1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la WHO lafanya juhudi kuudhibiti ugonjwa wa Ebola

Josephat Charo
27 Mei 2018

Mripuko wa ugonjwa wa ebola katika Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na hatua ya kanisa Katoliki kuitisha maandamano kupinga mauaji ya kiholela ni miongoni mwa masuala yaliyoripotiwa na magazeti ya Ujerumani wiki hii.

https://p.dw.com/p/2yOh5
DR Kongo Ebola Ausbruch
Picha: Reuters/J. R. N'Kengo

Gazeti la Berliner Zeitung lilikuwa na kichwa na habari kilichosema "Katika hali ya tahadhari - mlipuko wa ebola Congo waliweka shirika la afya duniani WHO katika changamoto kubwa."

Mhariri wa gazeti hilo alisema mabadiliko yanaonekana kuwa yasiyo na athari zozote, lakini yanachukuliwa kwa uzito na uangalifu mkubwa. Nje ya maeneo ya biashara vyombo vya kuwekea maji vimewekwa, ndoo za plastiki zikiwa na dawa ya kuua vijidudu, ambayo wateja wanatumia kunawa mikono yao. Hata watu wanaofahamiana wanapokutana barabarani hawasalimiani kwa kupeana mikono.

Na katika maeneo ambako ugonjwa huu umejitokeza kunashuhudiwa foleni ndefu za watu wanaosubiri kuhudumiwa na wataalamu wa wa afya waliovalia magauni meupe pepepe wenye vifaa vya kupimia viwango vya joto mwilini mfano wa bunduki. Kwa siku kadhaa mji wa bandari wa ziwa Congo, Mbadaka, mji mkuu wa jimbo la Equator hali imebadilika. Tangia kisa cha kwanza cha maambukizi ya Ebola kilipogunduliwa mjini humo, wakazi zaidi ya milioni moja wa mji huo wako katika hali ya tahadhari kubwa.

Gazeti hilo la Berliner Zeitung lilimnukuu mwalimu wa shule ya msingi mjini Mbandaka Jean Mpono mwenye umri wa miaka 53, akisema wanafunzi hawaruhusiwi kutangamana kuepusha maambukizi. Kilichobaki ni kuomba tu kwamba janga hili halienei katika maeneo mengine.

Matumaini yapo kuudhibiri ugonjwa wa Ebola

Mhariri pia alisema yapo matumaini kutokana na jinsi wataalamu walivyoushughulikia kwa haraka mlipuko wa ebola safari hii, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita katika eneo la Afrika Magharibi. Wakati huo shirika la WHO lilikaa miezi kadhaa pasipo kuchukua hatua tangu kisa cha kwanza cha ebola kilipogunduliwa.

Ebola ikaenea Liberia, Guinea na Sierra Leone kama moto wa nyikani mpaka watu 26,0000 wakaambukizwa na 11,300 kati yao wakafa. Kutokana ha hali hiyo shirika la WHO likapata somo la wazi ndio maana sasa limechukua hatua za haraka, hata mkuu wake, Tedros Adhanom Ghebreyesus, akafanya ziara nchini Congo kujionea hali halisi ilivyo. Mhariri alisema ziara hiyo ilikuwa zaidi ya kampeni ya kulitangaza shirika hilo.

Nalo gazeti la Stern liliandika katika kichwa chake cha habari: Je, kuna kitisho cha janga jipya la mlipuko wa Ebola? Mhariri alisema Ebola imelipuka tena nchini Congo. Hofu ya kutokea janga kama lile lililotokea mwaka 2014 Afrika Magharibi ni kubwa.

Kanisa Katoliki Nigeria laitisha maandamano

Mada ya pili iliyowashughulisha wahariri wa magazeti ya Ujerumani wiki hii ni maziko ya mapadri wawili wa kanisa Katoliki pamoja na waumi 17 siku ya Jumanne, takriban mwezi mmoja tangu walipouliwa wakati kanisa lao la mtakatifu Ignatius liliposhambuliwa huko mjini Mbalom. Gazeti la die Tageszeitung lilizungumzia "Maombelezo na hali ya kukata tamaa nchini Nigeria".

Fulani Konflikt
Maiti zikizikwa za watu waliouliwa kwenye mzozo kati ya jamii za wakulima na wafugaji NigeriaPicha: Getty Images/P. Utomi Ekpei

Mhariri wa gazeti hilo alisema baada ya mauaji hayo ya kiholela kanisa Katoliki lilitoa tangazo lenye athari zaidi ya elfu moja. Kanisa hilo limefaulu kufanya kile ambacho mashirika ya kutetea haki za binadamu na mashirika mengine yenye masilahi hayajawahi kukifanya Nigeria, wala hata kujaribu tu. Wakati wa maziko siku ya Jumanne kanisa Katoliki liliwatolea wito watu wajitokeze kwa maandamano katika miji mbalimbali na katika ibada maalamu ya maombolezo huko Mbalom.

