1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SPD kufanya mazungumzo ya kuunda serikali na CDU

Grace Kabogo
8 Desemba 2017

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na chama chake cha Christian Democratic Union, CDU kitafanya mazungumzo ya awali ya kuunda serikali ya muungano chama cha Social Democratic, SPD, ili kuumaliza mkwamo wa kisiasa.

https://p.dw.com/p/2ozul
Combo Angela Merkel und Martin Schulz
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Afisa wa ngazi ya juu wa SPD, amesema leo kuwa mazungumzo hayo yataanza Jumatano ya wiki ijayo. Kiongozi wa chama cha SPD bungeni, Andrea Nahles amesema hakuna kingine chochote cha kufanya kwa sasa, isipokuwa kushiriki katika mazungumzo. Chama cha SPD jana kilipiga kura ili kuruhusu kufanyika kwa mazungumzo hayo ya kuangalia uwezekano wa kuunda serikali mpya ya muungano na chama cha CDU cha Kansela Merkel pamoja na chama ndugu cha Christian Social Union, CSU.

Kiasi ya wajumbe 600 wa SPD waliokuwa wakihudhuria mkutano wa mwaka wa chama hicho hapo jana, walipiga kura kwa wingi kuunga mkono hatua ya kuanza kwa mazungumzo ya awali ambayo yatasaidia kuumaliza mzozo wa kisiasa uliodumu kwa miezi kadhaa katika nchi hiyo yenye uchumi mkubwa barani Ulaya.

Katika mkutano huo, kiongozi wa SPD, Martin Schulz aliwasihi wanachama wa SPD kuzingatia maslahi ya taifa, kwa kukiunga mkono chama cha CDU na CSU, akisema kuwa muungano huo utaliimarisha bara la Ulaya.

SPD Parteitag in Berlin
Wajumbe wa SPD wakipiga kuraPicha: Reuters/F. Bensch

''Chama chenye nguvu, SPD imara ni muhimu kuifanya Ujerumani kuwa imara. Na Ujerumani imara kuifanya Ulaya kuwa imara. Tunataka kushiriki katika mazungumzo ya wazi na kuona iwapo tunaweza kufikia makubaliano makubwa. Hatuhitaji kutawala kwa gharama yoyote ile. Kilicho muhimu ni kile ambacho tunaweza kukitekeleza,'' amesema Schulz.

Kwa mujibu wa SPD, mazungumzo hayo ya wazi yanaweza kusaidia katika kupatikana kwa serikali mpya ya muungano, kukubalika kwa serikali ya wachache ya Merkel au kama mazungumzo yakishindikana, basi patakuwa na uchaguzi mpya.

Msimamo wa Schulz

Baada ya kushindwa vibaya katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba, Schulz alitangaza msimamo kwamba chama chake hakitoshiriki katika mazungumzo ya kuunda serikali mpya, na aliendelea kushikilia msimamo huo hata pale mazungumzo kati ya Merkel na chama kinachowapendelea wafanyabiashara cha Free Democratic, FDP na chama kinacholinda mazingira cha Kijani, yalipovunjika.

Hata hivyo, SPD kimeorodhesha masuala kadhaa muhimu yatakayowasilishwa katika mazungumzo hayo, ikiwemo mageuzi ya kumaliza marufuku kwa baadhi ya watu walionyimwa hifadhi kuungana tena na familia zao, malengo madhubuti ya mabadiliko ya hali ya hewa, kuondoa bima binafsi ya afya na mageuzi ya kupambana na umasiki miongoni mwa wastaafu.

Berlin Bundesparteitag der SPD
Mwenyekiti wa tawi la vijana la SPD, Kevin KuehnertPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Licha ya uamuzi huo, SPD imekumbana na pingamizi kutoka kwa upinzani na hasa tawi la vijana la SPD, linalojulikana kama Jusos. Mwenyekiti wa tawi hilo, Kevin Kuehnert amesema serikali ya muungano wa vyama vikuu ni jambo baya kwa SPD na demokrasia. Amesema matokeo ya uchaguzi wa Septemba yameonyesha kuwa hakuna mamlaka ya kuwepo muungano wa vyama vikuu.

Chama cha CDU kimeipongeza hatua hiyo ya SPD. Mmoja wa viongozi wa CDU, Klaus Schueler amesema lengo la CDU na CSU ni kuunda serikali imara na inayoaminika.

Wakati huo huo, zaidi ya asilimia 80 ya wajumbe wa SPD wamepiga kura kumchagua tena Schulz kuendelea kuwa mwenyekiti wa chama hicho. Schulz alipata asilimia 81.9 ya kura ikilinganishwa na asilimia 100 alizopata wakati alipochaguliwa mara ya kwanza mwezi Machi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, Reuters, http://bit.ly/2j60W9I
Mhariri: Caro Robi