1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya amani yafikiwa Colombia

Mjahida24 Septemba 2015

Rais wa Colombia Juan Manuel Santos amesema serikali yake na waasi wa FARC watatia saini makubaliano ya amani ndani ya miezi sita kumaliza mgogoro wa takriban nusu karne.

https://p.dw.com/p/1GdCk
Regierung Kolumbiens hat sich mit den linken Farc-Rebellen geeinigt
Rais wa Colombia Juan Manuel Santos akitoa mkono kwa kiongozi wa waasi wa FARC Timoleon "Timochenko" JimenezPicha: picture-alliance/dpa/A. Ernesto

Rais Santos na kiongozi wa waasi wa FARC Timoleon "Timochenko" Jimenez waliongoza sherehe ambapo wapatanishi wa pande zote mbili walitia saini mpango wa haki kwa uhalifu uliofanywa, wakati wa mgogoro jambo ambalo lilikuwa muhuminu na pingamizi ya kufikia makubaliano ya amani.

Santos amesema yeye pamoja na Timochenko wamekubaliana kuwa katika miezi sita ijayo majadiliano yao yanapaswa kuwa yamemalizika na makubaliano ya mwisho ya amani kutiwa saini.

"Haitakuwa kazi rahisi kwa sababu bado kuna mambo magumu tunayopaswa kukubaliana, lakini hayo ndio maelekezo tuliyoyatoa kwa ujumbe wetu, wanapaswa wakamilishe mkataba haraka iwezekanavyo," alisema rais Santos.

Kuba Havanna FARC Kolumbien Friedensabkommen Rodrigo Londono-Echeverry
Kiongozi wa waasi wa FARC Timoleon "Timochenko" JimenezPicha: picture-alliance/dpa/O. Barria

Ameongeza kuwa amani sasa iko karibu sana na watu wa Comombia pamoja na mamilioni ya watu walioathirika na vita. Rais huyo aliye na miaka 64 alifanya ziara ya kushutukiza mjini Havanna kunakofanyika mazungumzo hayo na ambapo makubaliano ya amani yalitiwa saini. Hii ni mara ya kwanza rais huyo alikutana na kiongozi wa waasi Timochenko na kupeana mikonon baada ya kutiwa saini mpango huo wa amani.

Timochenko, aliye na miaka 56, amesema mpango huo unafungua uwezekano na kutoa ukweli wote kwa waathirika wa mgogoro. Rais wa Cuba Raul Castro pia alikuwepo wakati wa kusainiwa makubaliano hayo.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry apongeza makubaliano

Kwa upande wake Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani ameyapongeza hatua iliyofikiwa kwa kuiita "Maendeleo ya kihistoria" yatakayofikisha kikomo mgogoro uliosababisha mauaji ya zaidi ya watu 220,000 huku wengine milioni sita wakiyakimbia makaazi yao.

Aidha mazungumzo hayo yaliyoanza mjini Havanna mwaka wa 2012 yalisimamishwa kufuatia suala lililokuwa likiwaumiza wengi kichwa juu ya iwapo waasi wa guerrillas watawekwa korokoroni kwa visa vya utekaji nyara, utumiaji wa watoto kama wanajeshi, usafirishaji wa madawa ya kulevya kama cocaine pamoja na uhalifu mwengine.

Großbritannien US-Außenminister John Kerry
Waziri wa Mambo ya nchi za kigeni wa Marekani John KerryPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Vucci

Hata hivyo maafisa kutoka Cuba na Norway nchi zinazoongoza mazungumzo hayo wamesema mpango huo unajumuisha msamaha kwa uhalifu wa kisiasa japokuwa mpango huo hautatoa msamaha kwa uhalifu dhidi ya ubinaadamu, mauaji ya halaiki, uhalifu wa kivita au ukiukwaji mwengine mkubwa.

Mpango huo pia unajumuisha mahakama maalum zikiwa na majaji wa kigheni na wale wa Colombia kuwahukumu wale watakaopatikana na hatia ya uhalifu mkubwa. Aidha wale watakaokubali makosa yao watapata kupunguziwa kifungo chao kwa miaka mitano hadi minane, na wale ambao hawatakubali makosa yao watapewa kifungo cha hadi miaka 20.

Mwandishi: Amina Abubakar

Mhariri: Iddi Ssessanga