1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya 11 Wasudan bado wako ngangari

Saumu Mwasimba
16 Aprili 2019

Wanalitaka baraza la kijeshi liunde serikali ya kiraia na kukabidhi madaraka kwa serikali hiyo baada ya kumtia kishindo rais wa zamani Omar Al Bashir kuondoka kwa nguvu madarakani

https://p.dw.com/p/3GrYm
Sudan, Khartoum: Sitzblockade vor dem Verteidigungsministerium
Picha: Getty Images/AFP/A. Mustafa

Harakati za maandamano bado zinaendelea nchini Sudan leo ikiwa ni siku ya 11 ya waandamanaji kupiga kambi nje ya makao makuu ya jeshi wakilishinikiza kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.Inaripotiwa  bado waandamanaji wameshikilia msimamo wa kulishinikiza jeshi liachie madaraka kwa utawala wa kiraia na hasa baada ya jana usiku waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kujitokeza kuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni wa nchi kukutana mjini Adis Ababa  na baraza la mpito la kijeshi linaloshikilia madaraka huko Sudan, na kuahidi kuiunga mkono nchi hiyo jirani. Kufuatia kikao hicho baadae jenerali Jalal Eldin Alshaik ambaye ni miongoni mwa wanaounda baraza hilo la mpito la kijeshi alisikika akisema kwamba baraza hilo limeyazingatia mapendekezo mengi ya waandamanaji lakini baadhi ya mapendekezo au matakwa hayo yanahitaji muda kujibiwa. Lakini juu ya hilo Jalal Eldin alisisitiza kwamba wako katika njia ya kujiandaa kuyakabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia.

Sudan Militärrat Abdel Fattah al Burhan
Picha: picture-alliance/AA

''Ningependa kusema kwamba tayari tupo kwenye mchakato wa kumtafuta waziri mkuu ili tuunde serikali ya kiraia. Kwahivyo tunayafanya hayo kabla ya kuwa na kikao na Umoja wa Afrika. Hii ndio nia yetu na hii ndio njia ya kwenda mbele kuelekea amani lakini pia tunaiheshimu na tumejitolea kufanya maamuizi ya amani na baraza la usalama.''

Pamoja na ahadi hiyo jenerali huyo  pia ameahidi kwamba waandamanaji hawatotimuliwa kuondoka nje ya makao makuu ya jeshi lakini pia kwa upande mwingine ameonekana kubadili kabisa msimamo wa baraza la kijeshi juu ya hatua ya kupelekwa katika mahakama ya jinai ya Icc mjini The Hague.

Msimamo wa jeshi kuhusu kumpeleka ICC Bashir

''Kuhusu suala la ICC kwetu sisi hili ni suali ambalo sio sehemu ya madaraka yetu. Tuko mwanzoni mwa kipindi cha mpito, endapo tutamfikisha mahakamani nchini Sudan au kumkabidhi kwa ICC ni hatua inayotakiwa kuamuliwa na serikali. Hili sio suala lililopo chini ya madaraka yetu. Linapaswa kuangaliwa na serikali itakayokuja.''

Sudan Omar Al-Bashir
Picha: Reuters/M. N. Abdallah

Baraza la kijeshi awali lilisema kwamba Bashir aliyekamatwa baada ya mapinduzi ya siku ya alhamisi wiki iliyopita hatokabidhiwa mahakama ya ICC kukabiliana na mashtaka ya uhalifu wa kivita jimboni Darfur.Muungano wa upinzani uliokuwa sehemu ya maandamano ya kumuondowa Bashir umeonekana kujipanga na kuendelea kuwa na umoja katika kutia msukumo yafanyike mabadiliko ya kisiasa nchini Sudan. Wachambuzi wa mambo nchini humo kama mwandishi habari mkongwe mwenye umri wa miaka 91 Mahjoub Mohammed Saleh anasema vyama mbali mbali vinavyounda upinzani sasa vinaelekea kuwa na umoja na kuzishughulikia tafauti zao.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri: Sekione Kitojo