1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Syria na upinzani wakutana Astana

Caro Robi
16 Februari 2017

Maafisa wa serikali ya Syria wamekutana ana kwa ana na wajumbe wa upinzani, hii ikiwa mara ya pili kwa pande hizo mbili kukaa chini kwa mazungumzo katika kipindi cha wiki tatu zilizopita. 

https://p.dw.com/p/2XhpF
Kasachstan Syrien Friedensgespräche in Astana Opposition
Picha: Reuters/M. Kholdorbekov

Duru nyingine ya mazungumzo ya kutafuta amani Syria imeanza mjini Astana, Kazakhstan katika juhudi za wanadiplomasia za kuzipatanisha pande zinazozana Syria kabla ya mazungumzo yanayosimamiwa na Umoja wa Mataifa yatakayofanyika mjini Geneva mnamo tarehe 23 mwezi huu.

Mkutano wa leo wa Astana unalenga kufikia makubaliano ya kusitisha vita kabla ya serikali kukutana na upinzani unaoishi uhamishoni pamoja na wawakilishi wa makundi ya wapiganaji kwa mazungumzo ya amani wiki ijayo yatakayonuia kufikia makubaliano mapana ya kisiasa. Makubaliano ya kusitisha mapigano yamekiukwa mara kadhaa tangu yalipopitishwa tarehe 30 mwezi Desemba mwaka jana.

Je ufumbuzi utapatikana?

Mkuu wa ujumbe wa Iran katika mazungumzo ya Astana amesema mazungumzo hayo yanakumbwa na matatizo na kuulaumu upinzani na wanaowaunga mkono. Iran, Urusi ambayo inaiunga mkono serikali ya Rais Bashar al Assad na Uturuki ambayo inawaunga mkono waasi ndiyo wanaosimamia mazungumzo hayo.

Syiren Präsident Bashar al-Assad Interview
Picha: Reuters

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov amekutana na mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Staffan de Mistura mjini Moscow kujadili mchakato wa amani wa Syria. Lavrov amesisitiza haja ya pande zote kuhusishwa katika mazungumzo ya kutafuta amani. De Mistura amesema mchakato wa kisiasa unapaswa kuharakishwa.

Hata hivyo mshauri wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kibinadamu Jan Egeland amesema Marekani na Urusi hivi karibuni zimekuwa hazishirikiani kuyatatua matatizo ya Syria ya kibinadamu na kuongeza anatumai nchi hizo mbili zitaungana na Uturuki na Iran katika kuondoa kile alichokitaja mkwamo mbaya wa kutoruhusiwa misafara ya magari ya kusafirisha misaada ya kibinadamu.

Wakati huo huo, Rais Assad ameutetea uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kuwapiga marufuku raia wa Syria kuingia Marekani akisema wale wanaolengwa na magaidi na sio watu wa Syria.

Assad amesema magaidi kutoka Syria huenda wakaingia Marekani wakijifanya wakimbizi na kufanya mashambulizi kama yaliyotokea Ulaya na kuongeza lengo lake sasa ni kuukomboa mji wa Raqa na kuapa kuikomboa kila kona ya Syria kutoka mikononi mwa majihadi.

Assad amezishambulia pia nchi za Magharibi kwa kujaribu kuutatua mzozo wa Syria ambao umedumu kwa miaka sita na kusababisha vifo vya zaidi ya watu laki tatu akisema nchi hizo hazina nia ya kupatikana amani Syria.

Mwandishi: Caro Robi/ap/Afp

Mhariri: Grace Patricia Kabogo