1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la fedha la kimataifa laonya uchumi usizidi kuzorota

21 Septemba 2011

Picha ya kutisha ya shughuli za kiuchumi za dunia imetolewa na shirika la fedha la kimataifa muda mfupi kabla ya mkutano wake wa msimu wa mapukutiko kuanza kesho mjini Washington

https://p.dw.com/p/12dPS
Nembo ya mkutano wa kesho wa IMF na benki kuu ya dunia msimu wa mapukutikoPicha: DW

Wakishindwa hadi wakati huu kumaliza migogoro ya fedha inayozitikisa nchi za eneo la sarafu ya Euro, mabwana fedha wakubwa wakubwa wa dunia wamekusanyika mjini Washington kudhihirisha kwa pamoja kwamba wanaweza kuzuwia uchumi usiporomoke, tena bila ya kuzidisha mzigo wa madeni.

Picha iliyochorwa jana usiku na shirika la fedha la kimataifa haisaidii kutuliza hali ya mambo katika masoko ya hisa: kudorora hali jumla ya kiuchumi na matarajio duni hasa kwa nchi za magharibi, kikiwepo hata kitisho cha kuzorota upya ukuaji wa kiuchumi nchini Marekani na Ulaya ikiwa serikali hazitatekeleza ahadi zao.

Akichambua makadirio ya maendeleo ya uchumi wa dunia mjini Washington jana, mkuu wa shughuli za kiuchumi wa shirika la fedha la kimataifa, Olivier Blanchard, amesema

"Uchumi wa dunia umeingia katika awamu mpya na ya hatari kupita kiasi. Ishara za uchumi kufufuka upya zimedhoofika na hatari ya kudorora upya shughuli za kiuchumi imeongezeka sana. Kinachohitajika hivi sasa ni hatua kali na za dhati za serikali ili kuweza kuimarisha makadirio ya ukuaji wa kiuchumi na kupunguza kitisho kilichoko."

G7-Finanzminister beraten‎ in Marseille Frankreich Christine Lagarde 2011
Mkuu wa shirika la fedha la kimataifa Christine LagardePicha: AP

Makadirio hayo yanathibitisha hali iliyochomoza tangu msimu wa kiangazi. Hata hivyo, mawaziri wa fedha wa dunia wanashindwa kutoa risala za kutuliza hali ya mambo.

"Jibu la maana lililoahidiwa Sepetmber 7 na nchi 7 tajiri -G7- halikusaidia kitu.Na mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya na Marekani waliagana jumamosi iliyopita nchini Poland bila ya kufikia makubaliano wala kutangaza tiba yoyote ya migogoro inayozikaba upya nchi za zoni ya Euro.

Kwa mujibu wa makadirio ya hali ya kiuchumi ya dunia yaliyofafanuliwa jana na shirika la fedha la kimataifa-IMF- uchumi wa dunia unaweza kukuwa kwa kiwango cha wastani cha asili mia nne tu na sio asili mia nne na nusu kama ilivyokadiriwa msimu wa kiangazi mwaka huu. Katika nchi zinazoinukia kiuchumi shirika la fedha la kimataifa linakadiria ukuaji wa kiuchumi wa asili mia 6.5 na katika nchi zilizoendelea ukuaji wa kiuchumi hautapindukia asili moja moja nukta sita mwaka huu.

Dilma Rousseff
Rais wa Brazil Dilma RousseffPicha: AP

Wawakilishi wa kundi la nchi zinazoinukia, zikiwemo Brazil, Urusi, India, China na Afrika kusini wamewasili Washington wakipania kubainisha hakuna maamuzi yanaweza kupitishwa bila ya wao pia kushirikishwa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/afp

Mhariri: Miraji Othman