1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shinikizo lazidi kuongezea dhidi ya Muammar Gaddafi

18 Mei 2011

Shinikizo dhidi ya kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi limezidi kuongezeka baada ya kusalitiwa na waziri wake, mashambulizi ya NATO mjini Tripoli pamoja na shinikizo la mahakama ya kimataifa ICC kutaka kukamatwa kwake.

https://p.dw.com/p/11Iks
Kiongozi wa Libya, Muammar GaddafiPicha: dapd

Serikali ya Tunisia imeliambia Shirika la Habari la Ufaransa kwamba Waziri wa Mafuta wa Libya Shukri Ghunem ambae ni mkongwe katika utawala wa Ghaddafi ameondoka nchini humo na kuingia nchini humo.

Ghunem, ambae pia ni mwenyekiti wa kampuni ya mafuta ya Libya, ameonekana akivuka mpaka wa nchi yake na Kuingia Tunisia ambapo anadaiwa kukodi hoteli moja ya kitalii iliyopo katika kisiwa cha kitalii cha Djerba.

Hata hivyo ilipohojiwa mamkala ya hoteli hiyo ilikiri kuwa kiongozi huyo alifikia katika hoteli hiyo na familia yake lakini ameondoka kuelekea kusiko julikana mapema jana.

Kama itathibitika kwamba kiongozi huyo ametoroka,itakuwa ni miongoni mwa viongozi wa ngazi ya juu kumtelekeza Ghaddafi tangu kuzuka kwa vuguvugu la kisiasa nchini Libya katikati ya Februari mwaka huu.

Na Waasi wanataka kuitumia vyema nafasi ya kuondoka kwa Ghunem ambapo sasa wanataka uwakilishi wa nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta katika mkutano wa OPEC wa Juni.

Msemaji wa waasi hao Mahmud Shammam amedai wataangalia taratibu za kisheria na pia kusubiri kama OPEC itawaalika.

Huko nchini Urusi, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Sergei Lavrov amesema alikuwa na mkutano na ujumbe wa Gaddafi na ameutaka kufuata matakwa ya azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa.

Ziara ya ujumbe unaoongozwa na Muhammad Ahmed al-Sharif, katibu mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Wito wa Kiislamu yenye makao yake makuu mjini Tripoli ambayo inafadhiliwa na Gaddafi inafanyika wakati Urusi ikijiandaa kukutana na upande wa Waasi.

Libyen Rebellen
Mpiganaji muasi nchini LibyaPicha: picture alliance/dpa

Lavrov amesema Libya ipo tayari kushirikiana na waasi ikiwa watakubali pamoja na NATO kuacha mashambulizi.

Urusi ambayo imekuwa ikikosoa kwa nguvu zake zote kampeni ya kimataifa dhidi ya utawala wa Gaddafi imepanga kuzungumza na pande zote mbili za serikali na waasi ambao ziara yao nchini Urusi itachelewa kidogo.

Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Gerard Longuest amesema mashambulizi ya anga ya ndege za NATO yamesambaratisha kabisa ndege za kivita za Gaddafi pamoja na kulipunguza nguvu sana jeshi lake.

Na Canada ambayo inashiriki katika operesheni ya NATO nchini Libya imewafukuza mabalozi watano wanaoiwakilisha Libya nchini humo.

Nchi hiyo imesema hakuna uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili kwa sasa. Na hata ubalozi wa Canada nchini Libya umefungwa kwa wiki kadhaa sasa.

Mwandishi: Sudi Mnettte RTR//AFP

Mhariri Yusuf Saumu