1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Taji ni la City kushinda

1 Machi 2021

Manchester City wameongeza mwanya sasa baina yao na Manchester United walio kwenye nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya England.

https://p.dw.com/p/3q4D0
Champions League I Borussia Mönchengladbach - Manchester City
Picha: Bernadett Szabo/REUTERS

Hii ni baada ya United kuzuiwa sare ya kutofungana na Chelsea hapo Jumapili uwanjani Stamford Bridge. Kocha wa Chelsea Thomas Tuchel ambaye tangu aajiriwe hajafungwa, anasema bado kuna kazi kubwa sana ya kufanya katika kikosi chake.

"Ninaweza kuhisi wazi kabisa nguvu ya timu yangu inapokuwa uwanjani. Ni kundi lenye nguvu, tumeshikamana vyema na tuna washindani katika kikosi chetu na kwasababu hiyo ni vigumu kutufunga. Naamini kwamba mpira ni juhudi za timu," alisema Tuchel.

Na licha ya kuishikilia nafasi ya pili, kocha wa Manchester United Ole Gunnar Solskjaer anasema hiyo haimaanishi hapo ndipo watakapoumalizia msimu.

"Nafikiri bado safari ni ndefu, sidhani kama nafasi zitaamuliwa mapema. Msimu wenyewe pia hautabiriki, tumeona timu zikipitia kipindi kigumu kisha zinapata matokeo mazuri, na pia huezi jua kitakachotokea kutakapokuwa na majeraha na jinsi wachezaji watakavyokabiliana na hali hiyo. Kwa hiyo kwangu mimi kila mechi ni muhimu," alisema Solskjaer.