1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

TAKUKURU yawachunguza watumishi wa Muhimbili kwa hujuma

Hawa Bihoga13 Januari 2021

Taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa nchini Tanzania TAKUKURU, inawachunguza watumishi zaidi ya 20 wa Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili MOI, kwa kuhujumu mfumo wa ugavi na kusababisha hasara ya shilingi bilioni 1.2.

https://p.dw.com/p/3nsHh
Tansania Sitz der Wahlkommission Takukuru in Dodoma
Picha: DW/S. Khamis

Taasisi hiyo imetoka hadharani mapema leo kuzungumza na waandishi wa habari ikiwa ni takriban miaka miwili hujuma hizo zimekuwa zikifanyika katika mifumo rasmi ya serikali kwa kuandika taarifa za uongo, kwa kuweka idadi kubwa ya vifaa ama dawa zilivyotolewa kwa mgonjwa tofauti na idadi halisi iliyoelekezwa na daktari.

Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo amewaambia waandishi habari kuwa, kwa kushirikiana na uongozi wa taasisi hiyo inayohudumia watu hata kutoka mataifa ya jumuia ya Afrika Mashariki na yale ya jumuiya ya maendeleo ya mataifa ya kusini mwa Afrika, SADC, walibaini kuchepushwa kwa dawa hizo katika mifumo rasmi ya kutunza taarifa za kumbukumbu katika utoaji wa dawa na vifaa tiba.

"Tunapenda tuufamishe umma juu ya uchepushaji wa dawa zenye thamani ya bilioni 1.2 ambazo zilichepushwa au kuhujumiwa kwa manufaa binafsi na watumishi wa kitengo cha famasia katika taasisi ya tiba ya mifupa hospitali ya taifa Muhimbili MOI," alisema Jenerali Mbungo.

Mbali na kufanya ubadhirifu huo ambao kwa kiwango kikubwa unatajwa kuwaathiri wahitaji pale wanapohitaji huduma, kadhalika walitumia mbinu kama hizo katika kuongeza gharama za matibabu tofauti na bei elekezi iliyotolewa na serikali katika kuwahudumia wagonjwa hatua ambayo inatajwa kuleta usumbufu kwa baadhi ya wateja.

Krankenhaus in Tansania
Lango la kuingilia eneo la mapokezi katika hospitali kuu ya rufaa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.Picha: DW/K. Makoye

Mamlaka hiyo huru imesema tayari imedhibiti mfumo huo rasmi wa ugavi na watuhumiwa hao wanaedelea kuhojiwa na uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mbele ya sheria.

"Wafamasia walikuwa wanasababisha upotevu wa dawa kwenye mfumo ambao unaonesha mgonjwa kachukua dawa na wanazidisha kwa zaidi ya mara mbili hadi tatu jambo ambalo hata lingefanyika kwa makosa basi ingesababisha madhara kwa wagonjwa.”

Hata hivyo, baadhi ya wananchi ambao wamewahi kupata huduma katika kitengo cha MOI wanasema kuna haja ya mamlaka zingine kuelekeza jicho la ziada katika taasisi hiyo ili kustawisha zaidi huduma za kitabibu ili kuvutia wahitaji wengi kutoka mataifa mengine na hata kuendelea katika hatua ya utalii wa kimatibabu.

"Isiwe Takukuru tu na taasisi zingine ziweke macho huenda kuna mengi zaidi na endapo yataondolewa tutafanya vizuri kwenye tiba hata kuwa mfano kwa wenzetu," alisema mkaazi wa Dar es Salaam Rocky Mansoul.

TAKUKURU imefanya uchunguzi huo ikiwa ni oparesheni maalum ya ufuatiliaji na urejeshaji wa mali za serikali na wananchi wanyonge, kulingana na sheria inayoongoza mapambano dhidi ya rushwa na katika kipindi cha miezi sita tayari wameokoa kiasi cha fedha shilingi bilioni 14.4.