1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sudan yaahidi kumaliza mabishano, kuhusiana na mji wake wa Abyei, wenye utajiri wa mafuta.

Nyanza, Halima6 Juni 2008

Viongozi kutoka kaskazini na kusini mwa Sudan wamefikia makubaliano ya kumaliza tofauti zao, kugombea mji wenye utajiri wa mafuta wa Abyei, tofauti ambazo ziliongeza hofu ya kuzuka tena kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

https://p.dw.com/p/EEck
Rais Hassan Omar al-Bashir wa Sudan, ameelezea makubaliano ya kumaliza tofauti kati ya Kusini na Kaskazini kuhusiana na mji wa Abyei.Picha: AP Photo

Rais Omar Hassan Al Bashir wa Sudan, amewaambia Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wanaoitembelea nchi hiyo kwamba mabishano kati ya serikali ya kaskazini na waasi wa zamani wa kusini mwa nchi hiyo, kuhusu mkoa wenye utajiri wa mafuta wa Abyei utamalizwa wiki ijayo.

Aliwahakikishia wajumbe hao kuwa pande zote mbili zinafanyia kazi kwa karibu suala hilo, na kwamba karibuni watalimaliza kupitia mashauriano kati ya pande hizo mbili.

Hata hivyo, Maafisa wa serikali ya kusini wametahadharisha kuwa masuala muhimu bado yanahitaji kuamuliwa.

Wajumbe hao wa serikali ya Sudan ya kusini walikutana na wenzao wa kaskazini mjini Khartoum, kwa ajili ya kutoa maelezo kamili kuhusiana na makubaliano hayo ya Abyei.

Licha ya kuwepo kwa wawakilishi hao wa serikali ya Sudan ya kusini, wanadiplomasia wamemuelezea Rais wa Sudan ya kusini Salva Kiir kwamba ni mtu aseyependa kutoka katika mji mkuu wa serikali hiyo, Juba.

Bwana Kiir ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa serikali ya mseto ya Sudan ni mmoja wa waanzilishi wa mpango wa amani wa mwaka 2005, uliopelekea kumalizwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya eneo la kaskazini na kusini nchini humo, vilivyodumu kwa zaidi ya miongo miwili.

Naye Balozi wa Afrika kusini katika Umoja wa Mataifa, akizungumza, baada ya kukutana na Rais Bashir, amesema amewajulisha kuwa muswada huo wa makubaliano unatarajiwa kuwasilishwa leo katika bunge la kusini na endapo utaridhiwa utaanza kutekelezwa June 10.

Mapigano makali kati ya majeshi ya kaskazini na kusini mwa Sudan katika eneo hilo la Abyei yalisababisha vifo vya zaidi ya wanajeshi 20 na kulazimisha watu wengine maelfu kukimbia nyumba zao.

Wachambuzi wa Mambo walionya kuwa hali hiyo ikiendelea inaweza kusababisha kuanza tena kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Eneo hilo la mafuta lililopo Abyei linadhibiti sehemu kubwa ya utajiri wa mafuta nchini Sudan.

Mkoa huo pia unazunguukwa na eneo la visima vya mafuta vyenye utajiri mkubwa pamoja na bomba la mafuta ambalo watafiti wanasema linabeba karibu nusu ya mapima laki tano ya Sudan ya uzalishaji kwa siku.

Bado haijaeleweka wazi iwapo viongozi hao wa kaskazini na kusini wamefikia makubaliano kuhusu mipaka na utawala wa Abyei au katika kuondoa vikosi vya jeshi vya pande zote mbili ambavyo vilikuwa vimerundikana ndani na kuzunguuka mji huo.

Katika hatua nyingine Serikali ya Sudan, imezuia kampuni zote za Marekani kufanya biashara na Jeshi la Pamoja la Kulinda amani la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika lililopo Darfur, kutokana na Marekani kuiwekea vikwazo nchi hiyo.

Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, Abdalmahmood Abdalhaleem Mohamed amesema mkataba wa miezi sita wa dola milioni 250, kwa kampuni moja ya Kimarekani, kujenga vituo vitano vipya katika jimbo la Darfur, kwa ajili ya kikosi hicho cha kulinda amani, hautaongezewa muda.

Aidha amesema, watapokea kampuni yoyote duniani ambayo haijaweka vikwazo dhidi ya Sudan, kufanya kazi hiyo.