1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sessions ajiondoa kwenye uchunguzi

John Juma
3 Machi 2017

Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Jeff Sessions amejiondoa rasmi kutoka kwenye uchunguzi kuhusu uhusiano kati ya timu ya kampeni ya Donald Trump na Urusi.

https://p.dw.com/p/2YaKV
USA Justizminister Jeff Sessions | Erklärung zu Russland-Kontakten
Picha: Getty Images/W. McNamee

Jenerali Jeff Sessions amejiondoa kwenye uchunguzi kuhusu kujiingiza wa Urusi katika kampeni za Rais Donald Trump mwaka uliopita. Tangazo la mwanasheria huyo mkuu wa Marekani linajiri baada ya shinikizo kutoka kwa wabunge wa Democrat waliotaka ajiuzulu kufuatia ripoti kwamba hakuieleza kamati ya seneti juu ya mazungumzo aliyoyafanya na balozi wa Urusi  katika kipindi cha kampeni hiyo.

Kutokana na uungwaji mkono thabiti kutoka kwa Rais Donald Trump, wito wa kumtaka ajiuzulu haujaitikiwa, kufuatia madai kwamba alilidanganya baraza la kuhusu mikutano aliyoyafanya na balozi wa Urusi Sergey Kislyak kabla ya uchaguzi mkuu uliopita. Lakini siku ya Alahamisi, Sessions alisema kuwa baada ya kuzingatia sheria za maadili ya ofisi yake na ushauri kutoka kwa maafisa wake, hana budi kujitoa kwenye uchunguzi, lakini hatua hiyo isichukuliwe kama ni kukubali makosa. "Nimeamua kujitenga na uchunguzi wowote unaoendelea au ujao unaohusu kwa namna moja au nyingine kampeni za rais wa Marekani. Ukitathmini sheria, ninahisi sipaswi kuhusika katika uchunguzi wa kampeni ambayo nilihusika."

Mjumbe wa Democrat Nancy Pelosi na mwenyekiti wa bunge la Vietnam, Nguyen Sinh
Mjumbe wa Democrat Nancy Pelosi na mwenyekiti wa bunge la Vietnam, Nguyen SinhPicha: Reuters/Kham

Wademocrats wengine wametaka uchunguzi huru na mchunguzi maalum mpya kusimamia uchunguzi huo. Kiongozi wa walio wachache bungeni Nancy Pelosi alimlaumu Sessions kwa kuidanganya kamati iliyokuwa ikimuidhinisha mwezi Januari. "Kwamba mwanasheria mkuu, mlinzi mkuu wa sheria nchini alidanganya Wamarekani kwa kula kiapo, ni msingi tosha kwake kujiuzulu. Amethibitisha kuwa hajahitimu na hastahili kutumikia wadhifa unaohitaji uaminifu."

Hapo jana Sessions alisema kuwa maelezo yake mbele ya kamati ya seneti iliyomuidhinisha yalihusu ikiwa kulikuwa na mahusiano yoyote na Warusi kwa niaba ya au kuhusu kampeni za urais, huku akiongeza kuwa yeye na Kislyak walizungumzia tu siasa za kimataifa. Licha ya madai yanayomkabili Rais Donald Trump ameendelea kumunga mkono huku akimtaja kuwa mtu mwaminifu. Aidha Trump ameeleza kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa Sessions hakusema lolote baya huku akielekeza lawama kwa wajumbe wa Democrats kuendeleza hujuma za kisiasa baada ya kushindwa katika uchaguzi wa rais.

Jeff Sessions akipongezwa na Rais Donald Trump
Jeff Sessions akipongezwa na Rais Donald TrumpPicha: Reuters/K. Lamarque

Mwezi uliopita, aliyekuwa mshauri wa Trump kuhusu usalama Michael Flynn alilazimika kujiuzulu ilipobainika kuwa aliwapotosha maafisa kuhusu mazungumzo yake na balozi wa Urusi. Ikulu ya White House imekanusha madai kuwa washirika wa kampeni ya Trump walishirikiana na Urusi kuingilia uchaguzi.

Kando na hayo shirika moja la habari pia limemtaja makamu wa rais Mike Pence kuwa alitumia anuani yake binafsi katika  masuala ya umma alipokuwa gavana wa Indiana.

Mwandishi: John Juma/AFPE/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman