1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Merkel yapata pigo kubwa Mecklenburg-Vorpommern

5 Septemba 2011

Serikali ya mseto ya Kansela wa Ujerumani Angela Merkel imepata pigo jipya huku vyama vikuu vya upinzani vikifurahia matokeo ya uchaguzi uliofanywa jimbo la Mecklenburg- Vorpommern, kaskazini-mashariki ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/Rjwa
Der Ministerpräsident von Mecklenburg-Vorpommern und Spitzenkandidat der SPD, Erwin Sellering, jubelt am Sonntag (04.09.2011) in Schwerin nach der Bekanntgabe der ersten Progosen. Die SPD hat die Landtagswahl in Mecklenburg-Vorpommern klar gewonnen. Foto: Jens Büttner dpa/lmv +++(c) dpa - Bildfunk+++
Waziri Mkuu wa jimbo la Mecklenburg-Vorpommern, Erwin SelleringPicha: Picture-alliance/dpa

Chama cha kihafidhina cha Kansela Merkel CDU na cha kiliberali FDP kinachoelemea upande wa wafanyabiashara, mara nyingine tena vimepata pigo kubwa katika uchaguzi wa jimboni. Kinyume na vyama hivyo viwili vinavyoshirikiana katika serikali kuu ya mseto mjini Berlin, vyama vikuu vya upinzani SPD na cha Kijani vinaenedelea kujiimarisha katika chaguzi zinazofanywa majimboni. Chaguzi hizo zinatazamwa kama ni mtihani kwa umaarufu wa serikali kuu mjini Berlin.

Katika uchaguzi wa hapo jana katika jimbo la Kansela Merkel la Mecklenburg-Vorpommern, chama cha kisoshalisti cha SPD kilijinyakulia asilimia 35.7 ya kura zilizopigwa. Chama cha Merkel CDU kimepata asilimia 23.1 ya kura - kinyume na takriban asilimia 29 hapo mwaka 2006. Chama hicho hakijawahi kuwa na matokeo mabaya kama hayo katika jimbo hilo. Mshirika mdogo katika serikali ya mseto ya Merkel FDP, kimeweza kupata asilimia 2.7 tu. Kiongozi wa kundi la wabunge wa CDU mjini Berlin, Peter Altmaier amesema:

"Tumevunjika moyo kuwa CDU kimepoteza kura nyingi kama hizo. Tulitazamia kutunukiwa kwa kazi nzuri tuliyoitekeleza."

Akasisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na umoja kwani hilo ni sharti ili umma uweze kuamini sera zao.

Sigmar Gabriel, chairman of the German Social Democratic Party, (SPD, speaks during a party meeting in Berlin, Germany, Sunday, Sept. 26, 2010. (AP Photo/Michael Sohn)
Mwenyekiti wa chama cha SPD, Sigmar GabrielPicha: AP

Kwa upande mwingine, chama cha SPD kinachoendelea kuimarika katika serikali za majimboni, sasa kitaamua iwapo kiendelee kushirikiana na CDU katika serikali ya muungano jimboni Mecklenburg-Vorpommern au kiunde serikali pamoja na chama cha wakomunisti wa zamani Die Linke, kilichoshinda asilimia 18.4 ya kura.

Mwenyekiti wa SPD, Sigmar Gabriel akizungumza baada ya chama hicho cha kisoshalisti kuibuka mshindi alisema:

"Huo ni mkakati wa ufanisi wa SPD wa tangu zamani - na uliotekelezwa vizuri kabisa na Waziri Mkuu wa jimbo la Mecklenburg-Vorpommern, Erwin Sellering. Ni mchanganyiko wa mafanikio ya kiuchumi na kuwajibika kijamii."

Washindi wengine katika uchaguzi huo ni chama cha Kijani kinachoendelea kuvutia wapiga kura katika chaguzi zinazofanywa majimboni. Ushindi wa asilimia 8.4 ya kura, humaaaisha kuwa chama cha Kijani kwa mara ya kwanza kinaingia katika bunge la jimbo la Mecklenburg-Vorpommern na hivyo kinawasilishwa katika mabunge ya majimbo yote 16 nchini Ujerumani.

FDP kikiendelea kupoteza umaarufu wake miongoni mwa wapiga, kimeshindwa kuvuka kiwango cha asilimia 5 kinachohitajiwa kwa hivyo hakitokuwepo katika bunge la Mecklenburg- Vorpommern. Kwa upande mwingine chama cha NPD cha mrengo wa sera kali za kulia, kitabakia bungeni baada ya kupata asilimia 5.9 ya kura.

Kwa chama cha FDP uchaguzi wa jana ni pigo kubwa sana na tayari kuna uvumi kuwa kiongozi wa zamani wa chama hicho, Guido Westerwelle, alie waziri wa nje wa Ujerumani, huenda akawa mhanga wa matokeo ya uchaguzi huo na hivyo huenda akapoteza wadhifa wake.

Mwandishi:Martin,Prema/ape,dpae

Mhariri: Miraji,Othman