1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier azuru Burkina Faso

12 Februari 2008
https://p.dw.com/p/D6PS

Naibu kansela wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, amewasili nchini Burkina Faso leo ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake barani Afrika.

Kiongozi huyo amewasili mjini Oaugadougou akitokea nchini Togo.

Akiwa nchini Togo waziri Steinmeier ametoa mwito Togo ifutiwe deni lake ili kuisadia katika juhudi zake za kuleta mageuzi ya kidemokrasia.

Togo ilifanya uchaguzi wa vyama vingi mnamo mwaka jana.

Katika matamshi aliyoyatoa wakati alipokutana na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na rais wa Togo, Faure Gnassingbe, Frank Walter Steinmeier, ambaye pia ni waziri wa mashauri ya kigeni wa Ujerumani, ameahidi kwamba nchi yake itaisaidia Togo.

Aidha kiongozi huyo amesema kwa kuwa Togo inaendeleza demokrasia, jumuiya ya kimataifa inaweza pia kusaidia kuiimarisha.

Steinmeier ni afisa wa ngazi ya juu wa Ujerumani kuitembelea Togo katika kipindi cha miaka 15. Togo ilikuwa zamani koloni ya Ufaransa lakini pia ilitawaliwa na Ujerumani kati ya mwaka wa 1894 na 1914.

Umoja wa Ulaya ulianzisha tena ushirikiano wa kiuchumi na Togo mwezi Novemba mwaka janabaada ya kuusitisha kwa miaka 15.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Togo kufanya uchaguzi wa vyama vingi mwezi Oktoba mwaka jana, mojawapo ya masharti yaliyowekwa na Umoja wa Ulaya kabla kurudisha ushirikiano na kuipelekea misaada nchi hiyo iliyositishwa mwaka wa 1993 kwa kile ambacho umoja huo ilikiita historia mbaya ya demokrasia nchini Togo.