1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sehemu ndogo ya chakula inawafikia walengwa

Mjahida14 Januari 2016

Tume ya uangalizi wa mpango wa amani Sudan Kusini imeonya nchi hiyo inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibidaadamu, huku ikisema sehemu ndogo tu ya msaada wa chakula inafika mahali unapohitajika.

https://p.dw.com/p/1Hcwz
Südsudan Mehr als 30.000 Menschen laut UNO vom Hungertod bedroht
Baadhi ya watoto na wazazi wao Sudan KusiniPicha: Getty Images/AFP/N. Sobecki

Mapigano yaliyoikumba nchi hiyo tangu Mwezi Desemba mwaka 2013, imezuwiya kilimo na kusababisha uhaba wa chakula, alisema mwenyekiti wa operesheni ya pamoja ya tume ya ufuatiliaji na tathmini (JMEC) Festus Mogae. Tume hiyo imeundwa kwa uungwaji mkono wa shirika la maendeleo katika pembe ya Afrika IGAD lililoongoza mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan Kusini na waasi.

Akiwa katika mji mkuu wa Juba, Mogae amesema vizuizi katika magari ya misaada na ukosefu wa usalama, yanatatiza zoezi la kupeleka chakula cha msaada katika maeneo ya Bahr el Ghazal na mikoa ya Upper Nile Magharibi na Kaskazini mwa nchi hiyo.

Hata hivyo mashirika yanayotoa misaada yamekuwa yakiishutumu serikali kuzuwiya usafirishwaji wa misaada hiyo huku serikali ikiyashutumu mashirika hayo kwa kuwaunga mkono waasi. Usafirishwaji wa Misaada pia imeathiriwa na kitisho cha mapigano na wizi.

Kiongozi wa waasi Riek Machar na rais wa Sudan Kusini Salva Kiir
Kiongozi wa waasi Riek Machar na rais wa Sudan Kusini Salva KiirPicha: picture-alliance/AP Photo/P. Muller

Sudan Kusini Mogae amesema tani 75,000 za chakula cha msaada zitahitajika katika miezi mitatu ijayo lakini kwa sasa ni tani 5000 tu za chakula zinazosafirishwa kwa mwezi.

Aidha wiki iliyopita serikali ya Salva Kiir na waasi wanaoongozwa na makabu wa zamani wa rais Riek Machar walikubaliana juu ya kuundwa kwa serikali ya Umoja wa kitaifa.

Pande hizo mbili zilitia saini makubaliano hayo mwezi Agosti lakini licha ya hayo bado mapigano yanaendelea kuripotiwa Kaskazini na Kusini mwa Sudan Kusini. Kulingana na Umoja wa Mataifa takriban watu milioni 4 ambao ni nusu ya idadi ya watu nchini humo hawakuweza kupata chakula mwezi Septemba.

Zaidi ya watu milioni 2 waachwa bila maakazi kufuatia mapigano

Mzozo wa Sudan Kusini uliyoanza baada ya Kirr na Machar kuanza kungangania madaraka umesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kuwaacha wengine zaidi ya milioni mbili bila makaazi.

Huku hayo yakiarifiwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwashughulikia watoto UNICEF limesema watoto milioni 24 wanaoishi katika maeneo ya mizozo au mtoto mmoja kati ya wanne hawapo mashuleni wakiwemo nusu ya watoto wa Sudan Kusini.

Südsudan Mehr als 30.000 Menschen laut UNO vom Hungertod bedroht
Mwanamke wa Sudan Kusini akiwa pamoja na wanawe katika jimbo la UnityPicha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Shirika hilo limesema robo ya watoto hao waliyo kati ya miaka sita na kumi na tano wanaoishi katika mataifa 22 yanayokumbwa na mizozo wanakosa masomo yao hatua itakayowaathiri baadaye kwa kuwanyima nafasi ya maendeleo siku za usoni.

Hali ni ya wasiwasi mno nchini Sudan kusini kufuatia asilimia 51 ya watoto kukosa masomo kufuatia mapigano ya mara kwa mara yanyoendelea katika taifa hilo changa kabisa duniani.

Mwandishi: Amina Abubakar dpa

Mhariri: Yusuf Saumu