindi wa marudio hayo ya uchaguzi wa urais nchini Ufaransa hapo kesho yumkini hatoacha njia na kuwa mbali sana na pale alipoacha Rais anayeachilia ngazi Jaques Chirac.

Thierry de Montbrial mkuu wa jopo la ushauri la Taasisi ya Uhusiano wa Kimataifa anafikiri nafasi ya kufanya hila ni finyu.

Royal na Sarkozy wamesema kwamba wanakusudia kuendelea na sehemu kubwa ya sera mashuhuri ya mambo ya nje ya Chirac hususan kwa Mashariki ya Kati na wataisuka kivyake.

Royal amerudia kusema mara kadhaa kwamba Iran inapaswa kuzuiliwa kuwa na teknolojia ya nuklea kwa matumizi ya kiraia kutokana na hofu kwamba nchi hiyo inatengeneza kwa siri silaha za nuklea dai ambalo serikali ya Iran inalikanusha.

Msimamo wake huo unapindukia ule wa pamoja wa Ufaransa, Marekani,Ujerumani,Uingereza,China na Urusi ambao wanajaribu kuishawishi Iran kuachana na tekenolojia nyeti ambazo zinaweza kuzalisha umeme na pia kutengeneza silaha ili badala yake waipatie nchi hiyo marupurupu ya kiuchumi.

Kampeni ya Royal ilianza kwa makosa kadhaa ya kidiplomasia yenye kukirihisha.Alikemewa na umma kutoka Canada baada ya kuelezea kupendelea wazo la uhuru kwa jimbo lake la Quebec linalozungumza Kifaransa na mjini Beirut aliposema anakubaliana na mbunge wa kundi la Hizbollah juu ya uwenda hoka wa sera ya kigeni ya Marekani ikiwa ni muda mfupi kabla ya kuelekea nchini Israel mshirika wa Marekani.

Royal alisahihisha kauli yake hiyo ya Beirut muda mfupi baadae lakini wapinzani wake wanaendelea kuitumia dhidi yake.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa Sarkozy na kushangiliwa na umma wa watu waziri wa ulinzi Michele Alliot- Marie amesema hawahitaji mtu mwenye kubadili mawazo kila mara kama vile anavyobadili skati yake.

Sarkozy amekuja kushutumiwa kutokana na kujipendekeza kwa Marekani hususan kwa safari yake nchini humo ambapo alikutana kwa muda mfupi na Rais George W. Bush na kushutumu jinsi Ufaransa ilivyopinga uvamizi ulioongozwa na Marekani nchini Iraq hapo mwaka 2003.

Royal ameiambia televisheni ya Ufaransa kwamba katu hatomuomba radhi Rais Bush kutokana na msimamo wa Ufaransa wa kupinga kutuma vikosi vyake nchini Iraq.Jambo hilo limepelekea kambi ya Sarkozy kusisitiza kwamba kiongozi wao huyo hakuomba radhi kwa Marekani.

Wachambuzi wa mambo wanasema gumzo kwamba Sarkozy anaipendelea Marekani ambalo ni tusi katika nchi ambapo chuki ya Marekani imejikita ni kuongezea chumvi.

Katika mdahalo mkali wa televisheni Sarkozy amesema iwapo atachaguliwa atakuwa rais aliejifunga katika kuleta matokeo na Royal amesema Ufaransa inahitaji viongozi wanaowajibika kwa matendo yao.

Yoyote atakayeshinda uchaguzi huo wa kesho Chirac atakuwa amewazidi kete moja ya kumudu kimombo lugha ya Kingereza alioifuma wakati akiwa mwanafunzi nchini Marekani.