1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

'Shujaa wa Hotel Rwanda' kukabiliwa na miaka 25 jela

Lilian Mtono
16 Septemba 2020

Shujaa wa "Hotel Rwanda" Paul Rusesabagina huenda akakubiliwa na kifungo cha miaka 25 jela iwapo atakutwa na tuhuma zinazomkabili.

https://p.dw.com/p/3iYzO
Ruanda Paul Rusesabagina
Picha: Imago Images/Belga/M. Maeterlinck

Paul Rusesabagina aliyecheza kama shujaa katika filamu ya Hollywood kuhusiana na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994 huenda akakabiliwa an kifungo cha miaka 25 jela iwapo atakutikana na makosa kadhaa yanayomkabili hii ikiwa ni kulingana na upande wa mshitaka.

Rusesabagina,ambaye aliwahi kutoa mwito wa mapambano ya silaha dhidi ya serikali kupitia ukurasa wa YouTube alifunguliwa mashitaka katika mahakama ya mjini Kigali Jumatatu (14.09.2020) dhidi ya madai 13 ambayo ni pamoja na ugaidi na kuunda ama kujiunga na makundi mbalimbali yaliyokuwa yamejihami kwa silaha.

Msemaji wa mamlaka ya mashitaka ya Rwanda Faustin Nkusi ameliambia shirika la habari la Reauters kwa njia ya simu kwamba kwa baadhi ya makosa ya uhalifu anaweza kukabiliwa na kifungo cha miaka 25 jela na baadhi ya makosa yanaweza kuwa na adhabu kubwa zaidi ya hadi kifungo cha maisha jela.

Kesi yake imeibua ukosoaji dhidi ya serikali ya rais Paul Kagame ambayo inashutumiwa vikali na makundi ya haki za binadamu kwa ukandamizaji unaofanywa kwa wapinzani.

Ruanda | Paul Rusesabagina | Anklage erhoben
Upande wa mashitaka umesema hukumu ya Rusesabagina itakuwa ni ya haki Picha: picture-alliance/AP Photo

Upande wa mashitaka unapinga shutuma dhidi ya serikali kuhusiana na ukanzamizaji.

Nkusi anapingana na ukosoaji huo akisema upande wa mshitaka utahakikisha hukumu yake inakuwa ya haki. Alinukuliwa akisema "Hii ni kesi ya kisiasa huwezi kusaka uhuru wako wa kujieleza na haki za kisiasa kwa kuwauwa watu, kuwaibia mali zao na kuwateka."

Familia ya Rusesabagina imetoa mwito kwa mchakato huo wa kusikiliza kesi kuwa wa kimataifa huku wakiituhumu serikali kwa kumyima uwakilishi wa kisheria anaoutaka.

Nkusi na Rusesabaginawalichagua mawakili wawili waliomuwakilisha mahakamani siku ya Jumatatu na kuongeza kwamba aliruhusiwa kuzungumza na mkewe na watoto wanaoishi Marekani.

Wakati familia hiyo ikiituhumu serikali ya Rwanda kwa kumteka Rusesabagina akiwa Dubai, Nkusi alinukuliwa akisema "Alikamatwa katika ardhi ya Rwanda, katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kigali. Hiyo ndio taarifa pekee ninayoweza kuitoa. Sijui ni kwa namna gani alikuja, lakini aligundulika akiwa kwenye eneo la Rwanda na kukamatwa."

Filamu ya "Hotel Rwanda" iliyowahi kutajwa kwenye tuzo za filamu za Oscar  ilimuelezea Rusesabagina wakati huo akiwa meneja wa hoteli akitumia uhusiano wake na wasomi wa kabila ya Hutu kuwalinda Watutsi waliokuwa walijificha wakihofia kuchinjwa na Wahutu.

Mashirika: RTRE