1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la mazingira Ujerumani lakosoa kombe la dunia 2030

Zainab Aziz
5 Oktoba 2023

Shirika la mazingira la Ujerumani “Sports for Future” limekosoa uamuzi wa kuandaliwa kwa michuano ya Kombe la Dunia la mwaka 2030 katika nchi sita badala ya mabara matatu.

https://p.dw.com/p/4XA7j
FIFA - Sitzung in Shanghai - Gianni Infantino
Picha: picture alliance/dpa/XinHua

Mwenyekiti wa shirika hilo Stefan Wagner ameliambia shirika la habari la dpa kuwa, licha ya uamuzi huo kuhalalishwa na historia lakini umepitwa na wakati.

Wagner ameeleza kuwa, kutokana na uamuzi huo shirikisho la kandanda duniani FIFA limeonyesha wazi kwamba uhifadhi wa hali ya hewa sio kipaumbele chake.

FIFA hapo jana Jumatano ilisema, michuano ya Kombe la Dunia la mwaka 2030 itafanyika Morocco, Ureno na Uhispania baada ya mechi tatu za ufunguzi kuchezwa Argentina, Paraguay na Uruguay kama sehemu ya kusherehekea maadhimisho ya karne moja ya michuano hiyo ya dunia.

FIFA imesema nchi hizo tatu za Morocco, Ureno na Uhispania ndio wenyeji rasmi wa michuano hiyo itakayoshirikisha timu 48.