1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Syria yaandamwa na vikwazo vipya

Mohamed Dahman22 Juni 2011

Mataifa ya Umoja wa Ulaya yametanuwa vikwazo vyake dhidi ya Syria kuhusisha kampuni nne za kijeshi na watu zaidi wanaohusika na ukandamizaji wa maandamano ya kupinga serikali ya nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/11hOD
Rais Bashar al Assad wa SyriaPicha: dapd/Syrian TV

Mwandiplomasia wa Umoja wa Ulaya amesema Uingereza na Ufaransa zimeandaa orodha yenye kupendekeza kuongeza watu binafsi kadhaa na vyombo miongoni mwa wale ambao tayari wanalengwa na vikwazo vya Umoja wa Ulaya vya kuzuwiya mali zao na marufuku ya visa.

Syrien Demonstrationen
Wakimbizi wa Syria waliokimbia UturukiPicha: dapd

Orodha ya Uingereza pia imependekeza vikwazo dhidi ya wananchi wawili wa Iran waliohusika katika kuwapatia zana na kuunga mkono ukandamizaji wa upinzani nchini Syria lakini nchi moja kati ya nchi wanachama 27 wa Umoja wa Ulaya bado haikuudhinisha vikwazo hivyo.

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia mmoja orodha ya Ufaransa imeidhinishwa kikamilifu, lakini nchi moja imesita kuidhinisha orodha ya vikwazo ya Uingereza.

Orodha kamili itaidhinishwa leo hii iwapo hakutakuwepo pingamzi rasmi. Mwanadiplomasia huyo amekataa kuzitaja kampuni au watu watakaowekewa vikwazo lakini amesema hawako katika ulimwengu wa shughuli za uzalishaji wa mafuta nchini Syria.

Mwanadiplomasia huyo aliekataa kutajwa jina lake ameongeza kusema kwamba wote hao wanahusishwa na masuala ya kijeshi na ukandamizaji wa upinzani nchini Syria.

Hapo mwezi wa Mei Umoja wa Ulaya ilimuongeza Assad na maafisa wengine waandamizi kwenye orodha ya wale waliopigwa marufuku kusafiri kuingia Umoja wa Ulaya pamoja na kuzuiliwa kwa mali zao.
Rais Basher al Assad wa Syria akikabiliwa na kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa na kuzagaa kwa maandamano ya mitaani dhidi ya utawala wake licha ya kukandamizwa kijeshi kwa maandamano hayo ambayo hadi sasa yameuwa zaidi ya watu 1,300,hapo Jumatatu aliahidi kufanya mageuzi katika kipindi kisio kirefu.

Syrien Assad Unterstützer
Wafuasi wanaomuunga mkono AssadPicha: picture alliance/dpa

Lakini waandamanaji na viongozi wa dunia wamepuuzilia mbali ahadi zake kuwa hazitoshi na machafuko yaliendelea tena ambapo watu saba waliuwawa na vikosi vya usalama wakati wa mapambano katika miji miwili kati ya wafuasi wa Assad na waandamanaji.

Uturuki ni nchi jirani na rafiki wa karibu wa Syria. Rais Abdulla Gül wa Uturuki anahisi kwamba Rais Assad angependelea kufanya kitu lakini hasemi bayana ni nini.Rais huyo wa Uturuki ameendelea kusema:

Machafuko hayo ya jana yanafuatia maandamano yalioandaliwa na serikali katika miji kadhaa kumuunga mkono Assad ambaye kwa muda wa miezi mitatu amekuwa kimya ,wakati uasi huo dhidi ya utawala wake wa miaka 11 ulipoanza kwa kuchochewa na maandamano ya vuguvugu la umma yaliozikumba nchi za Kiarabu.

Wanaharakati wanasema watu waliuwawa wakati jeshi lilipoingilia kati kuwasaidia wafuasi wa Assad katika mji wa Homs na mji wa Mayadeen katika jimbo la kikabila la Deir al Zor lilioko kilomita 40 mashariki mwa mji mkuu wa jimbo hilo karibu na eneo la mpaka wa Iraq linalokaliwa na watu wengi wa madhehbu ya Sunni.

Wananchi wengi wa Syria nchi yenye watu milioni 20 ni wa madhehebu ya Sunni na mandamano yenye kudai uhuru wa kisiasa na kukomeshwa kwa utawala wa familia ya Assad wa miaka 41 yamekuwa makubwa kabisa katika maeneo ya miji mikubwa tafauti na katika maeneo yenye kukaliwa na watu wa madhehebu mchanganyiko.

Mwandishi: Mohamed Dahman /reuters
Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed