1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taiwan yasema haitashurutishwa na China

John Juma
10 Oktoba 2021

Taiwan imesema haitokubali shinikizo kutoka China. Rais wa kisiwa hicho Tsai Ing-Wen amesema Jumapili kwamba watalinda demokrasia yao. Haya yanajiri huku ndege za vita za China zikiendelea kuingia katika anga ya Taiwan.

https://p.dw.com/p/41Ui1
Taiwanesischer Nationalfeiertag Präsident Tsai Ing-wen
Picha: Chiang Ying-ying/AP Photo/picture alliance

Wakaazi milioni 23 wa Taiwan, kisiwa ambacho kina mamlaka yake ya ndani, wamekuwa wakiishi kwa wasiwasi wa uwezekano wa uvamizi kutoka China ambayo hukitizama kisiwa hicho kama milki yake na imedhamiria kukidhibiti hata kwa nguvu.

”Kadri tunavyoendelea kupata ufanisi ndivyo tunavyoendelea kupata shinikizo kutoka China,” amesema Tsai kwenye hotuba yake wakati wa kuadhimisha siku kuu ya Taifa ya Taiwan huku akiongeza kuwa: ”Hakuna anayeweza kuilazimisha Taiwan kufuata njia ambayo China imetutengenezea.”

Soma pia: Rais wa China Xi Jin Ping ataka muungano na Taiwan

Tsai amesema msimamo wa Taiwan kidemokrasia ndio utakuwa ngao yake ya kwanza. ”Tunatumai uhusiano wetu na China utaimarika na hatutafanya mambo kwa pupa. Lakini hakupaswi kuwa na fikra kwamba watu wa Taiwan watashurutishwa,” ameongeza kusema hayo.

Sehemu ya vikosi vya jeshi la Taiwan wakati wa gwaride katika maadhimisho ya Siku ya Taifa
Sehemu ya vikosi vya jeshi la Taiwan wakati wa gwaride katika maadhimisho ya Siku ya TaifaPicha: Daniel Ceng Shou-Yi/ZUMA Press Wire/ZUMAPRESS/picture alliance

Pande hizo mbili zimekuwa zikijitawala tofautofauti tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe vya China vilipomalizika mwaka 1949.

Soma pia: Biden amesema Xi amekubali kutii makubaliano ya Taiwan

Lakini mvutano wa sasa umeongezeka zaidi ya kuwahi kushuhudiwa katika miongo iliyopita chini ya rais wa China Xi Jinping ambaye alivunja rasmi mawasiliano na Taiwan kufuatia uchaguzi wa kisiwa hicho miaka mitano iliyopita na pia kukiongezea shinikizo la kisiasa, kiuchumi, kidiplomasia na kijeshi.

Mzozo wa hivi karibuni umesababishwa na ongezeko la ndege za kivita za China kuingia katika sehemu ya ulinzi ya anga ya Taiwan (ADIZ)

Siku chache kabla ya Oktoba 1, ambayo ilikuwa maadhimisho ya Siku ya Taifa ya China, uvamizi ulifanywa zaidi ya mara 150 katika eneo hilo la anga ya Taiwan, hiyo ikiwa idadi ya juu zaidi kuwahi kushuhudiwa. Kulingana na jeshi la Taiwan, ndege tatu za China zikiwemo mbili za kivita zimevuka na kuingia katika eneo hilo siku ya Jumapili.

Rais wa China Xi Jinping
Rais wa China Xi JinpingPicha: Andy Wong/AP/dpa/picture alliance

Rais Xi ameipa suala la kutaka kuidhibiti Taiwan kuwa kipaumbele katika uongozi wake.

Katika hotuba yake siku ya Jumamosi alisema ”ufanikishaji wa muungano wa nchi yetu utatimia na unawezekana.”

Alisema alipendelea mchakato wa amani wa muungano. Hata hivyo matamshi hayo yamejiri baada ya miezi kadhaa ya vitisho vya kijeshi ikiwemo tukio la hivi karibuni la uvamizi katika anga ya Taiwan pamoja na luteka za kijeshi.

Tsai ambaye tayari ameshinda uchaguzi mara mbili anachukiwa na China kwa sababu anaichukulia Taiwan kama ‘taifa huru' na si sehemu ya China.

Hata hivyo hajachukua hatua ya kukitangaza kisiwa hicho rasmi kuwa huru, jambo ambalo Beijing imetahadharisha itakuwa sawa na kuvuka ‘mstari mwekundu' na linaweza kusababisha uvamizi.

(AFPE)