1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinbrück ajiuzulu

29 Septemba 2013

Mgombea aliyepambana na Angela Merkel kuwania ukansela katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani anan'gatuka katika mstari wa mbele wa siasa wakati chama chake cha SPD kikitafakari kujiunga na serikali ya mseto nchini.

https://p.dw.com/p/19q08
Peer Steinbrück wakati wa mkutano wa chama cha SPD mjini Berlin.(27.09.2013).
Peer Steinbrück wakati wa mkutano wa chama cha SPD mjini Berlin.(27.09.2013).Picha: picture-alliance/dpa

Mgombea aliyepambana na Angela Merkel kuwania ukansela katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani anan'gatuka katika mstari wa mbele wa siasa wakati chama chake cha Social Demokratik (SPD) kikitafakari iwapo kikubali kuanza mazungumzo ya kujiunga na serikali ya mseto itakayoongozwa na chama cha CDU.

Peer Steinbrück ametangaza kujiuzulu kwake huko kwa wajumbe wa mkutano maalum wa chama chake cha SPD hapo Ijumaa (27.09.2013) kujadili hatua zinazofaa kuchukuliwa na chama hicho ili kusonga mbele baada ya kushika nafasi ya pili katika uchaguzi mkuu wa Ujerumani uliofanyika tarehe 22 mwezi wa Septemba ambapo chama cha kihafidhina cha Christian Demokratic (CDU) cha Kansela Angela Merkel kiliibuka mshindi wa jumla.

Steinbrück amewaambia wafuasi wa chama chake katika mkutano huo uliofanyika Berlin "Maisha yangu ya kisiasa yatamalizika kwa mpangilio."

Mashirika ya habari pia yamemnukuu Steinbrück akisema hatotaka madaraka yoyote yale ndani ya chama au kwenye kundi la wabunge wa chama hicho cha SPD bungeni.Hata hivyo bado haiko wazi iwapo kauli yake hiyo inamaanisha kwamba atajitowa kwenye bunge la Ujerumani Bundestag.

Uchunguzi wa maoni tokea mwanzo ulionyesha kuwa Steinbrück hangeweza kushinda uchaguzi mkuu wa Ujerumani lakini alikuwa ni mtu wa kutokata tamaa kirahisi.

Sitotumika katika serikali ya Merkel

Kabla ya kushindwa kwake katika uchaguzi huo,alisema iwapo atashindwa hatashika wadhifa wowote ule katika serikali ya mseto kwa kushirikiana na Kansela Merkel. Wakati huo Peer Steinbrück alitupilia mbali mipango ya kuundwa kwa serikali ya muungano mkuu kwa kusema kwamba hatoshiriki katika serikali ya mseto na chama cha CDU cha Merkel.

Mgombea wa Ukansela wa SPD Peer Steinbrück wakati wa kampeni za uchaguzi mjini Berlin.(19.09.2013).
Mgombea wa Ukansela wa SPD Peer Steinbrück wakati wa kampeni za uchaguzi mjini Berlin.(19.09.2013).Picha: picture-alliance/dpa

Kwa upande mwingine alisisitiza kwamba ni muhimu kwa vyama vya kidemokrasia kuwa tayari kujiunga na vingine kuunda serikali.Chama chake cha SPD kilikuwa kikipigania tokea mwanzo wa kampeni yake kuunda serikali ya mseto na chama cha watetezi wa mazingira cha Kijani.

Mhitimu huyo mwenye shahada ya uchumi ambaye ana umri wa miaka 66 alikuwa akipuuza uchunguzi wa maoni wenye kuonyesha matokeo mabaya katika juhudi zake za kuwania ukansela.Lakini aliendelea tu kufanya kampeni licha ya kulaumiwa kwa makosa, kuboronga na kuwa nyuma kwenye matokeo ya uchunguzi huo wa maoni.

Mchumi huyo alijipatia heshima wakati alipokuwa waziri wa fedha kwenye serikali ya mseto ya Merkel mwaka 2005 hadi 2009.Lakini makosa na kuboronga kwake kulichafua kampeni yake ikiwa ni pamoja na kupiga picha iliotolewa kwenye ukurasa wa mbele wa jarida akiwa ameonyesha kidole cha kati.

