1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaSomalia

Somalia yakumbwa na mafuriko makubwa

Lilian Mtono
16 Mei 2023

Umoja wa Mataifa umesema mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa za mwaka yamesababisha uharibifu mkubwa kote nchini Somalia. Kulingana na ripoti hiyo, watu 460,000 wameathiriwa na mafuriko hayo.

https://p.dw.com/p/4RRl9
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameendelea kuyahimiza mataifa kudhibiti shughuli zinazochangia mabadiliko ya hali ya hewa.
Umoja wa Mataifa mara kadhaa umekuwa ukionya kitisho kitokanacho na mabadiliko ya hali ya hewa ulimwenguni.Picha: FEISAL OMAR/REUTERS

Kulingana na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric, ripoti walizokusanya zimeangazia kuanzia uharibifu wa makazi kutokana na kufurika maji, uharibifu wa mashamba hadi kufungwa kwa vituo vya afya, huku karibu watu 219,000 wakiwa wameachwa bila makaazi. 

Soma Zaidi:Mafuriko yaacha watu 200,000 bila makazi Somalia

Karibu watu watano, ambao ni pamoja na watoto wamekufa kwenye mafuriko, amesema Mohammed Moalim wa Taasisi ya usimamizi wa majanga, alipozungumza na shirika la habari la Associated Press.

Amesema kulikuwa na uharibifu mkubwa katika mkoa wa Hiiraan, ulioko katikati ya jimbo la Hirshabelle nchini Somalia.

Familia nyingi pia ziliripotiwa kuondoka kwenye makaazi yao kwenye mji wa Beledweyne, unaokaliwa na idadi kubwa ya watu baada ya kuta za mto Shabelle unaopitia mji huo kupasuka wakati mvua kubwa zikiendelea kunyesha.

Raia wa nchini Somalia walioyahama makazi yao kutokana na ukame.
Mabadiliko ya hali ya hewa yamechangia pia hali ya ukame katika maeneo mbalimbali ulimwenguni.Picha: Hassan Ali ELMI/AFP

Mamia ya wakazi wa Beledweyne waliolazimika kukimbia wamesema iliwalazimu kufanya hivyo kutokana na kitisho kilichokuwa mbele yao.

Iman Badal Omar alisema, "Tumekabiliwa na matatizo makubwa yaliyotokana na mafuriko. Kile tulichoweza kukifanya ni kukimbia na kuwanusuru watoto wetu. Hatukuchukua chochote. Tunashukuru Mungu."

Kulingana na ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, ikiwa mvua hizo zitaendelea kunyesha nchini Somalia na kwenye maeneo ya miinuko huko Ethiopia, kuna wasiwasi wa hadi watu milioni 1.6 kuathiriwa na mafuriko na zaidi ya watu 600,000 kuyahama makazi yao, amesema Dujarric.

Kuongezeka kwa kina cha maji cha vyanzo tofauti kwenye eneo hilo kumesababisha kufungwa kwa majengo mengi muhimu, ikiwa ni pamoja na ya serikali na hospitali kubwa, hii ikiwa ni kulingana na wakaazi. Baadhi wanasema mafuriko hayo yalikuwa makubwa mno kuwahi kushuhudiwa.

Soma Zaidi:Ripoti ya mabadiliko ya hewa yasema dunia yakumbwa na kasi ya kupanda vina vya bahari duniani

Eneo la Pembe ya Afrika, ambalo ni miongoni mwa yaliyo masikini zaidi ulimwenguni linakabiliwa na mizozo mingi. Baadhi ya maeneo nchini Somalia yana ukame mkubwa, lakini pia uasi unaofanywa na makundi yenye itikadi kali yanayoipinga serikali ya shirikisho iliyoko mji mkuu, Mogadishu.

Tizama Zaidi:

Kaya 105 zaathirika na mafuriko Mtwara