1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier ziarani Iraq

16 Agosti 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani amekutana na uongozi wa Iraq siku moja baada ya Umoja wa Ulaya kukubali kuvipatia silaha vikosi vya Wakurdi vinavyopambana na kundi la waasi la Dola la Kiislamu.

https://p.dw.com/p/1Cvlg
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Waziri Mkuu mteule wa Iraq Haidar al-Abadi mjini Baghdad. (16.08.2014)
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier akiwa na Waziri Mkuu mteule wa Iraq Haidar al-Abadi mjini Baghdad. (16.08.2014)Picha: picture-alliance/dpa

Baada ya kuwasili katika mji mkuu wa Baghdad Jumamosi (16.08.2014) Steinmeier amekaririwa akisema taswira za kila siku za mauaji yanayofanyika Iraq zimeifadhaisha na kuichukiza dunia nzima.

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani yuko Iraq kutathmini hali ilivyo nchini humo ambapo anatazamiwa kujadili masuala ya kisiasa na usalama halikadhalika njia za kuwasaidia wakimbizi na uongozi wa Iraq.

Ameongeza kusema "Tunahofia kwamba nguzo ya mwisho ya utengamano nchini Iraq inaweza kuanguka".

Katika ziara yake hiyo amekutana na Rais Fouad Massoum wa Iraq na waziri mkuu mteule Haider al- Abadi ambaye amepewa jukumu la kuunda serikali mpya na Rais Massoum baada ya waziri mkuu anayeondoka madarakani Nuri al-Maliki kuachana na nia yake ya kuwania uongozi huo kwa muhula wa tatu.

Mwanga wa matumaini?

Amesema hatua zinazochukuliwa sasa nchini Iraq kuunda serikali mpya ya mseto kufuatia kujiuzulu kwa Waziri Mkuu Nuri al-Maliki kumetowa "mwanga wa matumaini".

Steinmeier amesema uongozi wa al-Abadi ambaye ameahidi kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kukabiliana na uasi unaozidi kukuwa wa Waislamu wa itikadi kali unawekewa matumaini makubwa.

Waziri Mkuu mteule wa Iraq Haider al-Abadi.
Waziri Mkuu mteule wa Iraq Haider al-Abadi.Picha: picture alliance / AP Photo

Kwa mujibu wa waziri huyo wa Ujerumani hiyo ni njia pekee ya kuondowa hali ya kutoridhika iliyotanda nchini kote Iraq ambayo ilikuwa ikichochea kuungwa mkono kwa wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu (IS) hali ya uasi aliyoielezea kwa ni ya " balaa " ambapo kwayo "kundi la kigaidi la wauwaji lilikuwa likijaribu kuidhibiti nchi hiyo."

Kujiuzulu kwa Maliki hapo Alhamisi kumeondowa mkwamo wa kisiasa nchini Iraq.Kiongozi huyo alikuwa akishutumiwa kwa kuwabaguwa watu wa madhehebu ya Sunini nchini Iraq na hiyo kusababisha kuzidi kuungwa mkono kwa waasi wa kundi la Dola la Kiislamu ambao pia wanatoka kwenye madhehebu ya Sunni ya dini ya Kiislamu.

Al- Abadi amesema anakusudia kuanzisha sera zenye kukuza umoja wa kitaifa.

Kuwapa silaha Wakurdi

Steinmeier pia amepangiwa kwenda Erbil mji mkuu wa eneo lenye mamlaka ya ndani la Wakurdi ambapo atakutana na Rais Masssud Barzani kwa mzungumzo juu ya jinsi Ujerumani inavyoweza kusaidia katika kupambana na wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu (IS) na kutowa msaada kwa maelfu ya wakimbizi nchini humo.

Ziara hiyo ya waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani inakuja muda mfupi baada ya ndege ya kwanza ya uchukuzi ya Ujerumani yenye kubeba misaada kwa watu waliopotezewa makaazi kutokana na mashambulizi ya kundi la Dola la Kiislamu kutuwa huko Arbil.

Kutokana na jeshi la Iraq kuwa katika hali ya mchafukoge vikosi vya Wakurdi vilivyopatiwa mafunzo mazuri vinawekewa matumaini makubwa ya kuwazuwiya wanamgambo wa Dola la Kiislamu ambao wamekuwa wakiyatanuwa maeneo wanayoyadhibiti bila ya upinzani mkubwa.

Mpiganaji wa kikosi cha Wakurdi cha Peschmerga.
Mpiganaji wa kikosi cha Wakurdi cha Peschmerga.Picha: Ahmad Al-Rubaye/AFP/Getty Images

Kusonga mbele hivi karibuni kwa kundi hilo kuelekea kwenye eneo la Wakurdi la Kurdistan kumesababisha maelfu ya watu wa jamii ya Wazidi na Wakristo kuyakimbia makaazi yao.

Tokea mwezi wa Juni sehemu kubwa zenye utajiri wa mafuta mashariki mwa Syria na kaskazini magharibi mwa Iraq zimetekwa na kundi hilo na kuzusha hofu kimataifa ya kuibuka kwa kanda itakayokuwa chini ya mamlaka ya wanamgambo hao katika eneo hilo.

Uingiliaji kati kimataifa

Marekani ambayo ilianzisha mashambulizi ya anga dhidi ya wanamgambo hapo Juni nane imesema imefanya mashambulizi zaidi hapo Ijumaa baada ya kupata taarifa kwamba magaidi wa kundi hilo la Dola la Kiislamu walikuwa wakiwashambulia raia.

Mashambulizi ya anga ya Marekani ni ya kwanza tokea vikosi vya Marekani viondolewe kutoka Iraq hapo mwaka 2011. Hata hivo Rais Barack Obama wa Marekani ameondowa uwezekano wa kutuma tena vikosi vya Marekani kwenda kupigana nchini Iraq.

Katika hatua nyengine ya kimataifa kupambana na kusonga mbele kwa kundi hilo la Dola la Kiislamu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hapo Ijumaa limepitisha azimio lenye kuzuwiya kugharimiwa kifedha kwa kundi hilo na kujiunga kwa wapiganaji wa kigeni na kundi hilo.

Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power wakati wa kikao cha Baraza la Usalama New York. (15.08.2014)
Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Samantha Power wakati wa kikao cha Baraza la Usalama New York. (15.08.2014)Picha: Reuters

Azimio hilo lililorasimiwa na Uingereza limewaweka viongozi sita Waislamu wa itikadi kali kutoka Kuwait,Saudi Arabia na mataifa mengine kwenye orodha ya vikwazo vyenye marufuku za safari na kuzuwiya mali zao.

Mwaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya nao wamekubaliana katika mkutano wao mjini Brussels kuunga mkono kupatiwa silaha kwa wapiganaji wa Kikurdi nchini Iraq.Wiki iliopita wanamgambo wa kundi la Dola la Kiislamu waliusogelea mji mkuu wa Irbil na kuwa umbali wa kilomita 35 tu kabla ya kurudishwa nyuma na mashambulizi ya anga.

Mwandishi : Mohamed Dahman/dpa/Reuters/AFP

Mhariri : Bruce Amani