1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio lajeruhi watu wanne Ujerumani

Admin.WagnerD19 Julai 2016

Kijana wa miaka 17 mkimbizi kutoka Afghanistan jana(18.07.2016)aliwashambulia watu katika treni kwa visu na shoka, na maafisa wamesema wana imani alikuwa na hamasa za itikadi kali ya Kiislamu katikashambulio hilo.

https://p.dw.com/p/1JRKv
Deutschland Attacke in Regionalzug bei Würzburg
Eneo la shambulio lililofanywa na kijana wa miaka 17 kutoka AfghanistanPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Mchoro wa mkono wenye bendera ya kundi la itikadi kali la Dola la Kiislamu ulikutwa katika chumba alichokuwa akiishi kijana huyo mkimbizi kutoka Afghanistan aliyewashambulia abiria katika treni kusini mwa Ujerumani, amesema afisa mwandamizi wa jimbo la Bavaria leo.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 17 aliwajeruhi vibaya abiria wanne kabla ya polisi kumpiga risasi kijana huyo jana, siku kadhaa baada ya Mtunisia kuendesha lori la tani 19 na kuwauwa watu 84 miongoni mwa watu waliokuwa wakipunga upepo, katika mji wa kusini nchini Ufaransa wa Nice.

Deutschland Attacke in Regionalzug bei Würzburg
Polisi wakiwa katika shughuli za kuwasaidia waliojeruhiwa na kulinda usalama WürzburgPicha: picture-alliance/dpa/K. J. Hildenbrand

Shambulio hilo katika treni karibu na mji wa kusini wa Wuerzbug jana Jumatatu limewaacha watu wawili wakiwa katika hali mbaya, amesema Joachim Herrmann, waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria. Kijana huyo aliyefanya mashambulizi aliuwawa wakati akijaribu kukimbia.

"Tuna matumaini kwamba wale waliojeruhiwa vibaya wataweza kurejea katika hali ya kawaida, " Herrmann aliiambia televisheni ya Ujerumani ya ZDF.

Kilichomvutia mshambuliaji

"Ishara ya kwanza ya dharura kulifikia jeshi la polisi kutoka katika treni hiyo, ni kwamba watu walioshuhudia walisema kwamba mshambuliaji alisema , Allahu Akbar. Na baada ya uchunguzi wa chumba anachoishi, mchoro wa mkono wenye bendera ya IS ulipatikana.

Deutschland Attacke in Regionalzug bei Würzburg
Polisi wakiwa katika eneo nla tukioPicha: picture-alliance/dpa/K. J. Hildenbrand

Haya yote ukiyaweka pamoja, yanaonesha kilichomvutia kufanya hivyo, na kwamba tunaweza kuona malengo ya itikadi kali za Kiislamu na kwamba anaweza kuwa amehamasika binafsi kuingia katika itikadi kali."

Tukio hilo bila shaka linaweza kuimarisha wasi wasi juu ya kile kinachoelezwa kuwa ni "washambuliaji binafsi" katika bara la Ulaya na linaweza kuweka mbinyo wa kisiasa kwa kansela Angela Merkel, ambaye aliwakaribisha mamia kwa maelfu ya wahamiaji nchini Ujerumani mwaka mmoja uliopita.

Deutschland Attacke in Regionalzug bei Würzburg
walinzi wa amani karibu na mji wa Würzburg nchini UjerumaniPicha: Reuters/K. Pfaffenbach

Waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la Bavaria Joachim Herrmann alisema kwamba ni mapema mno hata hivyo kusema iwapo kijana huyo M'afghanistan alikuwa mwanachama wa kundi la Dola la Kiislamu , ambalo lilidai kuhusika na shambulio nchini Ufaransa, ama kundi jingine lolote la wanamgambo, licha ya kundi hilo kudai leo kwamba kijana huyo alikuwa mmoja kati ya wapiganaji wa kundi hilo.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe

Mhariri:Josephat Charo