1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanamgambo wa IS wakiri kuhusika na shambulizi la Kabul.

Amina Mjahid
29 Januari 2018

Watu waliokuwa na bunduki na washambuliaji wa kujitoa muhanga wamefanya shambulizi katika kambi moja ya kijeshi na kusababisha mauaji ya wanajeshi 11 katika shambulizi la tatu kubwa la hivi karibuni mjini Kabul.

https://p.dw.com/p/2rgvU
Afghanistan Angriff auf Militärbasis in Kabul
Picha: Reuters/M. Ismail

Misururu ya mashambulizi hayo likiwemo moja ya shambulizi baya zaidi kutokea mjini Kabul katika siku za hivi karibuni, limewaacha wakaazi wa mji huo na hofu na ghadhabu kubwa wakati wanamgambo wa Taliban na wale wanaojiita dola la kiislamu wakizidi kuimarisha hujuma zao.

Shambulizi la leo katika kambi ya kijeshi limesababisha mauaji ya wanajeshi 11 huku wengine 16 wakijeruhiwa hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa wizara ya ulinzi wa Afghanistan.

Afghanistan Anschlag in Kabul
Mmmoja wa maafisa wa Usalama akishika doria KabulPicha: picture-alliance/Zuma Press/Xinhua/R. Alizadah

"Washambuliaji wawili walijiripua huku wengine wawili wakiuwawa na vikosi vyetu, mmoja anazuiliwa," alisema msemaji huyo Dawlat Waziri, alipokuwa akizungumza na shirika la habari la  AFP huku akisisitiza kuwa kwa sasa mashambulizi yamekwisha.

Aidha maafisa wamesema wanaume hao waliokuwa na kombora, bunduki za kijeshi pamoja na vesti zilizosheheni mabomu, walijaribu kuingia kwenye kambi moja ya kijeshi karibu na chuo kimoja cha mafunzo ya kijeshi ambapo maafisa wa juu hupokea mafunzo yao.

Afisa mmoja katika chuo hicho amesema alisikia milio ya risasi na miripuko huku wale walioshuhudia wakisema shambulizi la kwanza na milio ya risasi ilianza kusikika mwendo wa saa kumi na moja alfajiri.

Wanamgambo wazidi kuimarisha hujuma zao mjini Kabul

Mwezi October mshambuliaji wa kujitoa muhanga alisababisha mauaji ya wanajeshi 15 walipokuwa wanasafiri kuelekea nyumbani kutoka katika chuo hicho cha kijeshi cha Marshal Fahim.

Jumamosi iliyopita mwanamgambo mmoja wa Taliban aliyeendesha gari la kupeleka wagonjwa lililojaa mabomu aliliripua katika eneo lililojaa watu mjini Kabul na kusababisha mauaji ya watu 103 wengi wakiwa raia na takriban watu 235 wakijeruhiwa katika moja ya matukio mabaya zaidi kutokea katika miaka ya hivi karibuni.

Afghanistan Taliban Kämpfer in der Provinz Zabul
Baadhi ya wanamgambo wa Taliban Picha: picture-alliance/AP Photo/M. Khan

Aidha wanamgambo wakiwemo wale wa Taliban na dola la kiislamu wamezidi kuimarisha mashambulizi yao dhidi ya wanajeshi wa Afghanistan na polisi katika miezi ya hivi karibuni. Mashambulizi hayo yameongezeka tangu vikosi vya Kimataifa vilivyoondoa majeshi yao nchini humo mwaka 2014.

Wakati huo huo raia wa Afghanistan waliendelea kuelezea masikitiko yao na hasira juu ya mashambulizi ya mara kwa mara yanayotokea mjini Kabul. Aftab Ali alieandika katika mtandao wake wa kijamii wa facebook kwamba mungu aziangamize  nyumba zao, kwakuwa wanasababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia.

Kwengineko ofisi ya rais wa Afghanistan imetoa taarifa inayoeleza kwamba rais wa Indonesia  Joko Jokowi Widodo yuko nchini Afghanistan kwa ziara rasmi. Rais Ashraf Ghani na mgeni wake  watakuwa na mkutano na waandishi habari baada ya kikao chao hii leo.

Mwandishi Amina AbubakarAFP/AP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu