1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Syria yajiuzulu

Saumu Ramadhani Yusuf29 Machi 2011

Rais wa Syria Bashar al Asssad ameridhia uamuzi wa kujiuzulu serikali yake kufuatia siku kadhaa za maandamano nchini humo.

https://p.dw.com/p/10jpB
Maandamano dhidi ya serikali yameifanya serikali ya Syria kujiuzuluPicha: AP

Televisheni ya taifa imeripoti kwamba rais al- Assad baadae anatarajiwa kulihutubia taifa kuhusiana na hali ya mambo nchini humo wakati ambapo awali serikali ilikuwa imeripotiwa kuondosha sheria ya hali ya hatari iliyowekwa tangu chama cha Baath kilipotwaa madaraka mwaka 1963.

Mbunge mmoja nchini humo ameliambia shirika la habari la ujerumani la dpa kwamba wabunge wametakiwa kuhudhuria kikao cha bunge hapo kesho asubuhi ingawa sababu ya kuitishwa  kikao hicho cha bunge haijulikani. Maelfu ya watu wa Syria wameingia mitaani nchini humo wakiandamana  katika mji mkuu Damascus pamoja na miji mingine kote nchini humo kumuunga mkono rais wao aliyeingia madarakani mwaka 2000.

Wakibeba mabango wamesikika wakisema kwamba wanautaka ulimwengu kuona na kufahamu kwamba wasyria wanamuunga mkono rais al- Assad.

Maandamano hayo yamefanyika kuyazima maandamano dhidi ya serikali yaliyokuwa yanafanywa nchini humo katika wiki za hivi karibuni maandamano ambayo yamewahusisha maelfu ya watu wanaodai kutaka mageuzi nchini humo,ikiwa ni pamoja na kumtaka rais al- Assad ajiuzulu madarakani.

Makundi ya upinzani nchini humo yanapanga maandamano makubwa yanayotazamiwa kufanyika ijumaa,kwa hivi sasa maduka,benki na shule zimefungwa nchini humo na vikosi vya usalama vimetawanywa katika barabara zote za nchi hii leo.

Televisheni ya taifa imeonyesha maandamano yaliyotokea katika kila miji ya taifa hilo isipokuwa kituo cha Ajazeera kimesema kwamba waandishi wao wa habari wamezuiwa kuingia katika mji ulioko Kusini wa Daraa na Latakia huko Kaskazini.

Serikali imeripotiwa kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali katika miji hiyo miwili.Mpaka sasa inaripotiwa kwamba kiasi ya waandamanaji 61 wameuwawa na vikosi vya usalama ndani na nje ya mji wa Daraa tangu Machi 18.Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadanamu la Human Rights Watch lenye makao yake mjini New York Marekani waandamanaji wengine 12 wameuwawa katika mji wa bandari wa Latakia.

Ama kwa upande mwingine inaarifiwa kwamba maafisa wa Syria wamewakamata wanasheria 4 wanaounga mkono maandamano yanayodai uhuru wa kisiasa na kumalizwa kwa rushwa.

Mwandishi: Saumu Mwasimba/ dpa-rtre

Mhariri: AbdulRahman