1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali mpya yaanza kujulikana

15 Desemba 2013

Chama cha upinzani cha SPD (Jumapili 15.12.2013) kimeanza kutangaza mawaziri wake watakaokuwemo katika serikali ya mseto nchini Ujerumani miezi mitatu baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/1AZwP
Mwenyekiti wa chama cha SPD Gabriel Sigmar akiwatambulisha mawaziri wa chama chake mjini Berlin. (15.12.2013)
Mwenyekiti wa chama cha SPD Gabriel Sigmar akiwatambulisha mawaziri wa chama chake mjini Berlin. (15.12.2013)Picha: Reuters

Chama cha upinzani cha SPD (Jumapili 15.12.2013) kimeanza kutangaza mawaziri wake watakaokuwemo katika serikali ya mseto nchini Ujerumani miezi mitatu baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.

Sigmar Gabriel kiongozi wa chama cha Social Demokratik amewaambia waandishi wa habari kwamba atakuwa naibu kansela na kuongoza kile kinachojulikana kama "wizara kuu" itakayojumuisha wizara ya uchumi na nishati. Frank Walter Steinmeier anarudia katika wadhifa wake wa waziri wa mambo ya nje ambao aliwahi kuushikilia kuanzia mwaka 2005-2009 chini ya uongozi wa Kansela Angela Merkel.

Chama hicho cha SPD kimetimiza ahadi yake kuzijaza nusu ya nafasi za mawaziri walizotengewa kwa kuwapa wanawake.

Katibu Mkuu wa chama hicho Andrea Nahles atakuwa waziri wa kazi wakati makamo mwenyekiti wa chama hicho Manuela Schwesig anashika wadhifa wa waziri wa masuala ya familia na mweka hazina wa chama hicho Barbara Hendricks kuiongoza wizara ya mazingira.

Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel na Katibu Mkuu wa chama hicho Andrea Nahles mjini Berlin.(15.12.2013).
Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel na Katibu Mkuu wa chama hicho Andrea Nahles mjini Berlin.(15.12.2013).Picha: picture-alliance/dpa

Viongozi wengine wa chama hicho waliochaguliwa kushika nyadhifa kwenye baraza la mawaziri ni Heiko Maas waziri wa uchumi wa jimbo la magharibi la Saarland ambaye ataongoza wizara ya sheria na masuala ya walaji naye naibu kiongozi mwengine wa SPD Aydan Özoguz atakuwa waziri wa nchi wa masuala ya uhamiaji, wakimbizi na kujumuishwa wageni katika jamii, hii ni mara ya kwanza kwa mwanamke mwenye asili ya Kituruki kushika wadhifa mkubwa katika serikali kuu ya Ujerumani.

Chama cha CDU cha Merkel na chama ndugu cha CSU vinatazamiwa kutangaza mawaziri wake baade jioni hii.

Waziri wa sasa wa kazi, Ursula von der Leyen, anatazamiwa kuwa mwanamke kwanza kuongoza wizara ya ulinzi katika historia ya Ujerumani.

Thomas de Maiziere akisalimiana na na mwanachama mwenzake wa CDU B Ursula von der Leyen. (09.12.2013).
Thomas de Maiziere akisalimiana na na mwanachama mwenzake wa CDU B Ursula von der Leyen. (09.12.2013).Picha: Reuters

Von der Leyen anaweza kuchukuwa nafasi ya mwanachama mwenzake wa CDU, Thomas de Maizière, ambaye anatazamiwa kurudi kwenye wizara yake ya mambo ya ndani, aliyokuwa ameishikilia kabla.

Hadi miezi michache iliyopita, waziri wa sasa wa mambo ya ndani, Hans-Peter Friedrich, alikuwa ameonekana kwamba angeendelea kuishikilia nafasi hiyo, lakini akajikuta kwenye shinikizo kutoka chama chake mwenyewe, CSU, akishutumiwa kwa kuwa na msimamo mwepesi sana juu ya kashfa ya ujasusi wa mawasiliano uliokuwa ukifanywa na Shirika la Usalama la Marekani, NSA.

Badala yake, Hans-Peter Friedrich, anatajwa huenda akachukua moja ya wizara mbili kati ya tatu za CSU, ama kilimo au maendeleo.

Schäuble kubakia Fedha

Kwa upande mwengine, Bwana Wolfgang Schäuble wa chama cha CDU, anayesifiwa na wengi ndani ya chama kwa hatua zake za kuushughulikia mgogoro wa kifedha kwenye eneo la kanda ya euro, anatarajiwa kuendelea kubakia na wadhifa wake wa waziri wa fedha.

Wolfgang Schäuble waziri wa fedha wa Ujerumani.
Wolfgang Schäuble waziri wa fedha wa Ujerumani.Picha: picture-alliance/dpa

Wakati huo huo, kwa mujibu wa gazeti la Rheinische Post na jarida la habari la Spiegel, katibu mkuu wa sasa wa CDU, Herman Gröhe, huenda akawa waziri wa afya, lakini hakuna uhakika ikiwa waziri wa sasa wa afya, Johanna Wanka, ambaye pia anatokea CDU, ataendelea na nafasi yake.

CSU, mshirika wa CDU kwenye jimbo la Bavaria, kinatazamiwa kupata nafasi tatu za uwaziri, ambapo katibu mkuu wake wa sasa, Alexander Dobrindt, anatajwa kuchukuwa nafasi ya waziri wa usafirishaji, inayoshikiliwa sasa na Peter Ramsauer.

Kiunzi cha mwisho cha serikali hii ya mseto kilivuukwa Jumamosi jioni (14 Disemba 2013) wakati SPD ilipotangaza matokeo ya kura za maoni zilizopigwa na wanachama wake. Asimilia 76 ya kura laki 370,000 ilikubaliana kujiunga na serikali ya muungano na Kansela Merkel, huku kiasi cha asilimia 24 kikisema hapana, kwa mujibu wa mweka hazina wa SPD, Barbara Hendricks.

Serikali hiyo mpya Ujerumani inatazamiwa kuapishwa Jumanne.

Mwandishi: Mohammed Khelef/DW English Website
Mhariri: Mohamed Dahman