Maandamano yalishuhudiwa katika mji mkuu Abuja na mji wa Makurdi, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Benue. Kwa njia hiyo kanisa limeweka wazi kutoridhika kwake na serikali ya rais Muhammadu Buhari. Wakati huo huo mzozo katikati mwa Nigeria ambao hadi sasa umekuwa mzozo wa kupigania rasilimali kati ya wakulima na wafugaji, umechukua taswira mpya. Rais Buhari ambaye aliliagiza jeshi kulinda amani amelauliwa kwa kutochukua hatua madhubuti kwa kuwa wafugaji ni watu wa kabila lake.

Eneo huru la kibiashara Afrika

Gazeti la Frankfurter Allgemeine liliripoti juu ya eneo huru la biashara barani Afrika. Mhariri anasema mataifa mengi barani humo yamefanya mabadiliko kuboresha mazingira ya wawekezaji kutoka nje kuanzisha biashara.

Ruanda Kigali Unterzeichnung Afrikanisches Freihandelsabkommen
Mkataba wa kuunda eneo huru barani Afrika ulisainiwa Kigali, RwandaPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/G. Dusabe

Gazeti hilo la Frankfurter Allgemeine lilisema hata wafanyabiashara wa Ujerumani walisitasita kuwekeza katika taifa lolote la Afrika miaka iliyopita kutokana na masharti magumu, vikwazo vya kibiashara na rushwa iliyokithiri. Lakini sasa mataifa mengi yamefanya mageuzi katika miaka michache iliyopita kuboresha mazingira kwa wawekezaji wa kigeni kufanyia biashara.

Katika nchi nyingi za Afrika sasa wawekezaji hawahitaji tena kuwa na washirika wa ndani. Imekuwa rahisi sasa kuhamisha faida kutokana na biashara inayoendelea au hata baada ya kuuza kampuni na kuhamia nje ya Afrika. Imekuwa rahisi na haraka kuanzisha biashara. Yote haya ni baadhi ya mambo yaliyozikwamisha kampuni za kigeni kuwekeza Afrika. Mkataba wa kuunda eneo huru la kibiashara Afrika uliosainiwa na nchi 44 kati ya 55 za Afrika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu mjini Kigali nchini Rwanda huenda ukazidi kuleta mabadiliko yenye manufaa.

Rushwa bado changamoto Afrika Kusini

"Mwisho wa ndoto ya taifa la upinde wa mvua" - Ndivyo lilivyoandika gazeti la Süddeutsche Zeitung. Raia wengi wa Afrika Kusini wamekatishwa tamaa na chama tawala cha African National Congress, ANC, kutokana na rushwa na wameyaweka matumaini yao kwa chama cha Democratic Alliance, DA.  Lakini sasa hata chama hicho nacho kimekosa fursa kubwa ya kupata muarubaini wa tatizo la rushwa Afrika Kusini.

Südafrika Mmusi Maimane
Mmusi Maimane, Mkuu wa chama cha Democratic AllaincePicha: imago/Gallo Images

Mhariri wa gazeti la Süddeutsche Zeitung alielezea juu ya bango la chama cha Democratic Alliance linalowakaribisha wageni katika uwanja wa ndege mjini Cape Town likiwa na picha ya meya wa mji huo, Patricia De Lille. Lakini bango hilo limepitwa na wakati kwa kuwa Patricia si meya tena wa mji huo na wakazi wengi wamepoteza muelekeo. Chama cha Democratic Alliance kilimfukuza Patricia na kumuondoa katika wadhifa wake; mara akarejea.

Mzozo umeendelea kwa miezi kadhaa huku chama kikimtuhumu kwa uzembe, kukosa uwajibikaji na rushwa, lakini mwenyewe anakanusha akisema anabaguliwa. Wanachama wengine wazungu wa chama cha Democratic Alliance wanampiga vita kama mwanasiasa mchanyiko mwenye damu ya mwafrika na mzungu. Mhariri alisema mzozo huu umewadhihirishia wazi dhahiri shahiri waafika kusini wengi kwamba chama cha Democratic Alliance si chaguo bora mdabadala la chama tawala cha ANC kama kinavyojiona, na hata kinavyojipiga debe kwenye mabango.

Mwandishi: Josephat Charo/Pressedatenbank

Mhariri: Mohammed Khelef