1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku za mwisho za kampeni Kenya

John Juma
4 Agosti 2017

Ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Madola wanajiandaa kukutana na wadau muhimu wa uchaguzi siku ya Jumamosi. Kadhalika kuyatembelea maeneo mbalimbali kabla siku ya kupiga kura wiki ijayo

https://p.dw.com/p/2hhzQ
Kenia Wahlkampf | Raila Odinga, Opposition
Picha: Reuters/J. Keyi

Nchini Kenya kampeni za uchaguzi zinakamilika rasmi Jumamosi (05.08.2017) zitakaposalia saa 48 kabla raia kupiga kura hapo Jumanne. Wakati huo huo, waangalizi wa Jumuiya ya Madola, wanajiandaa kuungana na wadau muhimu wa uchaguzi kuanzia hiyohiyo kesho.Kwa upande, mwengine viongozi wa kidini na kijamii wanawatolea wito Wakenya kudumisha amani. Kulingana na kura za maoni kwa mara ya kwanza katika historia, uchaguzi nchini Kenya huenda ukaingia katika duru ya pili kwa sababu ya ushindani mkubwa uliopo.

Waangalizi wa Jumuiya ya Madola kukutana na wadau

Ujumbe wa waangalizi wa Jumuiya ya Madola wanajiandaa kukutana na wadau muhimu wa uchaguzi siku ya Jumamosi kadhalika kuyatembelea maeneo mbalimbali kabla siku ya kupiga kura wiki ijayo. Wajibu wao ni kushuhudia uzinduzi, mchakato wa kupiga kura kuanzia vituo vikifunguliwa hadi kura kuhesabiwa na mshindi kutangazwa.

Rais Uhuru Kenyatta anayewania urais kwa muhula wa pili akifanya kampeni Kitui
Rais Uhuru Kenyatta anayewania urais kwa muhula wa pili akifanya kampeni KituiPicha: Reuters/B. Ratner

Kikosi hiki kinaongozwa na rais wa zamani wa Ghana, Dramin Mahama, aliyekuwa madarakani kati ya mwaka 2012 na 2017. Pindi baada ya kuwasili saa chache zilizopita aliwarai wagombea wa urais kukubali matokeo na kudumisha amani baada ya Wakenya kuiamua hatima yao siku ya uchaguzi. Kauli hizo zinaungwa mkono na jopo la wazee linalowahimiza Wakenya kulinda maslahi ya nchi.

Ifahamike kuwa kiongozi wa upinzani wa NASA, Raila Odinga, na mgombea wa Jubilee, Rais Uhuru Kenyatta, wanajiandaa kila mmoja kwa mhadhara wa kilele siku ya Jumapili kukamilisha kipindi cha siku 70 za kampeni. Mihadhara hiyo imepangwa kufanyika katika Bustani ya Uhuru na Uwanja wa Nyayo hapa jijini Nairobi.

Kinyang'anyiro cha urais kuingia duru ya pili?

Kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, kura za maoni zinaashiria kuwa huenda duru ya pili ya uchaguzi ikahitajika kwa sababu ya ushindani mkubwa uliopo.

Mmoja wa viongozi wa muungano wa NASA Moses Wetangula katika bustani ya Uhuru Park
Mmoja wa viongozi wa muungano wa NASA Moses Wetangula katika bustani ya Uhuru ParkPicha: picture alliance/AA/B. Jaybee

Kwa upande mwengine, duru zinaeleza kuwa wanasiasa wa upinzani wa NASA tayari wameteua kamati maalum ya muda inayowaleta pamoja wataalamu wa masuala ya katiba na sheria, uchumi, uongozi, usalama, siasa na sera za umma.

Ifahamike kuwa kamati hii itaundwa ikiwa rais aliye madarakani hataibuka mshindi katika uchaguzi wa tarehe 8 Jumanne ijayo. Ikiwa Uhuru Kenyatta atachaguliwa kuiongoza tena Kenya, kamati haitakuwa na nafasi ya kuundwa.

Yote hayo yakiendelea, magavana watatu na wabunge watano huenda wakashindwa kushiriki kwenye uchaguzi iwapo hawatalipa faini ya jumla ya shilingi milioni 10.5 ifikapo jioni hii leo. Wagombea hao wanane walitozwa faini kwa kukiuka sheria za uchaguzi.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya

Mhariri: Mohammed Khelef