1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sri Lanka yarefusha hali ya hatari katika jimbo la Kaskazini

Sylvia Mwehozi
14 Mei 2019

Sri Lanka imeondoa amri ya kutotembea usiku nchini kote isipokuwa katika jimbo la Kaskazini baada ya mwanaume mmoja kuuawa katika vurugu za  Jumatatu zilizofanywa dhidi ya jamii za Kiislamu.

https://p.dw.com/p/3ISmP
Sri Lanka, Colombo: Verschärfte Sicherheitsvorkehrungen nach Unruhen
Picha: Getty Images/AFP/L. Wanniarachchi

Genge la watu lilivamia na kuchoma maduka yanayomilikiwa na Waislamu, makaazi na misikiti katika ghasia za siku ya Jumatatu, ambapo polisi walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi katika maeneo kadhaa ili kutawanya umati wa watu uliokuwa na nia ya kuvamia misikiti. Waziri mkuu Ranil Wickremesinghe baadae alihutubia taifa akisema amri ya nchi nzima ya kutotembea usiku iliwekwa ili kuzuia makundi yasiyofahamika kufanya vurugu za kijamii.

"Nimevipatia vikosi vya usalama nguvu zote muhimu kuchukua hatua kali dhidi ya wale wanaovunja amani kwa kukiuka amri ya kutotembea usiku na hali ya hatari. Vikosi vya usalama vitachukua hatua zote dhidi ya wale wanaokiuka sheria. Kwa hiyo naomba ushirikiano kamili wa jeshi na polisi ili kulinda amani", alisema waziri mkuu.

Aidha ameongeza kwamba vurugu zozote zitakwamisha uchunguzi wa mashambulizi ya kigaidi ya mwezi uliopita ambayo yaliyalenga makanisa matatu na hoteli tatu za kifahari na kuwaua watu 258 huku wengine karibu 500 wakijeruhiwa.

Sri Lanka, Colombo: Verschärfte Sicherheitsvorkehrungen nach Unruhen
Afisa usalama akikagua gari katika mojawapo ya kizuizi Picha: Getty Images/AFP/L. Wanniarachchi

Soma zaidi...

Vurugu za Jumatatu pia ziliripotiwa katika jimbo la magharibi na kuilazimu serikali kuifunga mitandao ya kijamii nchi nzima. Mkuu wa jeshi la polisi Chandana Wickramaratne ameonya kuchukua hatua kali dhidi ya wale watakaofanya vurugu na kuongeza kwamba maafisa wa usalama wamepewa mamlaka ya kutumia nguvu kupita kiasi, ikiwemo kuwakamata washukiwa.

Mashambulizi ya Jumatatu yanakuja wakati jamii ya Waislamu nchini humo ikiendelea na mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Hali ya hatari ilitangazwa baada ya mashambulizi ya Aprili, ambayo kundi linalojiita Dola la Kiislamu lilidai kuhusika. Wimbi la machafuko ya karibuni lilianza wakati genge la watu lilipovamia maduka ya Waislamu katika mji wa Chilaw ulioko kilometa 80 kutoka mji mkuu wa Colombo baada ya kugadhabishwa na ujumbe uliowekwa kwenye mtandao wa Facebook na mmiliki mmoja wa duka.

Watoa huduma wa intaneti katika taifa hilo wamesema wameamrishwa kuzuia upatikanaji wa mitandao ya kijamii ya Facebook, WhatsApp, Youtube na hata Instagram katika juhudi za kuzuia kuenea kwa jumbe zinazochochea machafuko. Hali ya wasiwasi imeendelea kuwa juu tangu mashambulizi ya Jumapili ya pasaka nchini humo.

afp/ap