Alikuwa akiboronga

Pia alikuja kushutumiwa kwa kudharau bei ya wastani ya mvinyo "Pinot Grigio" kuwa ni bei ya chini na kileo hicho kinastahiki kunywiwa na walala hoi na sio mtu kama yeye mwenye nacho.Sio hayo tu,alikuja kuuponda mshahara wa kansela kuwa sio mkubwa na umezidi kidogo tu ule wanaolipwa mameneja wa mabenki.Alikuwa sio mtu wa kukataa tamaa na mapema na alionyesha kukubali kushindwa sio chaguo.

Peer Steinbrück akiwa katika mojawapo ya kile kinachotajwa kuwa kuboronga kwake.
Peer Steinbrück akiwa katika mojawapo ya kile kinachotajwa kuwa kuboronga kwake.Picha: Alfred Steffen/SZ-Magazin/dpa

Tamko la kujiuzulu kwa Steinbrück linakuja wakati chama chake cha SPD kikitafakari uwezekano wa kujiunga katika serikali ya mseto chini ya uongozi wa Kansela Merkel.Licha kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi, Merkel anahitaji kuunda serikali ya mseto na chama cha SPD au cha Kijani ili kuwa na wingi wa viti bungeni kuweza kuongoza serikali.

Tuko tayari kwa mazungumzo

Kiongozi wa SPD Sigmar Gabriel amesema kufuatia mkutano huo wa uongozi wa chama kwamba wako tayari kwa mazungumzo.Amekaririwa akisema " Tutafanya mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto ambayo yatahitimishwa kwa kura za wanachama wetu na matokeo yake yatatekelezwa na SPD.Hatutoingia mazungumzo hayo moja kwa moja na azma ya kujiunga na serikali lakini pia hatutoogopa kujiunga na serikali.Tunaingia mazungumzo haya kwa kujiamini."

Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel katika mkutano maalum wa chama mjini Berlin.(27.09.2013 ).
Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel katika mkutano maalum wa chama mjini Berlin.(27.09.2013 ).Picha: picture-alliance/dpa

Licha ya kukubali kuingia katika mazungumzo hayo wanachama wengi wa SPD bado wanaandamwa na na jinamizi la kumbukumbu mbaya wakati walipokuwa katika serikali ya mseto na Merkel wakati wa muhula wake wa kwanza hapo mwaka 2005 hadi mwaka 2009.

Wafuasi wao walikihama chama hicho kwa wingi kwa kukiadhibu kwa matokeo mabaya ya uchaguzi kuwahi kuyashuhudia na kusababisha wanachama wengi wa chama hicho kuwa na wasi wasi kukubali kujiunga na serikali yoyote ile mpya ya mseto.

Kabla ya mkutano huo wa faragha wa takriban wanachama 200, naibu kiongozi wa chama cha SPD Johannes Kahrs alisema chama hicho kisikubali kujiunga na serikali ya mseto bila ya kukubaliana kugawana madaraka kwa asilimia hamsini kwa hamsini. Madai ya SPD ni pamoja na kuwepo kwa kiwango cha chini cha mishahara, usawa kwa mashoga,kikomo cha kodi na utaratibu mkali wa mikataba ya kazi za kujishikiza na ile ya muda mfupi.

Juu ya kwamba asilimia 64 ya wajumbe wa SPD katika mkutano huo wameunga mkono kuundwa kwa serikali ya muungano mkuu kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni wa kituo cha televisheni cha ZDF uchunguzi tafauti wa maoni uliofanywa na Forsa umeonyesha takriban theluthi tatu ya wanachama wa SPD wanapinga serikali hiyo.

Mazungumzo yatakuwa magumu

Gazeti lilitolewalo kila siku la Tagesspiegel hapo Ijumaa lilikuwa na kigaragosi cha Merkel akimithilishwa na paka mwenye njaa akiiashiria SPD itoke nje ya tundu lake la panya.

Bendera za chama cha CDU na SPD zikipepea bega kwa bega mwaka 2005.
Bendera za chama cha CDU na SPD zikipepea bega kwa bega mwaka 2005.Picha: dpa

Alikuwa akitowa mkoromo wa tamko la "Toka nje!Fikiria juu ya wajibu wako wa kiraia kwa taifa."

Nalo gazeti mashuhuri la kila siku la Bild limeonya kwamba mazungumzo kati ya mahasimu hao wa jadi yatakuwa marefu na magumu kabisa katika historia ya Jamhuri ya Ujerumani.

Mwandishi: Mohamed Dahman/DW/AFP

Mhariri :Caro Robi