1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya kimataifa ya kutokomeza manyanyaso kwa wazee

15 Juni 2023

Ulimwengu waadhimisha siku ya kuhamasisha harakati za kutokomeza manyanyaso dhidi ya wazee. La kusikitisha ni kwamba mienendo hii hushuhudiwa kuanzia ngazi ya familia ambapo wazee hudhulumiwa mali zao.

https://p.dw.com/p/4Saxy
Äthiopien Volk der Shinasha / Bworo | Yehuala Abebe
Picha: Negassa Desalegen/DW

Makaazi ya wazee ya Mapeera Kateyamba mtaa wa Nalukolongo mjini Kampala hushughulikiwa na watawa wa Kikatoliki wa jumuiya ya msamaria mwema.

Kuwepo kwa makao hayo ni kielelezo kuwa kuna wazee wasiobahatika katika jamii na wanapotelekezwa na jamaa zao hapa ndipo wanakokimbilia. Miongoni mwa wazee hao ni wale kutoka mataifa jirani waliojikuta mashakani baada ya kutengwa au kutengana na jamaa zao.Oktoba mosi: Siku ya Kimataifa ya wazee duniani

Kinyume na utamaduni na maadili ya Kiafrika, idadi ya wazee wanaojikuta katika hali hii inaongezeka. Katika makaazi haya pekee kuna wazee 75 wa kiume na kike.

Mzee aliyeishi miaka 118
Mtawa wa kikatoliki mzee aliyeishi kwa miaka 118Picha: Nicolas Tucat/AFP/Getty Images

Hali halisi ni kwamba wazee wanazidi kunyanyaswa na kudhulumiwa kuanzia ngazi ya familia ambapo mienendo ya kuwatelekeza inashuhudiwa. Miongoni mwa manyanyaso na dhuluma dhidi ya wazee ni kutukanwa, kupigwa na kuteswa kimwili ikiwemo kubakwa kwa upande wa wanawake. Aidha, baadhi hudhulumiwa mali zao kama vile ardhi na hata pesa zao.

Katika baadhi ya jamii, wazee hushambuliwa kwa madai kwamba wao ni wachawi. Haya na mengine mengi huwatia katika hali ya upweke na unyanyapaa na kwa hiyo kuteseka kimawazo. Hiki ndicho chanzo cha baadhi yao kuugua ugonjwa wa akili.

Huku idadi ya wazee ikiongezeka kwa kasi kote duniani kutokana na kuimarika kwa huduma za afya, wadau wanakumbusha kuwa kadri wazee wanavyozidi kunyanyaswa na kutelekezwa, haki zao za msingi za binadamu zinakiukwa.