1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Zimbabwe yaamuru kufungwa kwa huduma za intaneti

Amina Mjahid
18 Januari 2019

Serikali nchini Zimbabwe imeiamuru kampuni kubwa ya mawasiliano nchini humo Econet kufunga tena huduma zake za interneti kama sehemu ya hatua kubwa iliochukuliwa ya kudhibiti maandamano ya kuipinga serikali

https://p.dw.com/p/3Bn1j
Simbabwe Harare - Nach den Wahlen: Emmerson Mnangagwa, Präsident von Simbabwe, lächelt im Anschluss an eine Pressekonferenz
Picha: picture-alliance/dpa/AP/T. Mukwazhi

Katika taarifa yake hii leo kampuni hiyo ya mawasiliano ya Econet imesema imepewa maagizo ya kufunga kabisa mawasiliano ya inteneti hadi pale watakapopewa maagizo mengine ya kufungua huduma hiyo. Econet  imesema imeshauriwa na mawakili wake kuendelea kutii amri ya serikali hadi pale mahakama itakapotoa uamuzi wake juu ya uhalali wa hatua iliochukuliwa.

Simbabwe Harare Benzinkrise Ausschreitungen
Baadhi ya waandamanaji mjini HararePicha: Reuters/P. Bulawayo

Uamuzi wa serikali ya kufungia huduma hiyo ni suala ambalo bado linawasilishwa katika mahakama ya juu nchini humo. Hata hivyo Naibu waziri wa Habari Zimbabwe Energy Mutodi amesema mawasiliano hayo yatarejeshwa hapo kesho.

Mutodi amesema walitoa amri ya kufungiwa kwa mara ya kwanza huduma za Interneti siku ya Jumanne wiki hii, maana waliona waandamanaji walianza kupanga maandamano zaidi kupitia mitandao ya kijamii huku akitetea hatua ya serikali kwa kusema kuwa kile wanachokifanya ni sahihi.

Hatua hiyo inakuja wiki moja baada ya maandamano makubwa ya kiuchumi yaliosababisha watu watano kuuwawa na wengine wengi kujeruihiwa  huku mkosoaji mkubwa wa serikali Evan Mawarire akiwa miongoni mwa watu 600 waliokamatwa wengi wao wakiwa viongozi wa upinzani.

Umoja wa Mataifa wataka pande zote kujizuwiya na vurugu

Wazimbabwe waliandamana kupinga hatua ya rais Emmerson Mnangagwa kupandisha maradufu bei ya mafuta. Umoja wa Ulaya leo umepaza sauti yake juu ya kile kinachoendelea nchini Zimbabwe kwa kulaani matumizi ya nguvu kupita kiasi dhidi ya waandamanji.

Msemaji wa mkuu wa sera za kigeni katika Umoja huo Federica Mogherini amesema wanatarajia serikali kufanya uchunguzi wa kina juu ya mauaji na visa vya maonevu vilivyoripotiwa. Umoja wa Ulaya umetaka huduma za internet kurejeshwa mara moja.

Simbabwe Evan Mawarire Pastor Aktivist
Mkosoaji mkubwa wa serikali ya Zimbabwe Evan Mawarire Picha: Getty Images/AFP/J. Njikizana

Wakati huo huo Shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia haki za binaadamu UNHCR limesema ina wasiwasi mkubwa juu ya ukandamizaji wa waandamanaji na matumizi ya risasi za moto.

Umoja huo umesema ni muhimu pande zote wakiwemo waandamanaji wajizuwiye kufanya vurugu  na kutafuta njia ya kusuluhisha tatizo kwa amani.

Zimbabwe imetumbukia katika mgogoro wa ukosefu wa pesa taslimu kitu ambacho rais Mnangagwa aliahidi kukirekebisha tangu mtangulizi wake Robert Mugabe alipoondolewa madarakani mwaka 2017 kupitia kile kilichotajwa kama mapinduzi ya kijeshi.

Mwandishi: Amina Abubakar/AFP/AP

Mhariri: Yusuf Saumu