1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Steinmeier ziarani mashariki mwa Afrika

Mohammed Khelef19 Februari 2015

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier anaanza leo ziara ya siku nne barani Afrika kwa mazungumzo na Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo mjini Kinshasa.

https://p.dw.com/p/1EeQs
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier.Picha: picture-alliance/dpa/Bernd von Jutrczenka

Pamoja na kukutana na Rais Kabila, Waziri Steinmeier atakuwa pia na mazungumzo na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa mashariki mwa Kongo, Martin Kobler, juu ya operesheni za Umoja huo.

Kongo inayokaliwa na zaidi ya raia milioni 70 imekuwa ikikabiliwa na mapigano ya muda mrefu ya wenyewe kwa wenyewe, hasa kwenye upande wa mashariki unakopatikana pia utajiri mkubwa wa madini. Umoja wa Mataifa una wanajeshi wake wapatao 20,000 kwenye eneo hilo katika kile kinachoitwa kampeni ya kulinda amani, ikiwa ni idadi kubwa kabisa ya vikosi vya Umoja huo kuwahi kutumwa kwenye operesheni moja.

Waziri Steinmeier anawasili mjini Kinshasa ikiwa ni chini ya mwezi mmoja tangu Rais Kabila kujaribu kubadilisha katiba ili apate muhula mwengine madarakani, hatua ambayo ilipingwa vikali na wananchi kupitia maandamano. Serikali ya Kabila ilijibu maandamano hayo kwa kutuma vikosi vyake, kukata mawasiliano ya simu za mkononi na hata kuwakamata waandamanaji. Watu kadhaa pia waliripotiwa kupoteza maisha.

Ziara hii ya Waziri Steinmeier, ambayo inajumuisha ujumbe wa wafanyabiashara na pia masuala ya utamaduni, itamchukuwa pia hadi Rwanda na Kenya, mataifa yanayokabiliwa na changamoto tafauti licha ya kuwa yote ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: AFP/Getty Images/A. Wandimoyi

Taswira ya Kenya, Rwanda kimataifa

Kwa upande wake, Kenya imekuwa kwa miaka mingi kituo kikuu cha utalii, lakini kwa siku za karibuni wimbi la ugaidi wa kundi la al-Shabaab umekuwa ukitanda taswira ya taifa hilo katika jumuiya ya kimataifa.

Kampeni ya Kenya kupambana na siasa kali ndani ya ardhi yake, imekuwa ikikosolewa kuvunja haki za binaadamu, hasa jamii ya Waislamu wenye asili ya Somalia. Rwanda nayo inapiga hatua za taratibu kujijenga upya miongo takribani miwili baada ya mauaji ya maangamizi, licha ya kuwa na utawala unaolaumiwa kukiuka haki za binaadamu.

"Matatizo ya haki za binaadamu ni mambo ya kila siku, ila tunapoutazama uhusiano wa Ujerumani na China na Saudia Arabia, kwa mfano, tunajuwa kuwa suala la haki za binaadamu si kiini cha ushirikiano, na vivyo kwa Afrika suala hilo si la mwanzo bali la mwanzo kabisa ni utulivu wa kisiasa," anasema Profesa Robert Kappel wa Taasisi ya Taaluma za Kimataifa ya Hamburg, Ujerumani.

Ziara ya waziri huyo wa mambo ya nje wa Ujerumani kwenye eneo hilo la mashariki ya Afrika, inakuja wiki mbili tu tangu Rais Joachim Gauck wa Ujerumani kumaliza ziara yake nchini Tanzania, taifa lenye ushawishi mkubwa kwenye ukanda huo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman