1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sissi aioya Ethiopia juu ya mzozo wake na Somalia

Lilian Mtono
22 Januari 2024

Rais Abdel Fattah el-Sissi wa Misri ameionya Ethiopia kwa kusema taifa hilo halitamruhusu yeyote kuitisha Somalia ama kuvuruga usalama wake, ikiwa kauli kali inayoashiria kusambaa kwa mzozo baina ya Somalia na Ethiopia.

https://p.dw.com/p/4bWsW
Abdel Fattah el-Sisi - Hassan Sheikh Mohamud wakutana Cairo
Rais Abdel-Fattah el-Sissi (kulia) akimkaribisha kwa heshima ya kijeshi mgeni wake, Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.Picha: Somalian Presidency/Anadolu/picture alliance

Sissi ametoa matamshi hayo siku ya Jumapili (Januari 21) katika ziara ya Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia nchini humo na kuongeza kuwa Ethiopia isiijaribu Misri wala kuwatishia ndugu zake na hasa ikiwa watawaomba kuingilia. 

Rais huyo wa Misri ametoa matamshi hayo baada ya Ethiopia kutangaza kwamba inaweza kulitambua jimbo lililojitenga la Somaliland kuwa taifa huru. 

Hii ni kufuatia makubaliano baina yao yanayoiruhusu Ethiopia kutumia bandari na kuanzisha kituo cha kibiashara na jeshi la maji katika ukanda wa pwani kwenye Ghuba ya Aden kwa miaka 50 ijayo.

Sissi, ambaye amesema Misri haitaruhusu Ethiopia "kukiuka uhuru wa ardhi ya Somalia," ameikosoa Addis Ababa juu ya namna inavyolichukulia eneo hilo lililojitenga.