1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Subira yaleta kheri

Oumilkher Hamidou16 Novemba 2010

Mkakati wa ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na Umoja wa Afrika,miaka mitatu baada ya kutiwa saini-viongozi wanatazamiwa kukutana wiki ijayo mjini Tripoli

https://p.dw.com/p/QABh
Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya uliofanyika Sharm El Sheikh nchini Misri december 5 mwaka 2007,kabla ya mkutano wa kilele wa pande hizo mbili December 7 hadi 8 mwaka huo huo mjini LisbonPicha: AP

Mataifa ya Afrika na Ulaya yalikubaliana miaka mitatu iliyopita mkakati wa pamoja ili kusimamia na kuimarisha uhusiano wao. Ili kujiandaa kwa ajili ya mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya na Afrika utakaofanyika wiki ijayo mjini Tripoli-Libya, wataalam na wawakilishi wa mashirika ya maendeleo wamekutana jana mjini Berlin kutathmini yaliyoweza kufikiwa hadi sasa.

Ilidhamiriwa kuwa mwanzo mwema pale viongozi wa mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya na wenzao 54 wa Afrika walipokutana mjini Lisbon mnamo mwaka 2007 .Viongozi wa mataifa na serikali wa Umoja wa Afrika na Umoja wa Ulaya waliamua mnamo siku za mbele uhusiano wao uwe sawia na kubuni mkakati wa pamoja.Lengo lilikuwa kufikia hatimae ushirikiano wa haki unaozihusu sekta zote.

Philipp Darmuzey, mkuu wa idara ya halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya inayoshughulikia masuala ya Afrika, anahisi hili ni jambo bora na hasa katika sekta ya usalama na masuala ya amani.

"Ni uhusiano ambao daima umekuwa ukiangaliwa kuwa maalum miongoni mwa mikakati ya pamoja ya Afrika na Ulaya. Katika uhusiano huu kulikuwa na shinikizo kubwa na masilahi ya kila upande, lakini pia hamu ya kutaka kushirikiana."Anasema Philipp Darmuzey aliyesifu ushirikiano kati ya taasisi za usalama za Afrika na zile za umoja wa Ulaya.

Wanachama wake hukutana kila kwa mara na kuzungumzia kwa njia ya uwazi na ya usawa masuala tofauti ikiwa ni pamoja na afya na ulinzi wa mazingira.

Afrika na Ulaya zinajongeleana kwa upande wa taasisi zake. Lakini utaratibu huo wakaazi wa maeneo haya mawili bado hawajaona matunda yake, anasema bibi Christa Randzio-Plath-ambae ni mwenyekiti wa shirikisho la mashirika ya misaada ya maendeleo ya Ujerumani-Venro.

Maoni kama hayo yametolewa pia na mbunge wa kutoka Namibia, Peter Katjavivi, anaethibitisha hata nchini mwake matunda ya mkakati huu mpya wa ushirikiano bado hayajachomoza. Anautaja mkakati huo kuwa ni changamoto kubwa kuwa kuwafafanuliwa wananchi. Bwana Peter Katjavivi anakiri, hata hivyo, jambo la maana kama hili linahitaji muda hadi kuanza kutoa matunda.

Hadi wakati huu serikali hazikufanya mengi ili kuyajumuisha mashirika ya huduma za jamii katika mkakati huo wa ushirikiano. Mwenyekiti wa shirikisho la mashirika ya misaada ya maendeleo ya Ujerumani-Venro- bibi Christa Randzio Plath, anataraji mkutano wa kilele wa wiki mijayo mjini Tripoli Libya utapitisha maamuzi kuhusu namna ya kuimarishwa ushirikiano katika sekta ya mazingira na kujiandaa kuelekea mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa.

Mwandishi: Kiesel Heiner/Hamidou Oummilkheir/ZR

Mpitiaji: Miraji Othman