1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sessions akana njama na Urusi, atetea kutimuliwa Comey

Iddi Ssessanga
14 Juni 2017

Mwanasheria mkuu wa Marekani Jeff Sessions amekana kufahamu kuhusu mahusiano kati ya timu ya kampeni ya Trump na Urusi. Sessions pia amejibu maswali kuhusu kufutwa kazi kwa mkurugenzi wa zamani wa FBI James Comey.

https://p.dw.com/p/2efhT
Jeff Sessions USA Anhörung
Picha: Getty Images/S.Loeb

Katika ushahidi uliofuatiliwa kwa karibu mbele ya kamati ya upelelezi ya baraza la Seneti jana Jumanne, Mwanasheria Mkuu wa Marekani Jeff Sessions alikanusha vikali madai kwamba alikula njama na maafisa wa Urusi wakati wa kampeini ili kumpa ushindi rais Donald Trump.

"Madai kwamba nilishiriki katika njama yoyote, kwamba nilikuwa nafahamu kuhusu njama yoyote ya serikali ya Urusi kuliumiza taifa hili...au kuvuruga uaminifu wa mchakato wa demokriasia yetu, ni uongo wa kuchukiza," alisema Sessions.

Sessions alisema uamuzi wake wa kujitoa katika chunguzi zote zinazoondelea ulitokana na sheria inayomtaka kujiweka kando kutokana na ushiriki wake katika kampeni za Trump. Alisisitiza kuwa hakujuwa kuhusu uchunguzi wa Urusi au alihusika katika uchunguzi.

Jeff Sessions Anhörung
Jeff Sessions alipowasili kutoa ushahidi mbele ya kamati ya uchunguzi ya baraza la Seneti mjini Washington Juni 13,2017.Picha: Getty Images/P.J.Richards

Sessions pia ajitetea dhidi ya tuhuma kwamba alipotosha pale aliposema hakukutana na maafisa wa Urusi wakati wa kampeni katika kikako cha kumthibitisha katika nafasi hiyo. Waziri huyo wa Sheria hakujiweka kando na uchunguzi wa Urusi hadi Machi 2, siku moja baada ya gazeti la Washington Post kuripoti kuhusu mikutano yake miwili na balozi wa Urusi Sergey Kislyak, ambayo hakuitaja.

Mbinyo kuhusu kufutwa kazi kwa Comey

Sesseions pia aliulizwa maswali kadhaa kuhusu mchango wake katika kufutwa kazi kwa James Comey. Mkurugenzi huyo wa zamani wa shirika la FBI alisema katika ushahidi wake wiki iliopita kuwa rais wa Marekani Donald Trump alimfuta kazi kama sehemu ya juhudi za kushawishi uchunguzi wa Urusi.

Msimamizi huyo wa juu wa sheria nchini humo alisema alipendekeza kuwepo na mwanzo mpya kwa FBI, lakini hakutoa ufafanuzi kuhusu mazungumzo yake na Trump kuhusu suala hilo.

Pia alikataa kusema iwapo alijadili suala la uchunguzi wa Urusi na Trump, akisema hawezi kuweka wazi mazungumzo ya faragha na rais. Wakati akitoa ushahidi wake wiki iliopita, Comey alisema kulikuwepo na jambo lakutatiza kuhusu kujitoa kwa Sessions katika uchunguzi wa Urusi. Alipoulizwa suala gani lilikuwa na matatizo, Sessions alikasirika.

USA Anhörung James Comey, früherer FBI-Direktor
Mkurugenzi wa zamani wa FBI James Comey alitilia mashaka mwenendo wa Sesseions wakati akitoa ushahid mbele ya kamati kuhusu madai ya Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani Juni 8, 2017.Picha: Getty Images/AFP/B. Smialowski

"Hivi ni vijembe vya siri vinavyovujishwa nje kunihusu, na sifurahii. Watu wanajaribu kusema kupitia vijembe kwamba sikuwa mkweli kuhusu mambo haya na nimejaribu kuwa muwazi," alisema Sessions.

Alipoulizwa kuhusu matamshi ya Trump kwamba alimfuta kazi Comey akiwa na uchunguzi wa Urusi akilini mwake na bila kujali mapendekezo kutoka kwa mtu yeyote mwingine, Sessions alisema anayaacha maneno ya Trump yajielezee na hana uhakika nini alikuwa anakiwaza hasa akilini mwake.

Kikao cha Jumanne ndiyo kilikuwa ushahidi wa kwanza wa wazi wa Sessions tangu alipothibitishwa kuwa Mwanasheria mkuu mwezi Februari, na umekuja mnamo wakati kukiwa na chunguzi kadhaa za wazi katika uwezekano wa kuwepo na njama kati ya timu ya kampeni ya Trump na maafisa wa Urusi.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe, rtre

Mhariri: Bruce Amani