1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Takriban raia 20 wauawa katika shambulizi nchini Kongo

Tatu Karema
26 Januari 2024

Takriban raia 20 wameuawa katika shambulizi lililotokea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Alhamisi. Haya yamesemwa na jeshi la nchi hiyo na waasi wa kundi la M23

https://p.dw.com/p/4bguJ
Mwanajeshi wa kikosi cha kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ashika doria karibu na lori linalobeba bidhaa za kijeshi nchini Kongo
Mwanajeshi wa kikosi cha kanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ashika doria nchini KongoPicha: Arlette Bashizi/Reuters

Shambulizi hilo lilifanyika katika mji wa Mweso eneo la Masisi umbali wa takriban kilomita 80 kutoka mji wa Goma katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Maelezo ya pande husika yakinzana

Katika taarifa, jeshi limesema kuwa waasi hao wa M23 walirusha mabomu kuelekea Mweso wakati walipokuwa wakirudi nyuma kuepuka operesheni ya kijeshi dhidi yao.

Soma pia:Mapigano kati ya kundi la M23 na Wazalendo yazua hofu Kongo

Kwa upande wake, kiongozi wa M23 Bertrand Bisimwa, amelishtumu jeshi hilo kwa kutumia droni na silaha nzito kushambulia maeneo ya makazi katika mji huo wa Mweso.

Soma pia:M23 wakamata mji mashariki mwa Kongo

Katika taarifa aliyochapisha katika mtandao wa X, Bisimwa amesema mashambulizi hayo yamewauwa watoto, wanawake na wanaume na kuharibu nyumba, makanisa na shule.