1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Strauss-Kahn na tuhuma mpya za kubaka

5 Julai 2011

Aliyekuwa Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa -IMF- Dominique Strauss-Kahn anakabiliwa na mashtaka mengine mapya ya kujaribu kumbaka, mwandishi wa habari wa Kifaransa, Tristane Banon.

https://p.dw.com/p/11p1W
Dominique Strauss-KahnPicha: dapd

Wakili wa mwanamke huyo, David Koubbi amesema mashtaka hayo yatakayofunguliwa na mteja wake yanahusiana na tukio lililotokea wakati Tristane Banon, alipokwenda kufanya mahojiano na Dominique Strauss-Kahn waziri wa zamani wa fedha wa Ufaransa, zaidi ya miaka minane iliyopita, mjini Paris.

Amesema mteja wake huyo, mwenye umri wa miaka 32, atafungua mashtaka leo mjini Paris, ya njama ya kubakwa.

Hata hivyo wakili huyo wa Banon hakusema kama muda alioupangilia mteja wake kufungua mashtaka hayo unatokana na mwenendo wa kesi nyingine inayomkabili Mkurugenzi huyo mtendaji wa zamani wa Shirika la Fedha la Kimataifa IMF, iliyofunguliwa mjini New York, Marekani kwa tuhuma zilizofanana na hizo za kujaribu kumbaka mhudumu wa hoteli.

Amekanusha taarifa pia kwamba uamuzi wa kuendelea na mashtaka hayo sasa hivi ni kutokana na hamasa za kisiasa.

Strauss Khan aliachiliwa kutoka katika kizuizi cha nyumbani mjini New York, Ijumaa iliyopita, baada ya waendesha mashtaka kusema kwamba wanatilia shaka madai ya mhudumu huyo wa hoteli, mzaliwa wa Guinea.

Katika wiki za hivi karibuni wakili wa Tristane Banon, David Koubbi alikuwa akisema mara kadhaa kwamba mteja wake anazingatia kuchukua hatua dhidi ya Strauss-Kahn, juu ya tukio hilo la ubakaji, ambalo alisema lilitokea mwanzoni mwa mwaka 2003.

Maelezo ambayo yamepishana na ya mama wa Banon, Anne Mansouret, mwanasiasa wa Kisoshialisti ambaye awali alisema tukio hilo limetokea mwaka 2002.

Awali mama huyo alithibitisha pia kwamba alimshauri binti yake kutofungua mashtaka wakati ule, kwa kuhofia kuwa hatua hiyo ingeathiri kazi yake ya Uandishi habari.

Mkuu wa chama cha Kisoshialisti cha Ufaransa Francois Hollande ambaye awali alidaiwa na Banon kufahamu shutuma hizo, Mei 20 mwaka huu alikanusha kutojua chochote juu ya jambo hilo.

Kulingana na sheria za Ufaransa, mashtaka ya kujaribu kubaka yanaweza kusikilizwa hadi miaka 10, baada ya kutokea kwa shambulio hilo.

Alipoalikwa kushiriki katika kipindi kimoja cha mazungumzo katika kituo kimoja cha televisheni nchini Ufaransa, Februari mwaka 2007, Banon alielezea jinsi mwanasiasa mmoja wa ngazi za juu, miaka michache iliyopita, alivyomshawishi kukutana naye katika nyumba iliyokuwa tupu, kwa lengo la kufanya naye mahojiano, lakini badala yake akataka kumbaka.

Kwa upande wao, mawakili wa Aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Fedha la Kimataifa, Dominique Strauss-Kahn wanasema mteja wao ana mipango ya kumshtaki mahakamani mwanamke huyo wa Kifaransa kwa kumkashifu.

Mawakili hao, Henri Leclerc na Frederique Baulieu wamesema wako katika utaratibu wa kuandaa mashtaka dhidi ya mwanamke huyo. 

Mwandishi: Halima Nyanza(afp, reuters)

Mhariri: Hamidsou Oummilkheir